Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake kwa hotuba nzuri sana na niseme toka mwanzo kabisa kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zimetolewa hoja nyingi ambazo ningependa na mimi nichangie baadhi yake. Moja, ilitolewa hoja kwamba kuna mkanganyiko wa takwimu ambapo kwenye hotuba ya bajeti ya mwaka jana ilionesha mapato na matumizi shilingi trilioni 29.5, lakini vitabu vya mapato na matumizi vinaonesha namba nyingine. Niwashauri tu Waheshimiwa Wabunge ni vizuri wakaelewa takwimu hizi maana yake nini.
Mapato yaliyopo kwenye Volume (I) ni mapato ya kodi, yasiyo ya kodi, misaada na mikopo nafuu. Sasa ukichukua matumizi ukatoa mapato kama yalivyo katika Volume (I), ile tofauti ni nakisi ya bajeti. Kwa hiyo, nadhani ni uelewa tu wa kusoma na kuelewa tafsiri ya hizi namba ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine lililosemwa ilikuwa ni kuhusiana na uwiano kati ya ukuaji wa uchumi na madai kwamba hali halisi ya wananchi hailingani na ukuaji wa uchumi. Niseme tu kwamba, kwanza, uchumi wa Tanzania hakuna ubishi kwamba unakua, namba hazidanganyi.
Ukiangalia World Economic Data Base, takwimu za IMF, takwimu za National Bureau of Statistics zote ziko wazi. Katika Afrika, Tanzania ni moja ya nchi, the top five ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tu Benki ya Dunia wametoa taarifa yao pale Dar es Salaam na inaeleza wazi kabisa katika Afrika Mashariki, Tanzania ndiyo namba moja na hata katika Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu ambazo uchumi wake unakua kwa kasi. Kwa hiyo, hili halina ubishi, tuachane kabisa kubishana na hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu uwiano na hali halisi ni kweli bado ile quality of growth haijafikia pale ambapo wote tunatamani na sababu ziko wazi. Sababu ya msingi ni performance ya sekta ya kilimo ambayo ndiyo inaajiri watu wetu wengi imekua kwa asilimia ndogo sana na wote tunajua, sababu yake kilimo chetu bado kinategemea mvua lakini pia uwekezaji katika sekta ya kilimo ni mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunajua pia kwamba hali ya maisha ya Watanzania haiwezi kuja mara moja. Ni wazi kabisa kuwa tumeanza kuona mabadiliko katika maisha ya Watanzania. Sababu yake moja ni kwamba baadhi ya sekta ambazo nazo zinaajiri watu wengi nazo zimeanza kukua kwa kasi. Kwa mfano, uzalishaji viwandani sasa unakadiriwa kukua kwa wastani wa asilimia 6.3 kwa mwaka lakini biashara pia asilimia 6.5 kwa mwaka, usafirishaji na uhifadhi wa mizigo asilimia 17 na hizi sekta zinaajiri wananchi wetu wengi, ndiko wanakopatia kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mkazo wa Serikali uko wazi. Katika mpango wa miaka mitano, tumesema tunataka kujenga uchumi wa viwanda ambao unatumia malighafi ambazo zinazalishwa hapa hapa nchini. Tukiweka jitihada kwenye agro-processing na agri-business, tukaweka jitihada kwenye elimu na ujuzi kama ilivyo katika mipango yetu, haya ndiyo yatakayofanya ukuaji wa uchumi sasa uweze kuleta matokeo yale ambayo tunatarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni ukweli pia, vigezo vingine vya hali ya maisha ya wananchi vinaonekana wazi kabisa vimeboreka. Hali ya nyumba imekuwa bora zaidi, hali ya afya, upatikanaji wa umeme, tumepeleka umeme vijijini, yote haya siyo vitu vya kubishia na vinaongeza ubora wa maisha vijijini. Namshangaa sana Mheshimiwa Mbowe, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, hivi kweli haya hata kule Hai hayaoni? Mimi naona kama yako wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja kwamba Serikali haina mkakati wa kuinua uchumi vijijini, hii siyo kweli hata kidogo. Someni Mpango wa Miaka Mitano Waheshimiwa Wabunge uko wazi. Tumesema tutaimarisha kilimo cha umwagiliaji, tutaongeza thamani ya mazao na
mifugo, tutainua kilimo cha kisasa, tunapeleka umeme vijijni kama nilivyosema, tunaelekeza fedha kwenye utafiti na mafunzo, tunajenga barabara ili mazao ya wakulima na mifugo yaweze kufika kwenye masoko, hii yote ni mikakati ya kuinua uchumi wa vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na tahadhari kwamba IMF mwezi Januari walisema uchumi unaweza kuporomoka kutokana na kubana matumizi kupitiliza.
Kwanza niseme tu kwamba, matumizi ambayo Serikali inabana ni yale ambayo siyo ya lazima siyo kila matumizi. Serikali imekuwa inajitahidi kuhakikisha kwamba uchumi unaendelea kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza hii ripoti ya Januari ni kweli ilitoa hiyo caution lakini Mheshimiwa Mbowe pia namshangaa maana ripoti hiyo hiyo ya Januari iliweka wazi kabisa, iliipongeza Tanzania kwa kuchukua hatua kusimamia sekta ya fedha vizuri, kudhibiti mfumuko
wa bei na kusimamia matumizi. Haya yenyewe hayaoni ila caution yenyewe ndiyo anaiona peke yake, kitu cha kushangaza kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunatambua changamoto za kupungua ukwasi katika uchumi wa Taifa letu na tumeanza kuchukua hatua mbalimbali. Hatua ya kwanza tuliyochukua ni kuendelea kulipa madeni baada ya kuyahakiki. Tumelipa shilingi bilioni 631 mpaka mwezi Machi
kwa ajili ya Wakandarasi na Wahandisi Washauri, tumelipa shilingi bilioni 67.5 kwa ajili ya watumishi, shilingi bilioni 78.8 kwa ajili ya wazabuni, shilingi bilioni 17.8 kwa ajili ya watoa huduma. Hii yote ni njia mojawapo ya kuongeza tena ukwasi katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni, Benki Kuu imechukua hatua mbili muhimu. Kwanza, imepunguza discount rate kutoka asilimia 16 mpaka asilimia 12, lakini imepunguza pia statutory minimum reserve requirement kutoka asilimia 10 mpaka asilimia nane. Mheshimiwa Dkt.
Chegeni alijaribu kulieleza jana au juzi nafikiri na hatua hizi zinalenga kuongeza uwezo wa commercial banks kukopesha sekta binafsi na hivyo kuongeza ukwasi katika uchumi. Pia tunajitahidi kuongeza nguvu sasa kupata fedha za wahisani na mikopo ya kibiashara kwa ajili ya matumizi ya maendeleo na hizi zote ni kwa ajili ya kuinua ukwasi katika Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zimekuwepo hoja kuhusu milioni 50 za kila kijiji. Serikali imefanya tathmini na tumeandaa utaratibu wa kupeleka fedha hizo vijijini. Tumefanya hivi ili tuhakikishe kwamba haturudii makosa yale yale yaliyoambatana na Mfuko wa JK. Imeonekana kulikuwa na
matatizo mengi, kuna vikundi ambavyo vililengwa lakini havikusajiliwa, fedha hazifiki kwa walengwa, hakuna elimu ya ujasiriamali, hakuna hata sheria yenyewe ya microfinance na kanuni zake lakini hata mfumo wenyewe wa ufuatiliaji ni dhaifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, inabidi kwanza kurekebisha haya isije ikaonekana ni kama vilevile kwamba hizi fedha zinatolewa ni kama zawadi. Kwa hiyo, muhimu sana hili lifanyike na hatua tuliyofika sasa umeandaliwa Waraka wa Baraza la Mawaziri ili Serikali iweze kufanya
maamuzi rasmi kabla ya kuzipeleka hizo fedha vijijini. Kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha, tumetenga shilingi bilioni 60, ziko Fungu la 21, Subvote 2001 ni mradi namba 4903 unaitwa village empowerment.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.