Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kukushukuru kwanza kwa kunipa nafasi hii, lakini pia naishukuru sana Kamati kwa maoni yake ambayo wamejaribu kutoa na ushauri mbalimbali walioutoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, siku zote nikisimama nikiwa nachangia hasa kuhusiana na mambo ya bajeti au na masuala ya fedha, najaribu kuzungumza sana kuhusiana na siasa kuondoka kwenye masuala ya kiutendaji. Masuala ya kiutendaji yakiingiliwa sana na siasa kama tunavyofanya sasa hivi katika nchi hii, lazima tukubaliane kabisa kwamba hatutaweza kufanya vizuri na tusitegemee kabisa kama Taifa hili litabadilika kama wataalam wetu ambao tumewasomesha kwa gharama kubwa na tumewapa majukumu wanashindwa kutekeleza wajibu wao, wanashindwa kuishauri Serikali kitaalam na sisi tunatoa maagizo kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza wajibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia na nimejaribu kupima bajeti yetu ya mwaka 2016/2017 na ushauri mbalimbali ambao umetolewa na Kamati. Ukijaribu kuangalia utaona kabisa kwamba sisi wakati tuko Bungeni humu tunatengeneza bajeti hii, sisi kama Upinzani tulitoa Bajeti Elekezi, ili kidogo vitu ambavyo viko mle viweze kuchukuliwa kama msaada wa kusaidia bajeti hii. Kilichotokea, tulionekana watu wa hovyo, tulibezwa humu ndani na baadaye ilionekana kwamba hata bajeti yetu isingeweza kusomwa na watu hawakuipitia kuangalia nini ambacho kinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana wenzetu ambao walikuwemo humu wanapitisha hii bajeti, leo wanalalamika na wao. Nami nashangaa, hata wewe Mheshimiwa Mapunda! Hata wewe fulani! Nashangaa sana, yaani wanalalamika wakati bajeti walipitisha wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tu kwamba uko upungufu mwingi sana ambao tuliukataa na tulishauri humu ndani. Tulianza na suala la VAT, tukajaribu kueleza hali halisi kwamba ndugu zangu mkiweka VAT kwenye masuala ya utalii mtapunguza pato la Taifa kwenye Idara ya Utalii. Tukawaambia ondoeni, angalieni wenzenu Kenya na Mataifa mengine yanafanya hivyo. Watu mkabeza mkasema haiwezekani, tunaweka sisi. Leo hii kila mmoja anashangaa humu ndani utafikiri hakuwemo Bungeni wakati wanapitisha bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu kwamba, sisi Wabunge tumepewa dhamana na wananchi kwa ajili ya kuishauri Serikali na kuisimamia Serikali. Kwa hiyo, wajibu wetu ni lazima tuutekeleze tukiwa ndani ya Bunge hili. Tukiendelea kuendekeza siasa ndani ya Bunge hili ni lazima tufike mahali ambapo tutaendelea kushindwa na kufeli na kila siku tutakuwa tunashtuka humu utafikiri hatukupitisha na kujadili sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kusema, tunachotaka kushauri hapa ni kwamba, ni lazima turudi kwenye misingi. Lazima Serikali ikubali kushauriwa na kama Serikali haitakubali kushauriwa, itaendelea kufunga masikio na kuendelea kuona Wabunge wanachozungumza ni hamna! Mheshimiwa Magufuli, kama Rais wetu, ni lazima akubaliane na sisi kwamba, sisi kama Wabunge tuliopewa majukumu haya, ni lazima akubali ushauri wa Wabunge. Sisi ndio tunaoishauri Serikali na kuisimamia Serikali, kwa hiyo, akubali ushauri wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulizungumza sana kuhusiana na hali halisi ya watumishi kukusanya mapato kwenye Halmashauri zetu. Leo Halmashauri zetu kwenye nchi hii, zote ambazo zilipelekwa kwenye majaribio, ziko chini ya 24% kwenye nchi hii katika makusanyo yake. Ni kwa sababu, watumishi waliokwenda kukusanya yale mapato wameshindwa kufikia malengo kwa sababu, watumishi ni wachache katika Halmashauri yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali tunazungumza hapa tunasema kwamba, makusanyo yanakwenda vizuri. Nataka kusema tu kwamba, fedha ambazo zimekusanywa kwenye Halmashauri zetu ziko chini kabisa. Sasa Serikali sijui kama nayo itachukua nafasi ya kuweza kufidia fedha ambazo tumeshindwa kukusanya kwenye Halmashauri zetu. Sielewi kama zitafidiwa fedha hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia kwenye Taarifa ya Kamati hapa, ukisoma kwenye ukurasa wa 26 kwenye kipengele cha 2.52 - Matumizi ya Serikali. Ukiangalia, utaona kabisa katika quarter ya kwanza katika Halmashauri, fedha kwenye Halmashauri zetu haikupelekwa hata shilingi kwenye upande wa utawala. Kwa hiyo, fedha ambazo zinatumika sasa hivi kwa ajili ya kuendeshea shughuli za utawala kwenye Halmashauri zetu, zinatumika fedha za vyanzo vya ndani, kitu ambacho kinarudisha utendaji kazi wa Halmashauri zetu. Nasi kama Halmashauri, tunashindwa kutekeleza majukumu ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba, ni lazima tukubaliane tukiwa tunatengeneza bajeti hii tujue kwamba ni bajeti ya Serikali, siyo bajeti ya vyama vya siasa. Kwa hiyo, lazima tunapoingia kwenye bajeti hizi, tukae tukubaliane, tusikilizane, tupokee ushauri wa kila mmoja wetu ili kujenga nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia shughuli mbalimbali ambazo zimefanyika na mambo ambayo yameshindwa kufanyika katika bajeti hii. Ukijaribu kuangalia katika hali halisi, Serikali yoyote duniani ina wajibu wa kuwajengea wafanyabiashara wadogo wadogo na wafanyabisahara wakubwa mazingira ya kufanya biashara ili wafanyabiashara wakubwa waweze kupata mitaji mikubwa ili waweze kulipa kodi ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yoyote makini inaendesha Serikali yake kwa kutumia kodi. Leo hii Watanzania wengi katika nchi hii wameshindwa kufanya biashara kwa sababu ya masharti magumu ambayo Serikali imeyaweka. Pia, Serikali hii haichukui hata jukumu la kuwaelimisha walipakodi wa nchi hii, ni nini ambacho kinalipwa katika Serikali hii. Wananchi hawaelewi; Watanzania hawajui! Watanzania wanajiuliza, kinacholipwa ni mtaji? Ni faida au ni kitu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania sasa hivi wanaviziwa, wanapangiwa fedha ambayo haiwezekani, wengine wanafunga maduka, wengine wanaacha biashara zao, wanahamisha biashara zao, Serikali haichukui jukumu la kuwafundisha na kuwaeleza wananchi nini ambacho kinatakiwa kilipwe kama kodi ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wajibu wa Serikali ni kuhakikisha kwamba inawaelimisha wananchi nini ambacho kinalipwa ili wananchi walipe kodi na Serikali iweze kupata fedha, lakini Serikali haina muda huo. Ni lazima tukubaliane, kama wananchi wataendelea kuwa maskini, biashara zao zitaendelea kufungwa na Serikali hii. Maduka sasa hivi tunahesabu. Ukienda Dar es Salaam wanakwambia maduka 300 yamefungwa; ukienda Mwanza wanasema maduka 200 yamefungwa; ukienda Mbeya wanasema maduka 300 yamefungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasema inatekeleza wajibu wake wakati watu wanaendelea kufunga maduka na uchumi unazidi kushuka katika nchi hii. Kwa hiyo, ninachotaka kusema, ni lazima Serikali ijikite kabisa kuwaelimisha wananchi na kuweka ustawi wa biashara zao ili wafanyabiashara wafanye biashara, mitaji ikue na waweze kuwa walipa kodi katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine la mikopo. Wanafunzi wamepewa mikopo mwaka 2016, lakini kitu cha kushangaza, sasa hivi ukienda mashuleni, ukienda UDOM hapa sasa hivi kuna wanafunzi ambao wameambiwa hawana sifa tena za kukopeshwa. Tunataka Serikali itupe ufafanuzi; kama mtoto alipata mkopo awamu ya kwanza, leo hii wanasema kwamba hana sifa ya kupata mkopo, tafsiri yake ni nini? Serikali haina fedha? Au nini kilichotokea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi sasa hivi hawaelewi kinachoendelea. Watoto wao wanapata shida, hawaelewi nini kitakachotokea hapo mbele ya safari. Kwa hiyo, tunataka tupate majibu; kama Serikali haina fedha, iseme kwa wananchi kwamba Serikali haina fedha ili wazazi wa wototo hawa waangalie ni namna gani watahangaika na watoto wao kuliko kuanza kuwahangaisha watoto ambao wameshalipiwa mkopo kwa Awamu ya Kwanza na leo hii wanaambiwa kwamba hizo fedha hazipo na watoto hawana sifa za kuweza kupewa tena mikopo. Ni jambo la kushangaza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kilimo. Wakati tunapitisha bajeti hapa, tulishangaa sana. Huko nyuma tulikuwa tunasema wakulima wanapata pembejeo kidogo, Serikali iongeze bajeti, lakini mwaka 2016 hapa wakati tunatengeneza bajeti, tulishangaa Serikali inaondoa shilingi bilioni 47 kwenye ruzuku ya Serikali kwa ajili ya wakulima, tukashangaa. Serikali hii inajinafasi kwamba inataka kuwa ni Serikali ya viwanda, huku inaondoa shilingi bilioni 47 kwenye bajeti. Leo hii mnashangaa kwa nini kuna 0.5 ambayo imeshuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnashangaa kitu gani wakati mliondoa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.