Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Nchi ambayo ametuwezesha katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuweza kupata fursa kuwasilisha hoja yetu hapa na Wabunge wamechangia, lakini pia napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa imani yake kwangu amenipa fursa ya kuhudumu katika Ofisi hii ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kipindi chote hiki. Kwa kweli Mheshimiwa Rais, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwa uongozi wake. Sambamba na hilo pia napenda kumshukuru Waziri wetu Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa kwa fursa kubwa anayotupa sisi wasaidizi wake tukiwa humu Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru kipekee, Waziri wangu mwenye dhamana, Mheshimiwa George Boniface Simbachawene kwa maelekezo mazuri, lakini umekuwa sio Waziri peke yake isipokuwa umekuwa kama kaka kwangu, pia ni kocha unayenipa fursa ya kuweza kutimiza majukumu yetu katika ofisi hii kubwa ambayo inawakilisha wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Namshukuru sana Waziri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge na viongozi wote wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia napenda sana kumshukuru Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Serikali za Mitaa na Utawala, ndugu yetu Mheshimiwa Rweikiza pamoja na Kamati yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hii ndiyo Kamati pekee ambayo ukija kuiangalia inajadili mafungu yapatayo
28. Kwa kweli tunawashukuru sana na timu yako kwa msaada mkubwa katika ofisi yetu. Hatuna cha kuwalipa, mmekuwa Walimu, mmekuwa waelekezaji wazuri mpaka leo hii tunapohitimisha hoja yetu hii ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nitoe shukrani zangu za dhati kwa watumishi wote wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ushirikiano wao mzuri, kwa upendo wao, wametusaidia sana na kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene kuhakikisha kwamba tunatekeleza majukumu yetu katika kipindi hiki cha mwaka huu na mpaka leo hii tunakuja kuomba sasa Bajeti nyingine ya mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru familia yangu; namshukuru mama yangu mzazi kwa malezi mazuri.

Kwa kweli nawakumbuka sana na ninajua mmeni-miss sana, lakini yote hii ni kwa ajili ya kulitumikia Taifa letu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe kwa msaada na dua zao njema siku zote wanaoniombea ninapotimiza majukumu yangu nikiwa hapa Bungeni, nikiwa Jimboni halikadhalika, nikiwa maeneo mbalimbali kuhakikisha kwamba dhamana aliyotupa Mheshimiwa Rais tunaitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Wajumbe tukiwasilisha hoja yetu, Waziri wangu mwenye dhamana akiwasilisha hoja hii, tulipata fursa ya kubaini michango mbalimbali ikitoka kwa Waheshimiwa Wabunge, nami niliyojifunza katika haya ni jambo moja kubwa. Lengo kubwa la Wabunge ni kuona Ofisi hii inaweza kufanya kazi yake vizuri na Wabunge wengi sana walijielekeza katika suala zima la sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ukija kuangalia, nami nimepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali. Nilipotembelea kweli katika nchi yetu hii, ukienda maeneo mbalimbali utakuja kubaini kwamba sekta ya afya ina changamoto kubwa. Ndiyo maana kiongozi wangu akinituma nipite sehemu mbalimbali, tumeweza kuzibaini na ndiyo maana humu tunapangia mipango ya pamoja, nini tufanye ili mradi twende mbele zaidi na tunajua wazi kwamba, nchi yetu ambayo tulikuwa tunataka katika Sera yetu ya Afya kuwe na ujenzi wa zahanati takriban kila kijiji, tulipaswa kujenga zahanati 12,545, lakini mpaka sasa hivi tumefikia zahanati 4,470. Halikadhalika katika vituo vya afya, tulikuwa na sababu ya kuweza kujenga vituo vya afya 4,420, lakini mpaka leo hii tumejenga vituo vya afya 507. Kwa hiyo, tuna kazi kubwa sana ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali zetu za Wilaya, kati ya Wilaya zetu ambapo Wilaya zetu 139, hivi sasa sehemu zenye huduma tunapata Hospitali 119 peke yake.

Maana yake tuna kazi kubwa ya kufanya. Katika hili nawashukuru Wabunge wote. Waziri wangu akija hapa kwa sababu atakuwa na muda mrefu wa kufafanua, atazungumza mambo haya kwa undani zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao katika njia moja au nyingine, nilivyokuja site kule tulishirikiana vizuri. Hili naomba nikiri wazi, mama yangu Mheshimiwa Anne Kilango Malecela hapo ulizugumza kwa uchungu sana, hasa katika kituo chako cha Ndungu kule, na mimi bahati nzuri nilifika kule Same mama yangu. Kilio chako unasema kwamba Same ni kubwa na hapa ulitoa reference kwamba ni kilometa za mraba karibu 10,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wananchi wa pale na nilipofika pale, ndiyo kilio ambacho wewe ulikileta siku zote, nilipofika pale kweli nilikikuta. Nikuhakikishie kwamba mimi na kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene, tulishirikiana na Wizara ya Afya ambapo wenzetu wapo katika upande wa sera, katika ile haja yako hasa ambayo umeipigia kelele kipindi chote na ukaacha maagizo kwa viongozi wako nilivyofika pale site, tutahakikisha mwaka huu huenda mwaka Mungu akijaalia, kabla ya mwezi wa saba kazi ya ujenzi wa theatre utaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafanya hivyo katika maeneo mbalimbali. Katika agenda yetu tulisema tutafanya ujenzi wa vituo vya afya vipatavyo 100. Lengo letu ni nini? Ni kuhakikisha sasa tunapeleka huduma kwa wananchi. Ndiyo maana wakati mwingine Hospitali zetu za Wilaya na zile za Rufaa zinahemewa kwa sababu huku chini vituo vya afya uwekezaji ulikuwa mdogo, ndiyo maana Serikali hii sasa imeamua kufanya maamuzi katika mpango wake hasa katika suala zima la ujenzi wa zahanati tumetenga takriban shilingi bilioni 22.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kuhakikisha kwamba tunaenda kuendeleza ule ujenzi wa zahanati takriban 370 huku tukishirikiana na nguvu za wananchi; tutaenda kufanya suala zima la ukarabati wa vituo vya afya 144, sambamba na kuhakikisha tunajenga maboma mengine 100, kuyamalizia 539. Hili tutaenda kulifanya katika katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika katika mpango mwingine mkakati tumetenga takriban shilingi bilioni 11.4. Katika eneo hilo, tutafanya? Lengo letu ni kwamba kuna vituo vya afya vinavyojengwa vipatavyo 94; tutaenda kuongeza nguvu hapo. Lengo ni kwamba tuweze kuvimalizia wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna vituo vyetu vingine 12 kama ni maboma yanataka umaliziaji, tutahakikisha tunashirikiana na wananchi ili hizi shilingi bilioni 11.4 na maeneo mengine twende tukawekeze katika suala zima la vituo vya afya tuweze kupata sasa mpango mkakati mzuri tuwasaidie wananchi Watanzania waweze kupata huduma nzuri. Mwisho wa siku ni kwamba wananchi waliipa ridhaa Serikali hii ya Awamu ya Tano, imani yao kubwa ni kwamba Serikali itaenda kuwatumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami na kaka yangu hapa naomba niwaambie kwamba tumejipanga kuhakikisha tunafanya mabadiliko makubwa katika sekta ya afya tukiwa sisi ni watekelezaji wa sera katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika kipindi cha sasa mnafahamu zamani tulikuwa na changamoto sana ya dawa na ninyi Wabunge mara nyingi mmekuwa mkiuliza maswali hapa kuhusu suala zima la ukosefu wa dawa; na ndiyo maana katika mwaka huu ambao tunaenda nao, tulitenga takribani shilingi bilioni 106.3 na mpaka tunafika katika miezi ya katikati, mwezi wa tatu tulipeleka takribani shilingi bilioni 79.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyokuwepo hivi sasa ni kwamba wakati mwingine Serikali inapeleka fedha, lakini usimamizi wa fedha siyo mzuri. Katika hili naomba nimshukuru Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI anayeshughulikia suala la afya, katika kuzunguka kwake huko ametuibulia mambo mengi sana na ya msingi.

Ndiyo maana naomba mtuwie radhi ndugu zangu Wabunge, kwamba wakati mwingine tukifika kama mtaalam hasa aliyepewa dhamana ya uongozi kama DMO, huenda fedha zipo, zinashindwa kutumika kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, jambo hilo hatutalivumilia kwa maslahi mapana ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani hata kidogo! Tulipofika mwezi wa saba mwaka 2017 mwaka unaanza, takriban shilingi bilioni 20.5 zilikuwa hazijatumika ambapo wataalam wetu walitakiwa wazitumiwe kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba. Hili jambo haliwezekani hata kidogo. Katika utaratibu wa sasa tutaenda kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunasimamia vyema sekta yetu ya afya, wananchi waweze kupata fursa nzuri ya kuamini kwamba Serikali yao sasa iko vitani kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma nzuri ya afya. Nawapongeze sana wadau mbalimbali, Waheshimiwa Wabunge, katika maeneo mbalimbali mmetumia mifuko yenu ya Mfuko wa Jimbo kuhakikisha kwamba mnajenga kusaidia nguvu za wananchi katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, hongereni sana katika hilo. (Makofi)

Pia niwapongeze badhi ya Wakuu wa Wilaya, wamethubutu kwa kiwango kikubwa; kwa mfano, nilifika kule Tunduru, kuna Mkuu wa Wilaya ya Tunduru pale Bwana Homera, nimekuta amefanya harakati kubwa za ufyatuaji wa matofali. Nilipokuwa site juzi juzi nilimwuliza, akaniambia kuna takriban matofali milioni 14 yameshafyatuliwa. Lengo ni kuhakikisha anasaidia ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, halikadhalika na katika sekta ya elimu. Tunataka mfano kama huu. Tunataka mfano kama DC yule wa Korogwe aliyefanya kazi kubwa katika maeneo hayo. Tushikamane kwa pamoja, lengo letu twende mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie suala zima la matumizi mifumo ya elektroniki; mkumbuke kwamba kama Ofisi ya TAMISEMI, tumefanya uwekezaji mkubwa sana katika suala zima la kimifumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani tulikuwa tunatumia zile risiti za kawaida za karatasi, lakini sasa hivi Idara yetu ndiyo Idara ambayo ina miundombinu iliyojitosheleza, lengo kubwa ni tujielekeza katika mifumo ya elektroniki. Ndiyo maana mpaka mwezi Machi, tumeweza kukamilisha kuweka mifumo katika Halmashauri zetu zipatazo 177. Hii ni kazi kubwa! Tumebakiza Halmashauri nane tufikie Halmashauri
185. Lengo letu ni kwamba ikifika mwezi Juni, tuwe tumekamilisha zoezi katika zile Halmashauri chache ambazo zimebaki, ambazo zote ni Halmashauri mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba nikiri wazi, katika eneo hili tumepata mafanikio makubwa sana. Kwa mfano, ukiangalia na hata ukienda Mikindani kwa ndugu yangu pale Mheshimiwa Maftaha, tulikuwa tunakusanya takriban shilingi milioni 600 tu kwa mwaka, lakini baada ya mfumo wa sasa hivi, taarifa inaniambia kwamba karibuni shilingi bilioni 2.6 zimeshaanza kukusanywa. Hii ni kazi nzuri inayoendelea kufanyika. Hata kule Arusha tulikuwa tunakusanya takribani shilingi bilioni tano, leo hii tumefikia shilingi bilioni 10 point something.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata suala zima la vituo vya afya, kwa mfano nilitembelea kituo cha afya cha pale Kaloleni, Arusha, walikuwa wanakusanya shilingi milioni nne tu kwa mwezi; lakini baada ya kuwaambia wasimike mifumo, baada ya hapo wanakusanya kuanzia shilingi milioni 24. Haya ni mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jukumu letu sisi Wabunge ni kuhakikisha tunaenda katika Halmashauri zetu; Serikali inapoenda kujipanga tuhakikishe na sisi tunachukua nafasi yetu kusimamia mifumo iende ikasimikwe vizuri, siyo kusimika peke yake, lazima matumizi ya mifumo yaweze kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie, Ofisi ya Rais, TAMISEMI itatoa ushirikiano wa kutosha. Lengo letu ni kwamba own source zikusanywe vizuri ili mradi wananchi waweze kupata fursa ya maendeleo katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja katika suala zima la Mfuko wa Vijana na Akina Mama; na mkumbuke katika mwaka huu wa fedha 2016/2017 ilikuwa imetengwa bajeti ya shilingi bilioni 56.8, lakini mpaka tunapozungumza hapa juzi juzi, ni shilingi bilioni 15.6 zimepelekwa.

Kwa hiyo, nawaombe ndugu zangu Wabunge, kwamba zile own source za asilimia tano za vijana na akina mama hazifiki kwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mpango; fedha zile zinaishia katika Halmashauri zetu. Niwasihi sana, tunaposimama katika vikao vyetu vya Kamati ya Fedha tuombe kuelekeza kwamba fedha itakayokusanywa lazima ipelekwe kwa vijana na kina mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie, sisi Ofisi ya TAMISEMI tutachukua jukumu hili kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba tunasimamia; lengo kubwa ni vijana na akina mama waweze kupata mikopo washiriki katika shughuli za uchumi wa nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata hoja ya msingi kutoka kwa Mheshimiwa Ikupa pale akisema walemavu wamesahaulika katika jambo hili. Naomba tuwaambie Mheshimiwa Ikupa na wenzako ni kwamba jambo hili tumelichukua na Mheshimiwa Waziri wangu ataliwekea utaratibu vizuri, tuone jinsi gani ya kufanya katika asilimia kumi angalau na walemavu waweze kukumbukwa, wananchi hawa waweze kushiriki vyema katika suala zima la uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ajenda kubwa ilizungumzwa hapa ya barabara. Katika ajenda hii ya barabara ukizungumzwa kila mtu anaguswa na ajenda ya barabara. Ndiyo maana ukikumbuka mwaka 2016 tulitengewa karibu shilingi bilioni 249.7 hapa na mpaka mwezi Machi, tulipelekewa karibun shilingi bilioni 142, lakini kuna kazi kubwa sana ilifanyika; tumejenga maboksi kalavati kama 23, tumejenga madaraja, tumejenga barabara ya kilometa 11,111.57. Hii ni kazi kubwa inafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, leo hii ukitembea katika Miji mbalimbali kazi kubwa iliyofanya TAMISEMI inapimika kwa vigezo vyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika hii Miji yetu Mikuu kupitia mradi ya TCSP Project, tumefanya kazi kubwa sana katika maeneo haya nane; lakini ukienda zile Halmashauri za Miji 18, zamani ukipita maeneo hayo utakuta barabara za vumbi, lakini leo hii, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeamua kuweka ujenzi wa barabara za lami katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie, katika bajeti ya mwaka huu ambayo imetengwa takribani shilingi milioni 247.7 tutaenda kufanya kazi kubwa ya kuondoa vikwazo hasa ujenzi wa madaraja na kuondoa vikwazo na ndugu yangu mmoja nimemsikia hapa jana alikuwa anazungumza kwamba sisi hatufikiki, hili ni jukumu la ofisi yetu. Nami bahati nzuri naomba niwaambie kwamba tumejipanga vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu ni kuacha legacy kwamba tukiondoka na kaka yangu hapa, hata tukihama watu waseme hapa alikuwa Mheshimiwa Simbachawene na Jafo, walifanya hii kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini binadamu aliyekuwa sahihi lazima afanye kazi aache legacy katika maeneo yake. Na sisi naomba niwaambie, tutaenda kuacha legacy katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua wazi kwamba Ofisi hii ni Ofisi ya wananchi, ndiyo bajeti ambayo inabajetiwa mwananchi kijijini, Mwenyekiti wa Kijiji, Diwani na Waheshimiwa Wabunge na kila…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya kama ni bashrafu tu, naomba niseme sasa naunga mkono hoja hii. Ahsante sana. (Makofi)