Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia kwenye hoja iliyoko mbele yetu taarifa ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti kuhusu utekezaji wa shughuli zake katika kipindi kuanzia mwezi Januari, 2016 mpaka Januari, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi ni Mjumbe wa Kamati hiyo ya Bajeti na kwa kipindi hiki chote tulikuwa tukifanya kazi pamoja kuhakikisha bajeti yetu inakwenda vizuri hasa zaidi katika jukumu letu la kutaka kuisimamia Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake. Kwanza kabisa Kamati yetu imekutana na changamoto nyingi sana; na Mheshimiwa Mwenyekiti wakati anawasilisha taarifa yake tumeona na karibu Kamati zote zilizokuwa zinatoa hapa taarifa zake wamekuwa wakilalamikia kuhusu jambo hili, kukosekana kwa mafunzo kwa visingizio kwamba hatuna bajeti ya kutosha kwenye kufanya shughuli hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali ya kushangaza kabisa, Kamati ya Bajeti kama ulivyosema ndio kubwa hasa na inayosimamia mustakabali mzima wa nchi yetu hasa zaidi kwenye mapato na matumizi, lakini tunakosa mafunzo ya kutosha, Ofisi ya Katibu, pia Ofisi ya Spika haijaipa Kamati hii kipaumbele kuhakikisha kwamba tunajua majukumu yetu ya msingi, kwa kuwa exposed kwenye maeneo mbalimbali na ukizingatia tulio wengi kule ndani ni wageni ambao tunahitaji hasa na sisi siyo wataalam wa mahesabu katika hali kubwa. Kwa hiyo, Bunge hili lione sasa kuna haja ya lazima kabisa ya kuhakikisha Wajumbe wa hii Kamati wanapata mafunzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tuna changamoto kubwa sana kutoka kwenye Wizara mbalimbali hata Wizara ya Fedha yenyewe, kumekuwa na usiri mkubwa sana wa kupatiwa hizi taarifa. Utakuta tunakwenda kwenye vikao, tumebakisha muda mchache kuanza vikao vyetu ndipo taarifa zinapokuja ambazo wanataka sisi tuweze kuchangia na kutoa mapendekezo kwa Serikali. Kwa hiyo, tuombe tuwe tunapata taarifa kwa wakati ili tuweze na sisi kuzipitia vizuri tuweze kutoa mapendekezo yetu kwa Serikali. Kama unavyofahamu jukumu letu ni pamoja na kusimamia suala zima la Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hapa inajadiliwa kwamba kuna ukuaji mkubwa sana wa Deni la Taifa. Siyo siri kwamba Deni la Taifa linakuwa na hasa zaidi deni la ndani limekuwa likikuwa kila mara, hii inadhoofisha sana sekta binafsi kwenye kupata mikopo. Kwa sababu Serikali nayo sasa imekuwa ikishindana na wafanyabiashara wadogo wadogo, Serikali imekuwa ikishindana na wamachinga na watu wengine kuweza kupata mikopo katika mabenki yetu ya kibiashara. Kwa sababu Serikali wana nguvu kubwa sana, wao ndiyo hasa wanaopendelewa na inaonekana hili jambo linafanywa kama maagizo maalum kwamba Serikali ipewe kipaumbele cha kukopeshwa.
Hivyo, tunazuia mzunguko wa pesa wa kawaida kabisa hapa ndani kwetu na ndiyo maana sasa tunaanza kuona inflation zinapanda. Wafanyabishara wanashindwa kulipa madeni yao, kwa sababu sasa hivi hawakopeshwi tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi tunaona wanafilisiwa kama tulivyosikia kuna wafanyabiashara wazabuni wa Serikali, kuna Wazabuni ambao walikuwa wamekopa na wanafanya shughuli na majeshi, tunaona watu hawa wanashindwa kulipa madeni yao kimsingi na hawawezi kukopesheka tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeacha jukumu lake, Serikali ni jambo kubwa sana, ilitakiwa itoe mikopo yao nje ya nchi kuja kuleta Tanzania, kuja kuongeza mzunguko wa pesa katika nchi yetu na katika mzunguko wetu wa kawaida kabisa wa pesa. Sasa hivi tumeona nao kwa sababu ya kutokutekeleza majukumu yao ya msingi, kutokufuata masuala ya utawala bora na sheria wameamua nao wawe wanakopa hapa ndani, kiasi kwamba wanazuia mzunguko wa pesa, na kufanya pesa iwe na mzunguko mdogo (circulation of money).
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaona wanakwenda kukopa au kuchukua pesa kwenye mifuko, kiasi kwamba wastaafu wanashindwa kulipwa pesa zao kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekuwa wakizungushwa, tunafahamu hapa katikati kuna ma- DAS, kuna ma-DED ambao kabisa ni Watumishi wa Serikali wanashindwa kupata pension zao. Mifuko ya PPF, NSSF tumeanza kuona sasa wanashindwa kuwalipa watumishi kwa sababu tu pesa nyingi zimechukuliwa tena na Serikali, Serikali inashindwa kuzirudisha pesa zile kwenye mzunguko, matokeo yake wanakwenda kugharamia vitu ambavyo viko nje ya bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi pesa hazitoki mfukoni kwa mtu mmoja, hazitoki mfukoni kwa Mheshimiwa Rais, hizi pesa ni zile ambazo sisi tunazikusanya, badala ya kwenda kufanya majukumu tuliyoyapangia kibajeti, zinakwenda kufanya kadri ya mahitaji ya Mheshimiwa Rais, na kwenda kufanya kadri ya mahitaji wa viongozi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuziachie pesa zizunguke, watu waliostaafu wapewe sasa haki yao, kwa sababu tunajua baada ya kustaafu watu wana muda mfupi tu wa kuweza kuishi hapa duniani, basi wapewe pesa zao kwa wakati wazitumie wanavyotaka wao, badala ya kwenda kugharamia miradi ambayo siyo ya kibajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia kuna madeni ya majeshi, watumishi wa jeshi tuliondoa hapa masuala ya kodi kwenye vifaa mbalimbali wanavyotumia kwenye maduka ya majeshi, lakini wakasema pesa hizo wataongezewa kwenye masurufu yao, pesa hizo wataongezewa kwenye mishahara yao. Sina uhakika mpaka kufikia leo ni shilingi ngapi zimepelekwa kwenye majeshi kwa ajili ya ku-subsidize ile kodi ambayo ilikuwepo walikuwa wanalipiwa mwanzo na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mwenyekiti wa Kamati anatoa taarifa hapa na wote tunafahamu kwamba Serikali iliamua kujikita kutoa asilimia 40 yote iende kwenye shughuli za maendeleo, lakini hapa tumesikia katika ripoti na hii kila mtu anaifahamu, hakuna reflection hauwezi kuona hali halisi ya kilichofanyika sasa hivi. Hakuna tofauti wakati huo asilimia 40 ya maendeleo iliyopo sasa hivi na asilimia zile ndogo ambazo zilikuwepo siku za nyuma. Pesa za maendeleo hazifiki kwa wakati kwenye maeneo yanakotakiwa kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashindwa kuelewa tunajitangazia kwamba tunakusanya pesa nyingi sana kwa ajili ya shughuli za maendeleo, nchi yetu iweze kufanikiwa kuvunja hapa rekodi, ukiangalia hapa kwenye baadhi ya kurasa inaonyesha kabisa wazi kwamba zimekusanywa pesa nyingi sana, lakini kimsingi pesa hizi haziendi ku-reflect maisha halisi ya wananchi wanayoyaishi mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaanza kuhisi kwamba hata inflation inapanda mzunguko wa pesa umekuwa mdogo. Serikali inasema inapeleka pesa za maendeleo, maendeleo hayo kwa sasa hivi kwa kweli hatuyaoni. Halmashauri zimekuwa zikilia njaa, hakuna mtu anayeweza kutekeleza wajibu wake, miradi mingi imesimama, pesa nyingi ndiyo tunatambua inakwenda kulipa madeni mbalimbali lakini kimsingi mzunguko wa pesa umeondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye ukurasa wa 43 wa hii taarifa tuliyonayo hapa, mpaka leo Serikali bado inang‟ang‟ana na vyanzo vilevile vya mapato vya asili wakati ilifanyika tafiti na Mheshimiwa Chenge wewe ndiye ulikuwa Mwenyekiti wa tafiti hizo, ukapendekeza vyanzo vipya vya mapato Serikalini, lakini Serikali hii tunayoiita sikivu mpaka sasa hivi bado imeshindwa kutumia vyanzo vipya vya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea tuendeshe nchi yetu kwa kulipia kodi au kuongeza kodi za sigara kila mara, si ajabu utakuja kuona bajeti ijayo sigara inapandishwa tena bei, soda, bia zinakwenda kupandishwa bei na vinywaji vingine lakini huu siyo msingi wa kweli, kama nchi inataka kusimama, kama nchi kweli inataka kuendelea tutegemee vyanzo hivi kila mara. Kulikuwa kuna mapendekezo mazuri kabisa ya vyanzo vipya vya mapato, lakini Serikali imeendelea kudharau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifikiri sasa Serikali hii itaamua kuchukua vile vyanzo na kuamua kuvifanyia kazi, lakini tunaona hapa Kamati inaleta taarifa yao. Tunatakiwa sasa kukamilisha tathmini ya ukusanyaji wa mapato kupitia Bahari Kuu, hiki chanzo ni kizuri sana cha mapato lakini hakijaanza kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa tunatakiwa tuanze sasa hivi kuongeza vyanzo vipya vya mapato. Tuseme kwamba Shirika la Umeme halizalishi vizuri umeme wake, kwa hiyo tuende tuanze kuipa nguvu zile sehemu mbalimbali ambazo zinataka kuzalisha umeme. Kwa mfano, watu geothermal, kuna umeme wa upepo, kuna watu wanataka kutumia hizi solar energies, tuanze kuona sasa hivi viwe vyanzo vingine vya kuweza kuongezea Serikali mapato na TANESCO iende kulipa deni lake sasa ili kimsingi watu uzalishaji uongezeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona tatizo kubwa sana la umeme hapa Mkoa wa Mtwara sasa hivi linatokea na hili jambo linatokea ni kwa sababu ya kung‟ang‟ania chanzo kimoja cha umeme. Wilaya nzima au Mkoa zima wa Mtwara kuna tatizo kubwa sana la umeme tuwaongezee wale watu nguvu ili waweze kuzalisha sasa na waweze kuchangia vizuri kwenye pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana niseme tu kwamba pamoja na Kamati kuleta taarifa zake hapa mbele, lakini siyo kila mara Kamati hii haionekani kuwa ni kipaumbele, wakati ina jukumu kubwa la kusimamia mchakato mzima wa bajeti toka mwanzo wake mpaka pale tutakapomalizia. Kwa hiyo, kifupi niseme tunaomba tafdhali kwamba sasa hivi mependekezo yale yaliyotolewa na Kamati ya Chenge, vyanzo mbalimbali vya mapato vianze kuwa adopted. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hapa karibuni kuna utaratibu umeanza wa kukata pesa kwenye miamala, hili jambo linaumiza sana Watanzania, hili jambo linaumiza wananchi wote tulifikirie tena upya ili kuwe kuna thamani halisi ya matumizi ya zile pesa shilingi 1,000 basi ipate thamani yake, shilingi 500 basi ipate thamani yake. Lakini tunakwenda kwenye miamala ya kibenki tuona gharama zimeongezeka, tunakwenda kwenye miamala ya simu, tunaona kule gharama zimeongezeka, hivi vitu vyote havileti picha nzuri kwa wananchi. Kwa hiyo, tufikirie vyanzo vingine vya mapato, kwa sababu vyanzo vya kawaida hivi vya kodi vimeshindwa kabisa na vimekuwa kama ni traditional sources of income to the government. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona sasa hivi mpaka polisi tunaanza kuwaingiza na wenyewe ili waanze nao kuwa ni source of income ya Serikali, hili jambo siyo jema tufikirie vyanzo vile ambavyo Mheshimiwa Chenge wewe kwa nafasi yako ulishauri kabisa Serikali. Kama walikuwa hawana haja ya kutaka kulisikia kusingekuwa na haja ya kutumia pesa nyingi kuipa ile Kamati iliyoanza kufikiri kuhusu hivi vyanzo. Asante kwa kunipa nafasi.