Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwa namna ya pekee naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi anazofanya hasa za kuiongoza nchi yetu Tanzania. Niwashukuru Mawaziri wote kwa namna ya pekee nimshukuru Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anazozifanya na Mheshimiwa Jenister Mhagama na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa wanazofanya usiku na mchana kuhakikisha kwamba Watanzania tunapata maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa walioifanya kwa kuimarisha viashiria vya kukua kwa uchumi, hasa kwenye upande wa ujenzi wa barabara. Lengo la Serikali ilikuwa ni kujenga na kukarabati barabara kilomita 692, lakini tumefanikiwa kukarabati na kujenga barabara kilomita 430 ambayo ni sawa na asilimia 62. Naipongeza sana Serikali yangu inayosimamiwa na John Pombe Magufuli na inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kidogo kidogo juu ya barabara yetu, hasa barabara yetu ya Lupembe. Barabara ya Kibena, Lupembe, Madeke ni miongoni mwa barabara zilizopangwa kutengenezwa kwa kiwango cha lami, mwaka jana kwenye Bunge la Bajeti tulipitisha shilingi bilioni nane kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, mpaka sasa bado tenda ya ujenzi wa barabara hii haijatangazwa, nimwombe Waziri mwenye dhamana na Waziri Mkuu mwenyewe aliona ile barabara jinsi ilivyo angalau tuweze kutangaza tender na ianze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana, ile barabara ya Lupembe kwanza inatuunganisha watu wa Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro kupitia Jimbo la Mlimba. Barabara hii imekuwa ni barabara muhimu ambayo wananchi wetu wa Lupembe wanasafirisha mazao yao. Lupembe tunalima chai, Lupembe tunazalisha mbao, tunazalisha nguzo za umeme, tunazalisha maharage, mahindi, viazi na kila aina ya matunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea barabara ile kutokana na mvua zinazoendelea sasa hivi haipitiki tena, imekuwa-blocked, kuna eneo kubwa gari zimekuwa zikikwama na hivyo wananchi kupoteza uchumi mkubwa sana kwa mazao yao kuozea barabarani kwa kutoweza kusafirisha au kupitisha kupitia ile njia, kwa mtindo huo maana yake tunakwamisha uchumi wa wananchi wa Lupembe. Naiomba Serikali yangu sikivu itenge hizi fedha ili tuweze kupata uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua Mkoa wetu wa Njombe ni moja ya mikoa ambayo tunaitegemea sana katika uzalishaji wa mazao ya chakula, pia nguzo kama nilivyosema na zao hili la chai. Sasa kama tutakuwa bado hatuna barabara nzuri, itakuwa ni vigumu wananchi
wanazalisha kwa wingi, lakini hawatoweza kuuza au mazao haya hayataweza kufikia soko kwa sababu barabara yetu siyo nzuri na haipitiki wakati wa kifuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba atakavyokuja kusimama baadaye niweze kujua ni lini sasa Serikali itatangaza tender ili barabara hii ianze kujengwa kwa kiwango cha lami kadri ilivyokuwa tumekubaliana katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi pia katika bajeti ya mwaka jana, kwa hizo fedha tulizotenga bilioni nane.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa kilimo, Mkoa wetu wa Njombe ni moja ya mikoa ambayo inategemewa sana katika uzalishaji. Mikoa mingine inapopata njaa sisi ndiyo watu tunaohusika katika kutoa chakula au wananchi wa Njombe ndiyo wanaosambaza chakula katika mikoa mingine tukishirikiana na Mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Rukwa. Mikoa hii pia iweze kupewa consideration maalum katika kuhakikisha kwamba tunaipatia kipaumbele hasa kwenye upande wa pembejeo. Mara nyingi pembejeo zimekuwa zikija kwa kuchelewa, zinafika wakati tumepanda, sasa bei yenyewe iko juu, wananchi wetu hawawezi kununua kwa bei hiyo kwa sababu kipato chao ni kidogo, tunaomba bei ya mbolea ipungue, pia iwahi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Njombe huwa tunalima mara mbili, tunalima mwezi wa Sita kwenye bustani baadaye mwezi wa Kumi tunalima sehemu za milimani ambako kunazalisha magunia ya kutosha au mazao ya kutosha. Kwa hiyo, tuombe mbolea zije mapema na
ikiwezekana zianze kuja mapema mwezi wa Sita ili wananchi wetu waweze kutumia mbolea vizuri na hatimaye waweze kupata mazao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee zao moja la chai ambalo tunalima hasa maeneo ya Lupembe na maeneo ya Luponde. Zao hili limekuwa likiuzwa kwa bei ndogo sana ukilinganisha na gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukipiga hesabu ya mbolea inayotumika shambani, kuhudumia ule mmea mpaka unapofikia kuanza kutoa chai, kilo moja ya chai inagharimu takribani shilingi 450 na zaidi, lakini bado tunauza kwa shilingi 250, sielewi ni kwa nini zao hili limekuwa likiachwa tofauti na mazao mengine kwa hiyo tuombe wananchi wetu ili wasiendelee kuzalisha kwa hasara, angalau tupunguze baadhi ya kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali mmeshapunguza tozo la moto na uokoaji, nipongeze sana Serikali kwa jitihada hizo lakini bado bei ya kuuzia wananchi haijapanda, pamoja na kwamba baadhi ya kodi imepungua, bado bei imebaki palepale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama kuna kodi nyingine ambazo zinafanya hili zao liuzwe kwa bei ndogo basi nazo tuziondoe ili waweze kunufaika na kilimo cha chai. Wote tunajua chai tunaitegemea sana hakuna mtu ambaye hatumii chai hapa ndani na ni zao ambalo kila mmoja
linamgusa hasa kwenye matumizi ya majani ya chai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwenye upande wa elimu, kwa kutoa elimu bure hasa kupeleka fedha kwenye shule zetu za sekondari na msingi kwa ajili ya kugharamia elimu bure. Ni kweli kabisa baada ya kuanza kutoa fedha hizi idadi ya wanafunzi wanaoingia
darasa la kwanza imeongezeka, hata watoto wa sekondari wanaoacha yaani drop out zimepungua baada ya kuanza kupeleka hizi fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazazi wengi walikuwa wanashindwa kulipa hizi ada na hatimaye kuwaondoa watoto shuleni na kuwarudisha
nyumbani, hasa watoto wa sekondari na shule za msingi, baada ya hii elimu bure tumeona shule nyingi zinakuwa na watoto wengi pia shule za msingi wanaoingia darasa la kwanza wameongezeka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo lipo kwenye walimu wa sayansi, pamoja na kwamba tumeajiri walimu elfu mbili na kitu, tuombe basi hao walimu wasambazwe kwenye hizi shule za sekondari ili tuwe na mkakati na ni lazima tuwe na mkakati wa kudumu wa kuhakikisha kwamba
tunawapata walimu wa sayansi wa kutosha, mkakati huu lazima tuanze mapema, tuwe na mkakati wa muda mrefu na wa muda mfupi. Tulichofanya sasa hivi ni kama muda mfupi, ni lazima tuanze kuandaa watu wetu hasa kuanzia shule za msingi kupenda masomo ya sayansi na wakienda sekondari wachukue masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutawezaje kufanya hivi, ni lazima sasa kule sekondari tusiweke option, tunapowaambia watoto wachague kuchukua combination za sayansi au kutosoma hasa chemistry na physics, tunafanya hawa watoto sasa waanze kukata tamaa mapema. Hivi sasa ukienda kwenye shule hizi za msingi, ukiuliza mtoto wa darasa la tano, utapenda kusoma masomo gani sekondari, atakwambia mimi nitasoma art. Nataka kuwa Mwanasiasa nataka kuwa Mwanasheria, ni lazima tutengeneze mazingira, tuwamotivate kwa kuhakikisha kwamba watoto wote wanapokwenda kidato cha kwanza… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.