Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Gimbi Dotto Masaba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kuwasilisha mchango wangu wa maandishi kuhusu Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Ningependa kuzungumzia kuhusu suala la uwazi katika mchakato wa utoaji haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ni nchi mwanachama wa OGP Open Government Partnership ambapo mojawapo ya misingi muhimu ni Serikali za nchi husika kutekeleza majukumu yao kwa uwazi wa hali ya juu ili wananchi wajue Serikali zao zinavyofanya kazi. Hata hivyo kwa Tanzania hali ni tofauti kwa kuwa uhuru wa habari umeminywa kwa kiwango cha juu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na usiri mkubwa sana katika mchakato wa utoaji haki Mahakamani. Vyombo vya habari vinazuiwa kuingia Mahakamani kuona mwenendo wa kesi, jambo ambalo limesababisha kushamiri kwa vitendo vya rushwa na wanyonge kudhulumiwa haki zao kutokana na usiri uliogubika Mhimili wa Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi jirani ya Kenya, kesi zote zenye maslahi kwa Taifa huwa zinarushwa moja kwa moja kwenye Televisheni na wananchi wanaona mwenendo wa mchakato wa utoaji haki. Kesi za uchaguzi na katiba katika nchi ya Kenya zilirushwa moja kwa moja na Citizen TV. Aidha, kuhusu kesi ya BREXIT ya Uingereza juu ya nani kati ya Bunge na Serikali ya Uingereza anatakiwa kuanzisha mchakato wa kujitoa katika umoja wa Ulaya ilirushwa live moja kwa moja na BBC na dunia nzima ilishuhudia na kuona mwenendo wa utoaji haki. Kwa kutumia mifano ya Kenya na Uingereza, nadhani Tanzania sasa inatakiwa kwenda level nyingine kwa kuruhusu uwazi zaidi katika mchakato wa utoaji haki Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na vyombo vya habari kuruhusiwa kuingia katika vyumba vya Mahakama ili kuripoti mwenendo wa mchakato wa utoaji haki, vyombo hivyo pia viruhusiwe kuwatembelea wafungwa Magerezani ili wafungwa wapate haki ya kueleza fikra na mtazamo wao kuhusu maisha yao Magerezani. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumepiga hatua kubwa ya kudumisha uwazi katika utendaji wa Mahakama, lakini pia tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika kujali haki za wafungwa ambazo ni miongoni mwa haki za binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.