Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Twahir Awesu Mohammed

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mkoani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. TWAHIR AWESU MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunijalia uzima na kuniwezesha kuandika maelezo yangu haya na kuyawasilisha mbele ya Bunge lako hili. Nazungumzia kipengele cha siasa ukurasa wa kumi (10) cha kitabu cha hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukamilika kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hata haiwezekani kuweka siasa pembeni kwa baadhi ya vyama vya siasa kuwa na uhuru wa kufanya shughuli za kisiasa na vyama vingine kumnyima fursa ya kufanya shughuli zake za kisiasa. Kauli ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara hadi mwaka 2020 jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, demokrasia ina uwanja mpana sana ukiwemo uhuru wa kujieleza, uhuru wa kupata habari haki ya kukosoa na kukosolewa na mengineo. Leo hii Taifa linashuhudia jinsi wananchi wanavyokosa fursa ya kuhoji ama kuwakosoa viongozi wao. Pia vyombo vya habari vinavyoshindwa kufanya kazi zake kwa uhuru na uwazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siasa za amani na utulivu ni za muhimu sana kwa wakati huu katika Taifa letu ili maendeleo yaweze kupatikana. Siasa ya amani na utulivu haziwezi kustawi hapa nchini kwa taasisi zilizojengwa kuvilea vyama vya siasa kugeuka na kuanza kuvihujumu vyama vya
siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini alipaswa abadilike na achane kabisa na dhamira aliyonayo ya kutaka kukisambaratisha Chama cha Wananchi CUF na aache kulazimisha kuwachagua viongozi wa kukiongoza kwani vyama vina Katiba na Kanuni zake Aviachie vyama vifanye maamuzi yake na asiviamulie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amani ya nchi ni muhimu sana kwa Muungano wetu una maslahi mapana kwa wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri na ni jambo la hatari; huyu Msajili wa Vyama vya Siasa asiachiwe akaliendeleza jambo hili litaleta mtafaruku mkubwa. Kwa upande wa pili wa Muungano wetu, hautariridhia hali ambayo amani ya nchi yetu itarudi kule kule tunakotoka katika siasa za chuki na uhasama baina ya wana CUF na wana CCM kule Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu:-
(i) Ili kudumisha mfumo wa Vyama vingi nchini Msajili wa vyama vya siasa afanye kazi kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na aachane kabisa kuvipangia ama kuviamulia Vyama vya Siasa.
(ii) Asaidie kutatua migogoro na sio kupandikiza migogoro.
(iii) Awe karibu na vyama vya siasa ache kujenga uadui na baadhi ya vyama vya Siasa.
(iv) Yeye ni mlezi kama baba atoe haki sawa kwa vyama asionyeshe ubaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha.