Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na mwingi wa utukufu, kwa kunijalia uzima siku hii ya leo na hatimaye kuweza kusimama hapa ili nami niweze kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma vizuri Bajeti ya TAMISEMI, ni nzuri sana. Ukiisoma inaleta raha, ambayo kimsingi Wizara hii inahitaji pesa takribani shilingi trilioni 6.8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mwaka huu wa fedha tunaokwenda 2017/2018 baada ya kuwa Bajeti ya msimu uliopita imetekelezwa kwa asilimia 75.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kabisa changamoto kwa msimu uliopita zilikuwa nyingi, basi Wizara hii ijipange vizuri kuhakikisha kwamba bajeti hii inayokuja sasa iweze kutekelezeka kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye asilimia 10 za vijana na wanawake ambazo zinatolewa kutokana na mapato ya ndani ya Halimashauri zetu kwenye maeneo mbalimbali hasa kwa Mkoa wetu wa Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC, ambaye nimekuwa nikiona kwa macho yangu mwenyewe namna gani jambo hili linatekelezwa kwenye Halmashauri mbalimbali. Jambo hili limechukuliwa tu kama ni jambo ambalo siyo muhimu sana kwa sababu bado
halijatungiwa sheria; likitungiwa sheria mahususi itasaidia hawa Wakurugenzi kuona kwamba ni muhimu na watalitekeleza kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo naipongeza sana Kamati ya LAAC lakini pia na CAG ambaye anatusaidia kukagua hayo mahesabu na kuona hali halisi.
Kamati hii imesimamia vizuri na sasa hivi Halmashauri zote zimeanza kupeleka pesa asilimia tano kwa vijana na asilimia tano kwa wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Wakurugenzi wote ambao wameanza kutekeleza jambo hili na ninaomba waendelee kufanya hivyo na wale wote wanaopewa fedha hizo wasidhani kama ni zawadi, basi hii ni kama Revolving Fund, inatakiwa ipelekwe kwa wengine na wengine waweze kufaidi baada ya wengine kurejesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye posho za Madiwani. Waheshimiwa Wabunge wenzangu pia wamesema kwamba Madiwani ndio wale ambao wanafanya kazi hasa moja kwa moja kwa wananchi na sisi tukiwa wakati mwingine tunatekeleza majukumu yetu katika
vikao mbalimbali vya Bunge, nao siku zote wamekuwa na wananchi; wakiamka asubuhi wapo na wananchi majumbani kwao. Sisi wakati mwingine tunaweza tukasema, nimesafiri nimeenda huku, lakini wao wanafanya kazi moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilidhani Serikali yetu ione uhumimu wa kuwaongezea posho Waheshimiwa Madiwani. Wizara hii ya TAMISEMI, tafadhali sana, naomba hata kama kuna sheria au kanuni basi ziletwe hapa Bungeni tuzirekebishe ili nao waweze kufanya kazi wakiwa wakiwa na mori mzuri ambapo kimsingi watakuwa wamewezeshwa vizuri lakini pia waweze kupatiwa vitendea kazi kwa maana ya usafiri.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yao ya utawala wakati mwingine unakuta Madiwani wengine wapo vijijini, anatembelea vijiji karibu vinne au vitano; ataenda kwa baiskeli au kwa mguu. Basi Serikali ione umuhimu wa kuwatafutia hata magari ili waweze kufanya kazi zao vizuri.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika TAMISEMI pia kwa masikitiko makubwa sana, bado Wizara hii ya TAMISEMI na Utawala Bora pia niseme hamjaona umuhimu wa Mbunge Viti Maalum. Mbunge wa Viti Maalum anafanya kazi kubwa sana. Eneo lake la utawala ni la Mkoa mzima, lakini bado kwa mujibu wa kanuni, Mbunge wa Viti Maalum yeye ni Diwani wa Halmashauri anayotoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza, Mbunge huyu hawezi kuingia kwenye Kamati ya Fedha na kuweza kuona changamoto zinazowakabili wanawake, wanatengewa fedha kiasi gani ili ziweze kuwafikia. Nani anawasemea huko ilihali sisi Wabunge wa Viti Maalum ndio
tupo kwa mujibu ili kuwasemea wanawake wenzetu, lakini kwenye Kamati za Fedha hatuingii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Utawala Bora, muone umuhimu wa kufanya hili na TAMISEMI pia tunataka Wabunge wanawake waingie humo na wanawake Madiwani wa Viti Maalum waingie humo ili waweze kuwasemea wanawake wenzao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa walimu. Katika Mkoa wangu wa Ruvuma, walimu wanapata shida sana, wanafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha mtoto ambaye hajui ‘a’ wala ‘be’ anafikia mahali ambapo anaweza kusoma na kuandika. Hii kazi ni kubwa sana.
Hata wewe Mheshimiwa Waziri ulioko hapa, nawe ulianzia a, be, che. Kwa hiyo, kumbuka, kama mwalimu yule asingeweza kukufundisha akawa na mazingira mazuri, ni wazi kwamba wewe usingefikia hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara ione umuhimu wa walimu kuwezeshwa wakawa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Pia walimu wangu wa Mkoa wa Ruvuma wote katika Wilaya zote, nikianza na Nyasa, Mbinga, Tunduru, Namtumbo, Songea Vijijini na
Songea Mjini hawa wote wana madeni. Madeni yao yanafikia takribani shilingi bilioni tatu. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up aniambie hawa walimu wanalipwaje hizo pesa zao? Mimi na wewe tutakuwa sambamba, vinginevyo Mheshimiwa Waziri nitakama shilingi
ya mshahara wako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye shule za sekondari. Kuna shule za sekondari zinazoanza katika Wilaya ya Namtumbo, ndiyo zinaanza kidato cha tano. Shule hizi zimetelekezwa, hazipelekewi fedha kwa ajili ya mahitaji mbalimbali katika shule hizo ni Nanungu sekondari iliyoko katika Wilaya ya Namtumbo pamoja na shule ambayo inayoitwa Pamoja sekondari, shule ya Namabengo na shule ya Nasuri. Shule hizi zimetelekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri wa TAMISEMI, tena bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI tulienda wote katika shule ya Nasuri katika Kata ya Namtumbo, ulishuhudia pale, lakini wale watoto uliwaona wameng’aa kwa uso, lakini ndani yake hawana huduma za
mzingi. Naomba tafadhali utakapokuja, uniambie hawa watoto wanapataje huduma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la utawala bora. Nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wangu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania; na hili nitalisema wazi wazi na nitatembea kifua mbele nikilisema. Mimi kama Mbunge wa Chama cha
Mapinduzi, nataka niwaambie kwamba Mheshimiwa Rais wangu anafanya anafanya kazi nzuri. Ninacho cha kusemea ninaposimama hapa, kwamba ameweza kudhibiti mianya ya rushwa; lakini pia ameweza kupambana na madawa ya kulevya; amerudisha nidhamu kwa watumishi wa umma; bado ameweza kusimamia na kudhibiri matumizi ya fedha katika nchi yetu. (Makofi)
Ndugu zangu, kwa wale wote wanaoitakia mema nchi hii ni lazima watasema kwenye jambo hili. Tunaweza tukasema wakati wowote ule kwa sababu tunajua kwamba Rais wetu anatekeleza na anasimamia vizuri ilani, licha ya shughuli nyingi anazokuwa anazifanya ikiwepo pamoja na
ndege ambazo zimekuja. Nchi hii ilikuwa haina ndege, ni nchi iliyokuwa inatia aibu, lakini kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja na nusu, tayari tumeona ndege, usafiri wa anga unakwenda barabara. Maeneo mbalimbali viwanja vinaendelea kurekebishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili mimi nitalisema tena kwa kifua mbele. Wale wanaochukia na wajinyonge tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, Mheshimiwa Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano, kwa haya aliyoyafanya ya kuweza kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya na mengine, ni lazima…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.