Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema na kupata fursa ya kuchangia bajeti hii ya Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia bajeti ya Wizara naomba kwa dhati ya moyo wangu niishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kufanikisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, barabara inayotoka Dar es Salaam mpaka Tunduru - Namtumbo
mpaka Songea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilihisi sitaitendea haki nafsi yangu kama zitazungumza jambo hili. Kwa dhati ya moyo wangu napenda sana niishukuru sana Serikali hii, kwa kipindi cha nyuma tumekuwa tukipata shida sana, wananchi walikuwa wakisafiri kwa muda mrefu, lakini kwa sasa inaleta faraja. Kwa kufanya hivyo, inachangia hata vyombo vya usafiri kuwepo na ushindani, tumekuwa na magari mazuri na wananchi wananeemeka na wanaahidi kuendelea kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi katika siku zijazo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la Wabunge wa Viti wa Maalum kutokushiriki katika Kamati za Fedha. Toka nimeingia kwenye Bunge hili nimekuwa nikisikiliza Wabunge wenzangu wakieleza masikitiko yao. Kwa bahati nzuri, mimi nimekuwa Diwani katika vipindi vinne na
nimemaliza nikiwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, naielewa vizuri sana Halmashauri. Nilikuwa Diwani wa Viti Maalum lakini nilikuwa Mjumbe katika kikao cha Kamati ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, nimesema nilizungumze hili kwa sababu tumekuwa tukizungumza masuala mengi yanahusu akina mama, masuala ya mikopo, maji na mambo mengine.
Ili sisi Wabunge wa Viti Maalum tupate fursa nzuri ya kuchangia masuala haya, ni lazima tuwe Wajumbe wa Kamati ya Fedha, nasema Kamati ya Fedha kwa sababu nafahamu ndio kamati mama katika Halmashauri. Masuala yote tunayozungumza ni lazima yaanzie kule. Tunapokuja kwenye vikao vya Baraza la Madiwani ni kama Bunge, kunakuwa na dakika za kuchangia. Kwenye Kamati ya Fedha kama sijaelewa jambo lolote linalohusu mama mwenzangu ambapo mimi namuwakilisha, ninayo fursa ya kuomba kuchangia mpaka pale ninapoelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri anayehusika kwenye hii Wizara, na mimi naanza kupata shida kwenye hii Wizara sijui kwa sababu Waziri ni mwanaume na Naibu Waziri ni mwanaume. Mimi naamini wangekuwa akina mama wenzetu, tungekuwa tunawauliza wenzetu nyie mna nini na sisi? Sasa naomba niliache leo kwa Wizara inayohusika ili itusaidie na katika kutenda haki. Na
mimi naamini hata tukiwa kwenye vikao vya Bunge, sisi Wabunge wote ni kitu kimoja. Tumekuwa tukishiriki Kamati mbalimbali, tatizo ni nini kwenye Halmashauri? Naomba kupitia jambo hili, Mheshimiwa Waziri anayehusika atupe majibu kwa sababu tumekuwa tukisema sana.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwa majibu ambayo yamekuwa yakitolewa, hata kama angekesha kuyaeleza nisingeelewa, kwa sababu tunavyozungumza, Madiwani wa Viti Maalum wanaingia kwenye Kamati ya Fedha, iweje Mbunge wa Viti Maalum unamzuia asiingie
kwenye Kamati ya Fedha?
Mheshimiwa Spika, nakushukuru, lakini tunazungumzia sasa. Sasa alikuwa mwanamke, mimi sikuwa Mbunge. Nazungumzia sasa
ambapo nimemkuta Mheshimiwa Simbachawene. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie ukurasa wa 11. Kwenye ukurasa wa 11 wamezungumzia suala la usuluhishi wa migogoro. Wewe na hata Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakuwa mashahidi kwamba kumekuwa na tatizo la migogoro ya wananchi katika maeneo yetu kati ya kijiji na kijiji, kati ya Wilaya na Wilaya; kati ya Mkoa na Mkoa; na kati ya wafugaji na wakulima. Hili jambo tumelisema sana kupita vikao vya Bunge na tuliambiwa kwamba imeundwa kamati ambayo itakuwa inashughulikia. Kamati zile tunatumaini zitafika kwetu.
Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutueleza, atuambie katika kusuluhisha na katika kuunda hizi Kamati ambazo zitahusisha Wizara tano, atuambie wamefikia wapi, ili tupate majibu. Kama hawajafikia ni vizuri sasa hatua zichukuliwe kwa sababu hali
ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji sio nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie tena suala la afya. Kwenye suala la afya kwenye ahadi yetu ya Chama cha Mapinduzi tuliahidi kujenga zahanati kila kijiji, lakini tuliahidi kujenga kituo cha afya kwenye kila Kata. Nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja atuambie mpaka sasa tumefikia wapi? Pamoja na kwamba hii ahadi ni kwa kipindi cha miaka mitano, lakini lazima tuoneshe hatua, tumefikia wapi? Nilikuwa naomba anapokuja atueleze sasa tumepata vijiji vingapi ambavyo vina zahanati na tumepata kata ngapi ambazo zina vituo vya afya.
Mheshimiwa Spika, katika kutenda haki, tumeunda Mabaraza ya Kata na kwenye Vijiji vyetu, lakini mabaraza yale ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yakishughulikia migogoro ya wananchi, wale Makarani hawajaajiriwa na wameeleza.
Kwa hiyo, naomba tupate ufafanuzi, katika kutenda haki. Ili haya masuala ya rushwa tunayoyazungumza yasiwepo, ni lazima yule mtu awe ameajiriwa; kama hatujaajiri, tunawezaje kufanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naweza kulizungumza ni suala la kukaimu watendaji kwenye vijiji vyetu na Kata. Tumesema sana kupitia kwenye vikao vyetu kwamba tunalo tatizo la kukaimu nafasi hizi, tunaomba sasa na wakati umefika wale kwenye vijiji vyetu tuwaajiri
watendaji; unapomwajiri mtu anakuwa na mamlaka kamili.
Kama hiyo haitoshi, hata Wakuu wa Idara, maeneo mengine Wakuu wa Idara hawajathibitishwa. Nilikuwa naomba kwamba kwa maana ya hao Wakuu wa Idara ambao wamekidhi vigezo, basi tuwathibitishe ili wafanye kazi wakiwa wanajijua kwamba wao ni Wakuu wa Idara kamili.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, nije katika suala la TASAF, Mheshimiwa Waziri, amekuwa akilizungumza vizuri sana na amegusa kwamba katika kipindi kilichopita amezungumzia kwamba umefanyika uhakiki wa kuangalia watu ambao walikuwa wanapata zile fedha ambao hawastahili.
Wameguswa watu wengine ambao wanastahili kupata pesa, ni vizuri Mheshimiwa Waziri anayehusika arudi aangalie upya, kwa sababu pesa zile zimelenga kusaida kaya masikini, ni vizuri arudi aangalie upya kuona kweli hizi takwimu tunazozipata ni takwimu sahihi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho ambalo naomba nilizungumze ni suala la kuongeza mamlaka za utawala.
Miongoni mwa Wilaya kongwe katika nchi hii ni pamoja na Wilaya ya Tunduru. Wilaya ile ilianzishwa mwaka 1905 na ina kilometa za mraba zisizopungua 18,000 yaani ukiichukua Wilaya tu ya Tunduru, ni sawa na Mkoa wa Mtwara. Imefika mahali wananchi wale wa Tunduru wanahisi kwamba siyo sehemu ya Tanzania kwa sababu eneo la utawala lile ni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kwenye Wizara hiyo wakati unapofika, ni vizuri sasa wakaangalia kuona katika kugawa maeneo ya utawala na sisi kwenye Wilaya ile watufikirie katika ule Mkoa wetu wa Ruvuma. Wilaya ile ni kubwa. Katika kuhakikisha huduma za wananchi zinakuwa
karibu, ni vizuri sasa tuone uwezekano wa kugawa hizo Wilaya, lakini ikiwemo na Wilaya ya Tunduru. Kama Mheshimiwa Rais itampendeza na ninafurahi kwamba Wizara hii sasa iko chini ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa mchango wangu. Naunga mkono hoja, ahsante sana.