Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Ester Michael Mmasi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikushukuru kwa kunipa fursa hii adimu nami niweze kuchangia kwenye Bunge lako hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla sijaenda mbali, napenda sana kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupa si tu Waziri lakini pia ametupa encyclopedia ya sheria katika Bunge hili. Si encyclopedia ametupa guru wa masuala ya sheria katika muktadha huu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli ametutendea haki sisi Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichangie masuala ya ajira kwa vijana kwa mlengo wa sheria. Kwa kuanza naomba nichangie Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ni kwa namna gani inasigina fursa ya ajira kwa vijana wetu lakini si hivyo tu ni kwa namna gani sheria hii imetumika katika kupora rasilimali ya Tanzania na kusafirisha na hata wazawa tumebaki kuwa watazamaji katika muktadha huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukianza na Sheria hii ya Madini ya mwaka 2010, ukiangalia Kanuni ya 16(1) inaruhusu mgeni kusafirisha madini nje ya nchi. Tukienda kifungu cha 16 tunaona kabisa hata kwenye maonyesho ya kibiashara, mgeni anaruhusiwa kununua madini na kusafirisha nje ya nchi. Si hivyo tu, tunaambiwa kwamba mgeni ambaye amekuja kwa visa siku tatu nchini Tanzania anaruhusiwa kusafirisha madini kwa kadri awezavyo lakini tu kama ata- comply kwenye requirement na miongozo ya kisheria. Namba moja atalipa mrahaba unaotakiwa kwa kusafirisha madini hayo lakini pia Kamishna wa Madini atakapokuwa ametoa kibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu, inasikitisha sana kuona kwamba mchimbaji mdogo ambaye ni brokers licensed holders ananyimwa kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi. Hii hatutokubali hata siku moja, sisi ambao tunaamini vijana wetu vitovu vyao vilivyozikwa katika ardhi ya Tanzania, kijana ambaye anajua kuongea lugha ya Kiingereza ananyimwa fursa ya kufanya biashara nje ya nchi kwa kigezo ambacho hatukielewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Sheria ya Madini kifungu cha 18 unaona adhabu iliyotolewa, unaambiwa kwamba mtu atakapokuwa amefanya biashara akakiuka haya yote katika muktadha wa sheria, adhabu ni miaka mitatu jela au shilingi milioni 10 tu, hii tunakataa. Tunakataa kwa sababu hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tumeagizwa tutetee haya. Nitasoma ni kwa namna gani Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesimama kuona kwamba imefika mwisho tuzuie biashara ya utoroshaji wa madini. Hili tulili-swear kwa wananchi wetu, naomba nirejee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ukurasa wa 34, kipengele ‘K’ kinasema:-
“Katika kipindi cha 2015 hadi 2020, Chama cha Mapinduzi kitaielekeza Serikali yake kutekeleza mambo yafuatayo: Kubuni na kutekeleza mikakati mahsusi itakayowezesha kupunguza au kukomesha kabisa vitendo vya utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi na biashara haramu ya madini nchini”. Hii ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema kwamba imefika mwisho, tunachotaka kuona ni kwamba viwanda vya uchenjuaji wa madini vinajengwa nchini Tanzania. Kwenye sheria hii kwenye kifungu cha 52 wameweka obligations za mwekezaji lakini hatujaona kipengele kinachomlazimisha mwekezaji kuweka plants katika nchi ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalitetea kwa nguvu zote kwa sababu naamini kiwanda cha uchenjuaji wa madini kitakapojengwa Tanzania, kwanza tutatengeneza ajira kwa vijana wetu lakini pili tutaongeza thamani ya madini na tatu mimi kama mwana Kilimanjaro, ninyi ni mashahidi tulipoenda juzi kwenye msiba Kilimanjaro, mliona Kilimanjaro hatuna ardhi. Mkoa wa Kilimanjaro ardhi iliyobaki ni kwa ajili ya makaburi ya bibi na babu zetu, hatuna pa kulima. Mimi ninapotetea viwanda hivi vya uchenjuaji vijengwe ni kwa sababu vijana wangu watapata ajira kwenye migodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona nchi ya Botswana ilivyopiga hatua. Miaka 40 wananchi wa pale wamebaki kuwa watazamaji kwenye masuala haya ya uwekezaji wa madini lakini baada ya kubadilisha sheria na kusema kwamba viwanda vya uchenjuaji vijengwe katika nchi ya Botswana ndipo ambapo nchi hiyo imeweza kuchangia asilimia 50 ya pato la ndani katika bajeti yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi vijana wa Chama cha Mapinduzi, sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, tunasema kwamba tuna kila sababu viwanda hivi vijengwe. Tofauti na Mheshimiwa Kaka yangu wa Siha pale, Mheshimiwa Dkt. Mollel, nilishangaa sana tarehe 20 mwezi huu hapa Bungeni aliona hakuna mantiki lakini amesahau vijana hawa wa Kilimanjaro hawana pa kulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitasema hata kama Mwanri hayupo, nitatetea vijana wa Kilimanjaro, nitatetea Siha, Hai, Moshi Vijijini, Moshi Mjini, Same na Mwanga, nitasema bila kuogopa, msiogope vijana wangu mimi nipo. Nitasema nitapaza sauti kwa ajili yenu Kilimanjaro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya lakini pia tukumbuke dada yangu Mheshimiwa Angellah Kairuki hata tungepitisha vifungu vyake mamia na maelfu, hana obsorption capacity ya kutengeneza ajira hizi ni sisi tumsaidie. Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria mimi na wewe ni mashahidi tulienda kufungua mabweni ya Chuo Kikuu pale lakini uliona juhudi za Mheshimiwa Rais, alitoka nje ya mikataba, alitoka nje ya utaratibu akaona kwamba tutengeneze ajira kwa kufanya TBA waweze kufanya kazi, vijana na akinamama waajiriwe ili tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri tunadaiwa, Ilani hii tuliahidi watu, nasema kwamba ifike mahali tujenge viwanda. Nitasoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi maana imeniagiza niseme, ukurasa wa 34 kwenye kipengele cha 10 tumeambiwa pamoja na majukumu haya Chama cha Mapinduzi kitafanya yafuatayo:-
“Kitasimamia na kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini ili kukuza mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasadiki hili na nitalisema siyo leo tu, kesho na kesho kutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika musuala haya ya ajira ukienda ukasoma Public Procurement Act ya Kenya utaona ni kwa namna gani kijana anathaminika katika nchi ile. Katika sheria ile ya Kenya inasema asilimia 30 ya public procurement activities zinafanywa na vijana na kunakuwa na dawati maalum katika Ofisi ya Rais. Mheshimiwa Waziri naomba utusaidie, ulipokuwa Kitengo cha Sheria kama Dean wafanyakazi wako walikuwa na imani sana na wewe, ulikuwa mkali lakini ulikuwa tayari kutetea maslahi ya Tanzania. Nakuomba Mheshimiwa Waziri usiishie kufundisha pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tunadaiwa ajira, Ilani hii imetuagiza tutengeneze ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu gani? Hata Bertha Soka, Mkurugenzi wa PPRA alikuwa hapa Dodoma, kuna siku…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.