Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Wizara hii muhimu kwa ujenzi wa uchumi wa nchi yetu. Nchi yoyote ile yenye miundombinu imara ya reli, barabara na anga, basi ni dhahiri uchumi wake huwa imara. Bila kuwa na miundombinu imara, kamwe hatutaweza kufikia Tanzania ya Viwanda kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano. Tuwe na barabara zenye kuwezesha usafirishaji wa malighafi kwenda viwandani na kuwezesha mazao kwenda sokoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuwa na reli imara itakayoweza kusafirisha mizigo na kupunguza uharibifu wa barabara zetu, lakini kuweza kusafirisha mizigo mingi kwa wakati mmoja, kusafirisha abiria kwa wingi na kwa muda mfupi. Vile vile tuwe na miundombinu ya anga imara ili tuweze kupokea ndege nyingi toka Mataifa mbalimbali hasa kwenye Majiji kama Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya na Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niweke msisitizo kwenye Uwanja wa Ndege wa Musoma tuwekewe lami kwenye runways na hata kupanuliwe ikiwezekana. Uwanja wa Ndege wa Mugumu Serengeti, ni wakati muafaka ukamalizika ili kuweza kuinua uchumi wa Mara kwa kuongeza idadi ya watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa bado kwenye dhamira ya kukuza utalii, ni vyema Serikali ikafanya tafiti za kina ni nini kilipelekea Shirika letu la ATCL kufanya vibaya toka kuwa na ndege kubwa zaidi ya kumi hadi kuwa na kandege ka kukodi? Sababu awamu hii Serikali imeamua kufufua ATCL kwa kununua ndege, basi ni vyema Menejimenti ya Shirika hili iweze kufumuliwa na kuundwa upya kwa kuweka wafanyakazi wenye weledi na dhamira ya kuendesha Shirika hili na kuona tunakuwa na National Carrier itakayoitangaza nchi yetu na hivyo kuongeza idadi ya watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa lisilokuwa na ndege zake, basi daima uchumi utayumba. Ni dhamira yangu na nadhani matumaini ya Watanzania wengi akiwemo Mheshimiwa Rais kuona tunakuwa na ndege zetu na hivyo kukuza uchumi wetu. Angalizo ni kwamba tuzingatie kanuni, taratibu za manunuzi na kuepuka kununua ndege kwa cash money.
Mhesimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kwamba ujenzi wa barabara ya kuanzia Tarime Mjini kwenda Nyamwaga - Mto Mara hadi Ngorongoro, ijengwe kwa kiwango cha lami ili kuweza kurahisisha usafirishaji wa chakula kati ya Tarime na Wilaya ya Serengeti. Pia kukuza uchumi kupitia utalii, kwani watalii wengi hupitia Sirari kutoka Kenya na kupita njia hii kwenda Serengeti, Mbuga ambayo ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Tarime Mjini na hata Majimbo mengine, tunaomba TANROADs wanapojenga barabara, basi wawe wanaingia angalau mita 20, kama kanuni inavyoelekeza, maana Jimboni kwangu barabara unganishi na TANROADs zimekatika kwenye maungio na kusababisha adha kubwa sana kwa watumiaji. Pia na uchimbaji wa mitaro ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.