Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE.ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, hizi Wizara mbili ni muhimu sana hebu kila mtu atumie dakika kumi vizuri zaidi kuliko kuzipoteza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niseme mimi nimekuwepo Bungeni hapa tangu mwaka 2000. Suala nitakaloliongea leo nimeliongea tangu mwaka 2001, naongelea upande wa TAMISEMI. Wilaya ya Same ni kubwa sana katika Mkoa wa Kilimanjaro. Mkoa wa Kilimanjaro una
Wilaya saba lakini Wilaya ya Same ina ukubwa wa kilomita za mraba 5,152 ambazo ni sawa na asilimia 40 ya Mkoa mzima wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Same hiyo ina majimbo mawili, Same Magharibi na Same Mashariki. Makao Makuu ya Wilaya yako Same Magharibi yako katika Kata ya Same ambayo ndiyo ya mwisho unakwenda Wilaya ya Mwanga. Jimbo la Same Mashariki liko mwishoni na Mkoa wa Tanga. Kata ya kwanza inaanza Bendera, Kiurio, Ndungu, Kalemawe, Maore hapa ni tambarare.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo linapojitokeza ni hapa. Tunapata tatizo kwamba Hospitali ya Wilaya ya Same iko, Kata ya Same ambako ni mbali sana na Jimbo la Same Mashariki. Kwa hiyo, athari kubwa inawakuta kina mama wajawazito, hili suala nimeliongelea kwa miaka 15. Kina mama wengi sana kutoka Jimbo la Same Mashariki wanapohitaji huduma ya upasuaji dakika za mwisho anataka kujifungua anagunduliwa kwamba upasuaji unahitajika ni lazima apelekwe Same, wengi sana wanapoteza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia 2010-2015 tumepoteza akina mama 18 na watoto wao. Hao ni wale waliofika Same. Waliopotezea maisha majumbani au kwenye zahanati sina takwimu za kusema.Watoto wachanga 28 wamepoteza maisha. Namshukuru sana Mheshimiwa Jafo alikuja Wilaya ya Same. Wabunge hatukuwa na habari tungekuja tukulalamikie kule kule, lakini mimi kwa sababu nimesema kwa miaka 15 naiomba sasa TAMISEMI ione umuhimu wa hapa Ndungu ndani ya Jimbo la Same Mashariki kwenye Makao Makuu ya Jimbo la Same Mashariki, kile kituo cha afya kipate huduma ya upasuaji. Inapokuja kuzungumzia akina mama nitapaza sauti mpaka dakika ya mwisho. Jimbo la Same Mashariki akina mama wanapoteza maisha sana kwa sababu ya kukosa huduma ya upasuaji. Kipare tunasema; “wekienda kutana na nashindaki taganyamaa.” Naomba nitafsiri, wewe kama umebeba nyama kichwani nzi watakufuata. Sasa kama unataka wale nzi wasikufuate hiyo nyama itupe. Hili suala ili nisilipigie makelele Serikali malizeni hili jambo, hamtanisikia tena nikisema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapo nimetoka TAMISEMI nije Wizara ya Utumishi na Utawala Bora. Mimi nazungumzia Mfuko wa Rais wa Kujitegemea. Huu Mfuko wa Rais wa Kujitegemea umeanza takribani miaka 33 iliyopita.
Mimi nimeungalia vizuri Waheshimiwa Wabunge, huu mfuko unawasaidia akina mama na vijana wanapata mahali pa kukopea kwa ajali ya miradi midogo dogo ya kujiendeleza ili waweze kujitengemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku duniani, nizungumzie Tanzania na Afrika akina mama pamoja na vijana ni wazalishaji wakubwa sana na mjue akina mama ndiyo wanaoangalia vijana, sijui mmenielewa? Kwa hiyo, mama anacheza kotekote anazalisha na anaangalia vijana. Huu
Mfuko wa Rais wa Kujitegemea takribani miaka 33 sasa hivi lakini umeonyesha kufanya vizuri sana. Kwa sababu gani nasema hivyo Mwenyekiti? Inapokuja kwenye marejesho hawa wanarejesha asilimia mia moja hakuna matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba nizungumze kwa unyenyekevu. Kwanza tuwapongeze wanaoratibu mfuko huu kwa sababu mahali popote ambapo kuna kukopa kurejesha kuna matatizo, lakini hawa wanarejesha asilimia 100 ina maana wanaoratibu mfuko huu
wanafanya kazi vizuri sana. Hata hivyo, kuna changamoto kwamba Serikali haiwapi pesa za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iwapo huu Mfuko wa Rais wa Kujitegemea inapokuja kwenye repayment ni 100% jamani kwa nini wasipewe fedha za kutosha? Kazi wanayoifanya inawasaidia akina mama na vijana kwa hiyo moja kwa moja inachangia kwenye uchumi. Naiomba Serikali
mfuko huu uangaliwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hapo tu, tangu 33 iliyopita mfuko huu uko kwenye Mikoa mitano tu ya Dar es Salaam, Lindi, Njombe na mwingine wa tano mniwie radhi nimeusahau.
Ombi langu kwa unyenyekevu mkubwa, Mheshimiwa Waziri wa Utumishi naomba unisikilize, kwa sababu marejesho ni 100% hebu sasa ongezeni mikoa mingine mitano. Katika hiyo mikoa mitano itakayoongezwa naomba Mkoa wa Kilimanjaro uwepo. Ukienda Same Magharibi akina mama wa Ruvu wanalima vitunguu wakipata mikopo watafanya kazi vizuri. Ukija Same Mashariki kuna akina mama wanaolima tangawizi na mpunga wakipata mikopo hiyo watafanya kazi vizuri zaidi. Naomba iongezwe mikoa mingine mitano na huu mfuko upewe pesa za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana.