Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza niwapongeze Kamati ya Bajeti kwa ripoti yao nzuri na kwa kweli vitu vingi wamevielezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongea machache. Moja, ni deni la Taifa. Naamini, nilisema wakati wa bajeti na leo naomba nirudie tena. Kama kuna eneo ambalo tusipolisimamia vizuri juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, hatutaziona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila unapoongelea deni la Taifa, tunaambiwa deni letu ni himilivu (sustainable) kulingana na viwango vya Benki ya Dunia na IMF. Naomba tufikiri tofauti kidogo. Deni hili tunatumia GDP kujua kama deni la Taifa linahimilika. GDP ni sawa, ndiyo mali zote tulizonazo, zinajumlishwa, halafu unaangalia percentage ya deni ulilonalo. Unapoanza kulipa deni, hutumii ile GDP sasa, unalipa deni kutoka kwenye mapato yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakusanya kila mwezi ukishakusanya, first charge mshahara, first charge, deni la Taifa. Wizara ya Fedha watatuambia, tumefika sasa tunakusanya makusanyo; asilimia 86 ya makusanyo yanaenda kwenye mshahara na deni la Taifa. Maana yake ni nini? Hatutapeleka hela kwenye maendeleo. Kwa hiyo, lazima tubadilike; tunapotaka kuliangalia deni letu, tuli-peg na revenue base yetu. Tukifanya hivyo, tutaweza kwenda huko tunakotaka kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye deni la Taifa, tumeshafika hapa. Hilo la kubadilisha namna ya ku-calculate, tuamue sasa kama Serikali, tutumie revenue ratio ili tuweze kujua tunaweza ku-manage deni la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo litaleta shida, mikopo yote ambayo tumeichukua, hasa ile ya kwenye mabenki, kuna kitu kinaitwa floating libor, wakubwa wanaenda kukopa kwenye mabenki wanatuambia chukua floating libor kwa sababu kwa hii inaweza interest zikashuka ama zikapanda; lakini trend imekuwa, ni interest zinapanda. Kwa sababu huwezi ku-control wewe. Ikishakuwa floating libor huwezi ku-control wewe, mwezi kesho unalipa nini kwenye interest rate? Anaye-control ni bwana mkubwa Marekani. Reserve Bank ya Marekani mwaka 2016 imeongeza kutoka 0.25% to 5%. Maana yake nini? Interest zetu nazo zikapanda. So we are here tumekaa, tunasubiri the mercy ya wengine. Lazima twende kama wanavyofanya wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti nilisema nikajiwa hapa, kwamba unachosema sawa, lakini nahitaji a complicated work force. Hii complicated ya wapi? Duniani wanafanya, kuna kitu kinaitwa swap interest rate. Ukifanya swap, utalipa kingi mwezi wa kwanza, baada ya pale, interest yako unayoilipa inakuwa ni constant kila mwezi. Kwa hiyo, kama Taifa, utakuwa unajua kila mwezi ni shilingi ngapi nalipa kwenye deni la Taifa. Leo hii tukimwuliza Waziri wa Fedha, mwezi kesho atalipa shilingi ngapi kwenye deni la Taifa, hajui kwa sababu sio yeye anaye-control. Ni uchumi mwingine ndiyo una-control kwa sababu tu tumekwenda kwenye floating libor.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kinachotokea? Wanakuja wale wenye mabenki wanakwambia ukienda kwenye floating libor interest rate mwezi wa kwanza utalipa 0.1% au 1.3%, lakini ukienda kwenye fixed anakwambia itakuwa ni 1.75%. Kwa hiyo, wewe as a country una-save kwenda kwenye 1.3%! Uliza mwezi wa Pili, mwezi wa Tatu au mwezi wa Nne inakuwaje? Unakwenda kila mwezi unaongezeka, utatoka 1.3% mpaka 5%, lakini yule aliyelipa 1.75% ataendelea kulipa hiyo mpaka mwisho wa hilo deni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya tunayoyasema wenzetu wamefanya, sisi sio wa kwanza. Nawaombeni sana watu wa Wizara ya Fedha, tufike sehemu tufikiri tofauti kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni suala la investment model ya growth ya economy yetu. Naomba sana Serikali, tusirudi tulikotoka miaka ya nyuma. Nawaombeni sana. Wenzetu wote wanakwenda kwenye private sector ndiyo engine ya growth. Tukidhani Serikali hii inaweza ikafanya kila jambo, nawaambia hatutafanikiwa. Mwalimu Nyerere alifanya hapa, alijenga kila kiwanda, leo viko wapi vyote? Kwa sababu, mambo haya ya viwanda, mambo haya ya investment, lazima uingize hela kila wakati. Siyo kila wakati utapata faida! Kitakachotokea leo utapata hasara, kesho unafanyaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zilizoendelea hivi karibuni baada ya miaka ya 60, nchi kama Malaysia wanatumia hela za watu kufanya uwekezaji. Wewe unachotaka kama nchi, unataka huduma. Nchi inataka umeme megawati 5,000; kuna mtu anaweza akaleta fedha zake akaweka umeme, shida yetu ni nini kumpa? Ni lazima kila kitu kifanywe na TANESCO? Mtu anataka kujenga barabara kutoka Dar es Salaam; Swiss Dual Carriage, mpaka Dodoma, aweke road toll, sisi hatutaki. Maana yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongea habari ya PPP, tumeweka Sheria, lakini soma Ripoti za Wizara ya Fedha; kama kuna jambo hawana interest ni suala la private sector. Private Sector ni wezi hawa. Naomba sana tubadilishe mentality ili twende kwa kasi. Kwa kasi ya Rais Magufuli, tukimsaidia tukaanzisha miradi ya private sector tutaenda kwa kasi sana ya maendeleo. Naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa bajeti tulisema kuhusu bei ya mafuta. Niliwaambia jamani eeh, bei ya mafuta duniani inapanda na wenzetu wana-hedge na hata Kenya wame-hedge, kwa nini sisi hatu-hedge? Watu ni kama vile tunaongea, tunayaacha hapo hapo. Ilikuwa wakati ule ni dola 44 per barrel, leo inakaribia dola 60 per barrel, tuko hapa hapa! We are at their mercy, tumekaa tunasubiri tu. Kwa hiyo, inaweza ikapanda mpaka ikafika 100, wakishakuja wanakwambia, unajua viashiria vya mwaka huu, bei ya mafuta duniani inapanda; lakini inapanda ukiwa unaangalia. Naomba watu wa sera wa Wizara ya Fedha mtusaidie. Vitu hivi wenzetu wanafanya, haiwezekani sisi tusifanye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kilimo. Naomba sana, kilimo chetu tumelima namna hii miaka 50, karibia 60 ya uhuru tunaendelea kulima namna hii. Mvua ikitetereka kidogo tunaanza kupiga kelele. Ni kwa sababu hatu-embrace commercial farming. Naomba tu-embrace commercial farming, ndiyo itakayotutoa hapa kwenda mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano rahisi wa commercial farming ndugu zangu, twende Zimbabwe. Bwana mkubwa yule wa Zimbabwe aliamua akafukuza wale Wazungu kwa sababu ya uzalendo wa ardhi, leo wanakufa njaa. Maana yake nini? Kilimo kinahitaji uwekezaji mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongea habari ya pembejeo hapa, mwaka huu pembejeo hakuna. Tumetoka shilingi bilioni karibu 80, mwaka huu tumeweka shilingi ngapi za pembejeo? Tunatarajia kupata nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kutoka hapa, ni lazima tuone namna bora tuwe na mashamba haya ya akina mama yake na Peter, ambayo wanalima miaka yote hawajawahi kujitosheleza, lakini tuwe na mashamba ya mabwana wakubwa wenye fedha ambao watajitafutia wagani wao, watanunua pembejeo za kwao, wataweka umwagiliaji, watatafuta mbegu bora, hawatasubiri Serikali. Hapo kama Taifa, tutatoka hapo tulipo, tufike tunapokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongea habari ya viwanda, tunaingiza mifuko ya jamii kwenye viwanda. Tuwe waangalifu sana. Tukizubaa mifuko hii tutaipoteza. Nilidhani mifuko iingie kama kuweka mtaji, shughuli ifanywe na wengine, lakini mkitaka waingie wafanye wenyewe, nawaambieni wataanza ku-provide losses hapa, tutashangaa baada ya miaka michache ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote hawafanyi. Wanachofanya, wanaingiza kwenye investment program. Kama Ilovo anaweza akalima shamba, ana uwezo wa kutengeneza sukari, unanunua mtaji, unaweka hela kule kwa sababu yeye ana ile experience. Tukiamua kufanya wenyewe, muwe na hakika tutakuja kuulizana hapa siku moja. Tuko tayari kuzibeba losses hizo? Kwa sababu, biashara ina faida na losses. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni mabenki yetu. Nawaomba sana, suala hili la Financial Sector tuwe waangalifu sana. Quarter ya pili, karibu benki 15 zime-provide loses. Majibu tunayopewa inawezekana ni majibu sahihi, lakini twende mbali zaidi tujiulize: Je, ni sahihi kwa uchumi wetu? Money supply kwenye market imepungua. Mwaka jana 2016 ni 4.6% wakati mwaka uliopita 2015 money supply ilikuwa almost 14.6%. Maana yake ni nini? Hela imetoka kwenye money supply. Kwa hiyo, hii ni shida. Lazima uchumi uende unaongeza, unatoa, unapunguza, then ndiyo tuta-stabilise.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua wanafanya kazi nzuri sana. Kamati imetuletea mapendekezo mazuri sana; ni matarajio yangu kwamba mapendekezo haya Serikali itaenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kusema, nawaombeni watu wa Hazina twendeni tukafanye analysis proper kuhusu deni la Taifa. Tusiposimamia deni hili, muwe na hakika mtakusanya kwa juhudi kubwa, hela yote inakuja inakwenda kulipa deni, maana kulipa ni lazima. Tunasema tunaenda kwenye miundombinu, tumekopa madeni haya yanakwenda kwenye miundombinu, sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme, bandari, baadhi ya barabara, naomba tuweke private sector wafanye. Hata viwanja vya ndege. Private Sector ndiyo inayoleta biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana watu wa Wizara ya Fedha, ni dhambi sana kujivunia kufunga biashara. Serikali serious, huwezi kusimama unasema nafurahi biashara zaidi ya 2000 zimefungwa. Hili siyo jambo la kusema. Tafadhalini sana wenzangu! Kama kweli Serikali you are serious, Waziri wa Fedha unasema mwaka 2016 tumefunga biashara 2000 ni jambo la kujisifia, hili siyo jambo la kujisifia hata kidogo, tunyamaze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli ya Serikali, shughuli ya Watu wa Wizara ya Fedha ni kusaidia biashara zianzishwe nyingi zaidi kwa sababu, biashara zikianzishwa nyingi zaidi maana yake ni ajira, maana yake kodi itaongezeka, maana yake maisha ya watu yataboreka. Kama kweli, mnataka tukae hapa tunasema wale tumewafungia maana walikuwa wanakwepa kodi, mtu wa kodi unamwita, una-negotiate naye unamwambia bwana wewe nakudai. Sasa nitakukata mwakani. Mna-negotiate! Ndio kazi ya taxation! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naombeni watu wa tax, kazi ya kukusanya kodi ni sayansi of its own. Haiwezi kuwa kazi yetu ni kufunga biashara, ni kuwashtaki, hapana! Ukifunga biashara zote, kitakachotokea ni nini? Wewe utapata kodi?Hatutapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono mapendekezo yaliyoletwa na Kamati ya Bajeti.