Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Salma Mohamed Mwassa

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii lakini vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na mimi niweze kuchangia ripoti hii ya Kamati hii ya Bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nijielekeze kwenye ukusanyaji hafifu wa mapato. Kwa kiasi kikubwa kabisa ukiangalia kwenye taarifa hii ya Kamati imeonesha kwamba ukusanyaji hafifu wa mapato umeathiri bajeti kwa kiasi kikubwa. Tuangalie kwa mfano kodi ya majengo kwenda TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukusanyaji hafifu wa mapato kwanza unasababishwa kwa kiasi kikubwa na Serikali Kuu kuingilia hizi Halmashauri zetu au Serikali ya Mitaa hata kwenye vyanzo vyao wanavyovibuni na kuviona kwamba sasa vinakua badala ya kuwapa moyo zaidi na kuwasimamia katika sera wanavipora vile vyanzo kama kodi ya majengo na kuvipeleka Serikali Kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, Kinondoni, Temeke, Ubungo zilikuwa zinafanya vizuri sana katika kodi hii ya majengo na ndiyo uti wa mgongo wa Halmashauri zetu lakini leo imepelekwa TRA hakuna hata mia iliyokusanywa. Wakati mwaka jana ukiangalia takwimu kwa mfano Manispaa ya Kinondoni imekusanya zaidi ya shilingi bilioni tisa kwa mwaka na ilikuwa ina uwezo wa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 800 mpaka shilingi bilioni moja kwa mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna miezi nane toka kodi hii ihame kutoka kwenye Halmashauri kwenda TRA, TRA haijaleta hata senti tano kwenye Halmashauri. Unategemea huo utekelezaji wa bajeti utafanyika kwa kiasi gani wakati Serikali Kuu ndiyo chanzo cha kuvuruga hizi kodi badala ya kuzisimamia. Miaka miwili tu iliyopita kodi hii ilikuwa kwenye Halmashauri na ilikuwa ina perform vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi, kodi hii ni kodi ya local, inatakiwa ikusanywe kule kwenye local level na sio kodi ya central level hii. Ukiipeleka kodi ya majengo kwenye central level unaharibu mpango mzima kwa sababu kodi hii inatakiwa ikusanywe kwenye mitaa. Kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali ingeandaa mfumo mzuri kuzisimamia Halmashauri ili kwamba wale Wahasibu wa Halmashauri waende kwenye mitaa na zile mashine za EFD wakusanye ile kodi ya majengo kutoka kule kwenye local level sio kwenye central level huku kwenye TRA ambayo kwanza akienda tu pale mwananchi wa kawaida anaulizwa, una TIN, majina yako matatu, sijui mfumo wa nini, yaani TRA kwa kifupi haina uwezo mzuri wa kukusanya kodi ya majengo kama ilivyokuwa kwa Halmashauri, tume-prove failure kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano sasa hivi ni miezi nane, miezi nane unajipanga vipi? Unajipanga mwezi wa kwanza, mwezi wa pili, wa tatu, mpaka miezi nane hujakusanya hata senti tano? Wakati Halmashauri yenyewe ilikuwa ina uwezo wa kukusanya kati ya shilingi milioni 800 mpaka shilingi bilioni moja kwa mwezi, wewe unajipanga nini? Wamechukua ma-valuer wa Halmashauri kuwapeleka TRA, wamechukua mifumo kutoka kwenye Halmashauri, majengo mengi kwa asilimia kubwa yamethaminiwa, kwa nini mpaka sasa hivi hawakusanyi, ina maana wameshindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge lako Tukufu lisimamie hii kodi irudi tena kwenye Halmashauri. Halmashauri zinakufa! Hii kodi ndiyo uti wa mgongo wa Halmashauri, Halmashauri zime-paralyze kwa sasa, hazina chochote kutokana na kuwanyang‟anya hii kodi yao na hiki ndiyo chanzo kikubwa cha mapato. OC zao kwa asilimia kubwa zilikuwa zinatoka kwenye kodi ya majengo. Kwa hiyo, naomba kabisa kwa miezi hii minane itoshe kutathmini kwamba TRA ni kama imefeli kukusanya kodi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nijielekeze kwenye kukopa zaidi ndani. Naishauri Serikali kwamba, ni vizuri tukatoka sasa kwenye wigo huu wa kutegemea mikopo ya ndani na tukaangalia kujenga mahusiano zaidi nje. Kukopa zaidi ndani, tuwaachie hawa sekta binafsi, lakini sisi kama Serikali tupunguze kukopa zaidi ndani, tukope nje ili tupate wigo wa kupata fedha za kigeni na kuja kuzisambaza ndani na uchumi uendelee kukua. Sisi kama Serikali ambao tuna uwezo wa kukopa nje kirahisi, tukiendelea kukopa ndani: Je, mwananchi mdogo atakakopa wapi? Kwa hiyo, tutaendelea kuudumaza uchumi wetu na hatutaweza kufikia lile lengo tulilojiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niende kwenye mada ya ukuaji wa uchumi kutokumfikia mwananchi wa kawaida. Kwenye ukurasa wa saba ripoti ya Kamati ime-quote kabisa, “pato la mwananchi wa kawaida bado ni dogo sana na asilimia kubwa ya wananchi wetu wanaishi kwa kipato cha chini ya dola moja za Kimarekani.” Nimemsikia Mbunge mmoja hapa anakana kabisa, hivi kweli sisi tunaotegemewa na watoto, sijui na akina nani, hivi kweli tungekuwa tunaishi kwa dola moja tungeweza? Kwa hiyo, ina maana unapingana na ripoti ya Kamati? Sijamwelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaishi chini ya dola moja kwa siku kwa sababu tu, sisi kwa ujamaa tuliojengewa toka huko nyuma na Hayati Mwalimu Nyerere kwamba huyu mwingine akiwa hiki, tunasambaziana; lakini ni ukweli kabisa tunaishi chini ya dola. Usibishe! Mheshimiwa Mbunge wewe tu kwa sababu tu maisha yako yako vizuri, uko hapa, lakini wananchi huko nje wanateseka. Sasa sisi tunaona tu uchumi unakua, unakuaje? Mbona hatuoni kwenye maisha halisi ya Mtanzania kwamba uchumi unakua! Sasa hizi taarifa tunazoambiwa kwamba uchumi unakua, unakua wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokukua kwa uchumi kwenye level ya chini inasababishwa na Halmashauri zetu zinaposhindwa kusambaza ule utajiri chini ya wananchi wake kutokana na kuingiliwa, mara hivi; wakiendelea kukusanya vitu vyao, wanaingiliwa, mara hivi. Kwa sababu huwezi ukawa Serikali Kuu kule juu ukapata maisha ya Mtanzania halisi. Maisha ya Mtanzania halisi yanapatikana huku chini kwenye Halmashauri. Kwa hiyo, Halmashauri zipewe uwezo, zitungiwe sera. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kikubwa cha kufanya, Serikali Kuu isimamie sera za kwenye Halmashauri. Siyo kuona kama, sasa hivi Halmashauri zime-perform kwa kiasi kikubwa kwenye chanzo hiki, inapora. Badala ya kubuni vyanzo vyao, wao wanatafuta tu kwamba chanzo hiki ipore iende kupeleka Serikali Kuu. Hii siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye hoja ya wahisani kutokuleta pesa kwa wakati. Kwanza tujiulize, kwa nini wahisani washindwe kupeleka pesa kwa wakati kipindi hiki? Kama Serikali tufanye tathmini kwa nini mpaka leo wameleta tu asilimia 16 na wakati ilitakiwa walete 36? Kwa hiyo, tujiulize ni nini hasa? Kama wao walikuwa marafiki zetu wa karibu tu, lakini leo hawana hata sababu na ripoti ya Kamati inasema, hata wao hawakuambiwa sababu ni nini. Yaani hawana sababu zinazokwamisha. Sasa kwa nini hamna sababu? Inawezekana sababu zimejificha huko kwa ndani, lakini hamzisemi. Nadhani tujitathmini upya. Je, tuna mazingira rafiki na wenzetu? Kwa sababu sisi tumejifungia hapa kisiwa. Hatusafiri kwenda ku-interact huko nje, wafanyakazi wa Serikali wamekuwa blocked, hawaendi huko nje. Sasa hao wahisani, huo urafiki tunaujenga wapi?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli kwenda kuomba kwa mwenzako si lazima kwanza uende wakuone ndio uende kuomba! Unaomba ukiwa hapa, utaweza? Hawa wahisani tujenge mazingira mazuri kule, internationally. Sisi Wabunge tusafiri tuka-interact kule, ili tukienda kule kwa Wabunge wenzetu, tunawaambia jamani sisi bwana wenzenu twafa huku. Hivi na hivi tuambieni. Eeeh, sisi hatuna huku hivi na hivi! Mahusiano Kimataifa ni madogo. Serikali hii ya Awamu ya Tano ijitafakari upya, tutoke. Wabunge wenyewe hapa hatusafiri; sasa kama hatusafiri tutaendaje kuomba kwa wenzetu? Utaomba vipi wewe usaidiwe huku wakati huendi kule kwa mwenzako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo, tuangalie tena kwa nini hii misaada imekuwa midogo? Tutoke tuanzie na Mheshimiwa Rais, atoke; sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge tutoke, wafanyakazi wa Serikali watoke, wote; yaani isiwe ile kubana bana sijui kitu gani. Tutoke huko tukaombe! Sisi hatuwezi kujitegemea wenyewe hapa! Eeeh, tutoke, Mawaziri wenyewe watoke vilevile wakaangalie hata wenzao kule wanafanya nini kwenye Wizara zile. Tokeni hii misaada tuipate tena. Mbona mwanzoni huko ilikuwepo! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru kweli Mheshimiwa Rais Kikwete, alikuwa anatoka sana. Mbona mambo yalikuwa sawa! Eeh, tutoke. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mambo ya ukame kuhusu chakula. Nakumbuka kabisa kwenye ndani ya Bunge lako hili, kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walilalamika kwamba mazao ya chakula yanaoza, hapa hapa ndani ya Bunge hili. Sikumbuki ni kikao kipi lakini akiwemo Mheshimiwa Keissy alikuwa analalamika kabisa; mazao yanaoza, hayanunuliwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii NFRA haipewi fedha za kutosha kununua chakula cha kuhifadhi na ndiyo maana leo Waziri wa Chakula anasema Halmashauri 55 zina upungufu wa chakula lakini hazina njaa; hivi hiyo si ni lugha tu! Yaani upungufu wa chakula na njaa, maana yake nini? Eti hazina njaa, lakini zina upungufu wa chakula. Sasa ndiyo nini? Mimi sijaelewa hapo, labda niombe kufafanuliwa zaidi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kabisa Serikali, sasa hivi tuendelee kuambiana ukweli kwamba hii mamlaka hii tumeiunda wenyewe, ipewe hela za kutosha inunue. Kama mahindi yapo Kibaigwa, basi yapelekwe Songea, yasambazwe kwenye magodauni yao ya mikoa ili hili janga la ukame na njaa lionekane kama linaweza kuepukwa, tujikidhi kwa mahitaji ya chakula kilichopo. Kwa mfano, kama hivi matetemeko, ingeku…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)