Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Awali ya yote, niwashukuru wananchi wa Jimbo la Buyungu kwa imani kubwa waliyonipa ya kuniamini, kuwawakilisha katika Jimbo la Buyungu na nina uhakika wamepata mwakilishi makini
na sahihi. Kabla sijaanza kuzungumzia vipengele kadhaa nitakavyovizungumzia, nataka niseme kwa ujumla wake, Hotuba ya Rais imesheheni matatizo ya Watanzania. Matatizo makubwa sana waliyonayo Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nilidhani tungekuwa pamoja kama itawezekana, tuone namna ya kuondoa haya matatizo na matatizo yenyewe, hata Watanzania nawashangaa, kwa matatizo yote haya yaliyosababishwa na Chama cha Mapinduzi, wameendelea kukiamini na kukirudisha madarakani. Hapa ndipo ninapopata mashaka makubwa sana. Kwa matatizo lukuki yaliyoko ndani ya Hotuba ya Rais, Watanzania
hawakutakiwa kukiamini Chama cha Mapinduzi na kukirudisha madarakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza maelezo yote hayo, nataka niulize style ya nchi hii sasa hivi tunayokwenda nayo ni ipi? Kuna style imeanza sasa hivi ya kuvamia. Mawaziri wetu wanavamia, wanaweza wakaja Mkoani hata Mkuu wa Mkoa hajui, sasa ni style ipi tunayokwenda nayo. Maana sekta zote tukubaliane zianze kuvamia, walimu nao wawe wanavamia, ukiingia darasani ilikuwa Kiswahili uvamie na wewe ukafundishe somo lolote tu.
Madaktari nao wavamie, yaani sijui ni style ipi ambayo haina work plan. Niwashauri Mawaziri, mtumie work plan, acheni kuvamia vamia. Aliyevamia mmoja tu yule alifanya tu vile msi-copy na ku-paste. (Kicheko)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba dakika zangu zitunzwe, lakini naomba kutoa tahadhari nisifundishwe namna ya kuchangia. Mimi ni Mwalimu, nina uzoefu mkubwa sana na hizi shughuli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilitaka nitoe tu angalizo hili, nadhani wamelichukua na watalifanyia kazi. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais, suala la elimu bure limetajwa, lakini limeleta mkanganyiko kwa wananchi. Sasa hivi hali ya neno elimu bure, nafikiri tungetafuta utaratibu wa ku-define neno bure, kama linaonekana linaleta utata. Kwa mujibu wa maelezo yanavyotolewa na inavyotekelezeka kule, hata Jimboni kwangu kule Buyungu hali ni ngumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, walioko shule za kutwa, wanaona hawajapata ule ubure unaotajwa kama bure. Walikuwa wanalipia chakula shule za kutwa, walikuwa wanachangia michango mbalimbali, chakula kimeendelea kubaki gharama kubwa, kuliko 20,000/= iliyoondolewa, sasa wanatusumbua na sisi Wabunge, hivi kweli hii ni elimu bure? Kama tunasema neno elimu bure, tusiwe na double standard, shule zote ziwekwe elimu bure na kama ni chakula kitolewe kwa wote, hata shule za kutwa wapewe chakula na Serikali na wao ni Watanzania wanahitaji kula ili waweze kupata masomo vizuri darasani.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kwenye elimu kuna matatizo lukuki, bado kuna wazabuni wanadai hawajalipwa, bado kuna walimu wanadai madai mbalimbali ambayo yameshaelezwa na baadhi ya Wabunge waliopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nizungumzie habari za kilimo. Katika kilimo nitajikita kwenye pembejeo. Pembejeo ni tatizo kubwa tunaweza tukasema ni la Kitaifa. Pembejeo zinakuja wakati ambao huwezi kujua huu ni wakati wa kulima, ni wakati wa palizi,
itafika wakati tutaleta mbolea ya kuvunia, kama itapatikana baadaye, lakini naona wakati wa kupanda DAP haipatikani. Unapofika wakati wa palizi ndio DAP inapatikana, yaani mbolea ya kupandia, inapatikana wakati wa palizi. Muda wa palizi unakwenda wakati mwingine, sijui
mbolea ya kukuzia inakuja wakati gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ilikuwa ni hivi, wakati wenyewe wa kuleta mbolea ile siyo wakati muafaka. Wananchi hawana fedha kabisa, ni miezi ambayo siyo ya mavuno, mbolea ikifika wakati wananchi wamevuna, watakuwa na uwezo wa kununua hiyo mbolea na
itatumika muda muafaka majira ya kutumia mbolea yanapofika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nataka nizungumzie, mtaniwia radhi natumia miwani wakati fulani, kodi kubwa kwenye mishahara ya wafanyakazi. Ifikie hatua, Watanzania, wananchi, wafanyakazi wanalalamika kuhusu kodi kubwa. Hili bila kuliangalia,
wafanyakazi tunawapa mkono wa kulia, tunachukua mkono wa kushoto. Lazima tufike mahali tuangalie nchi zinazotuzunguka, tusiwe kisiwa, nchi za wenzetu katika Afrika Mashariki hii wameshafikia single digit. Sisi hapa Tanzania kwenye Vyama vya Wafanyakazi walipoulizia
habari ya single digit kwenye Kodi ya Mapato ya wafanyakazi wanaambiwa itafikiwa mwaka 2018, kuna tatizo lipi? Wafanyakazi hawana amani nalo wanalipwa mshahara, halafu unarudi Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni ya suala la kuimarisha Muungano. Nilitegemea Waheshimiwa Wabunge, suala la Zanzibar tungeliangalia wote kwa pa moja. Zanzibar siyo kwamba siyo sehemu yetu, lakini kunakotokea matatizo Zanzibar, tuyabebe wote kwa pamoja, tuyajadili kwa pamoja. Hapa imefikia hatua ukizungumzia habari ya Zanzibar, unaonekana wewe una matatizo. Hivi kati yetu hapa nani hakuwa kwenye uchaguzi? Baada ya uchaguzi matokeo yako yangefutwa, ungejisikiaje? Wenzetu wamefanya chaguzi tano, zikafutwa nne, ikabaki moja ndiyo salama.
(Hapa kengele ya kwanza ililia)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, niliibiwa muda mtakumbuka hilo. Kama uchaguzi mmoja ulikuwa salama, hizi nne zinakosaje usalama? Tuwe na huruma kwa wenzetu!
Mheshimiwa Naibu Spika, tufike mahali tukubaliane uchaguzi ulio huru na haki, siyo lazima ishinde CCM, muwe tayari kumeza pini, ifike hatua mseme hapa, ngoma ime-tight, tunakubaliana nayo, tunasonga mbele. Mataifa yanatucheka, tunachekwa na Mataifa kufuta
uchaguzi wa nchi nzima mwanzo mwisho, halafu mnabakiza Wabunge wa Jamhuri wenyewe hawa ni halali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda haraka haraka, fedha za Jimbo zimezungumzwa kwenye hotuba hii, nashauri na niungane na Wabunge wengine, fedha hizi ziangalie ukubwa wa Jimbo. Kama hazitaangalia ukubwa wa Jimbo, zitakuwa haziwezi kukidhi mahitaji yaliyokusudiwa katika Jimbo. Kazi yangu siyo kulinganisha ukubwa wa Majimbo, lakini uhalisia wa Jimbo. Fedha zifanane na uhalisia wa ukubwa wa Jimbo.
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa afya, hali ni ngumu sana upande huo, bado wananchi hawana dawa kabisa, hali ni ngumu dawa hazipatikani. Niwaombe Mawaziri waliopo washughulikie hili wananchi waanze kupata dawa. Nakaa karibu na Burundi, kule Burundi
hospitali zake ni nzuri kuliko pale kwetu Kakonko na Watanzania wanaougua wanakwenda kutibiwa Burundi badala ya kutibwa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi Burundi, yaani nchi ndogo kama ile ambayo ina vita ya asubuhi, mchana na jioni, ina dawa nzuri, kwetu tuna amani na utulivu, lakini dawa hatuna!
Naomba hili tuliangalie kabisa, Watanzania waanze kupata huduma za afya ndani ya nchi yao, inaweza ikatusaidia vilevile kurudisha imani kwa Serikali yao, pale ambapo inaanza kupotea.
(Makofi)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia na suala la maji.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bilago tafadhali, naomba ukae muda wako umekwisha.
Nilikuwa pia nimemtaja Mheshimiwa Selasini ameshafika? Tafadhali endelea!