Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Omary Ahmad Badwel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuwa miongoni mwa Wabunge watakao changia katika hoja hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini kwa kuwa ndio mara yangu ya kwanza katika awamu yangu hii ya pili ya kuwa Mbunge wa Bahi kusimama hapa katika Bunge lako Tukufu naomba nichukue nafasi hii pia kuwashukuru wananchi wenzangu wa Jimbo la Bahi, kwa kweli kwa kuniamini na kunichagua tena kuwa Mbunge wao na mimi ninawaahidi mbele yako, imani ile ile waliyokuwa nayo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita nitaendelea kupambana nihakikishe mwaka 2020 imani yao inakuwa bado ipo hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mawaziri wote ambao Mheshimiwa Rais amewachagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili leo hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kupitisha bajeti yake katika mwaka wa fedha unaokuja. Nimemsikiliza kwa makini sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na maeneo mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu ambayo ameyagusa hususan amegusa katika uboreshaji na kuleta mapinduzi ya kilimo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni muhimu na nadhani wote tunatambua namna ambavyo kwamba sehemu kubwa ya wananchi katika nchi yetu ya Tanzania wanategemea kilimo. Zipo juhudi mbalimbali ambazo zimefanywa na Serikali zimewatoa walikuma walipokuwa wakilima kwa jembe la mkono kwa sehemu kubwa sasa wanalima kwa zana mbalimbali ambazo wanazitumia na wameongeza uzalishaji. Katika hili nataka nichukue nafasi kumpongeza sana Mheshimiwa Mwigulu, ameanza vizuri na mimi nataka nimtie moyo katika kazi yake ambayo amefanya, sisi tumekuwa tukimfuatilia, kama alikuwa nalala masaa kumi, sasa apunguze alale masaa matano kwa sababu kazi hii ni kubwa ya kupambana kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanapata mabadiliko makubwa ya kimapinduzi na waweze kuvuna kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ambayo yanapata mvua nyingi wachukue hatua ya kuwaendeleza lakini yapo maeneo kama Dodoma ambapo pia hayapati mvua za kutosha na tunahitaji sana kilimo cha umwagiliaji. Katika Wilaya yangu ya Bahi sehemu ya umwagiliaji ni sehemu muhimu kwa sababu ni Wilaya ya ukame lakini tumeanza, miradi ile ni ya muda mrefu imechakaa nilikuwa naomba Wizara ipitie ione namna ambavyo itaboredha na kufufua miradi mbalimbali ya kilimo cha umwagiliaji katika Wilaya ya Bahi ili kuwapunguzia wananchi adha ya kuomba chakula kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nisisitize na niseme wakati tunaendelea kuwahamasisha wananchi kulima na kufanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha kwamba kilimo kinachukua nafasi kubwa katika nchi yetu lazima tuangalie na mambo mbalimbali ambayo yanaweza yakawakuta wakulima hasa wakati wanandelea na zoezi la kulima. Kwa mfano majanga mbalimbali, nilikuwa najaribu kuangalia pamoja na juhudi mbalimbali Serikali bado yapo maeneo inapaswa kujipanga upya. Kwa mfano, unapo himiza wakulima kulima wanakumbwa na majanga mbalimbali, wanakumbwa na ndege waharibifu wa mazao, wanakumbwa na wadudu, wanakumbwa na magonjwa lazima sasa pia tuwe na dhama ambazo zitaweza kupambana na mambo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wananchi wa Bahi wamekumbwa na ndege waharibifu, Mheshimiwa Mwigulu amehangaika sana lakini Tanzania nzima hatuna hata ndege moja yaani ni jambo la ajabu kabisa! Kwamba hakuna hata ndege moja katika nchi yetu ambayo inaweza kumwagilia dawa wakati kuna wadudu au kuna magonjwa au kuna ndege wamevamia mashamba. Tukipata matatizo kama haya tunakwenda kukodi ndege Nairobi, tunakwenda kukodi ndege nchi jirani, hivi maafa haya yakija kwa pamoja nchi zote hizi za Afrika Mashariki Tanzania tutakimbilia wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anajibu hoja hii atuambie katika Bajeti ijayo wahakikishe kwamba wanatenga fedha za kununua ndege kwa ajili ya dharura ya mambo mbalimbali yanayowakumba wakulima. Kwa kweli, hii ni aibu na ni jambo la hatari kwa sababu wakulima wamefanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue nafasi nimshukuru sana Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye kitengo chake cha maafa wakati zoezi linaendelea na Mheshimiwa Mwigulu anahangaika wale ndege wameshindikana alituma watu wa maafa kupitia Brigedia Msuya kwenda kuona namna ambavyo ndege wanashambulia na wenyewe wamejiaonea lakini hakuna kitu cha kufanya. Ndege imekodiwa, imekuja mpaka Dodoma haijafanya kazi unaambiwa ndege haina dawa ya kumwagilia. Sasa hata gharama ambazo ndege hiyo imekodiwa kuja kutoka Nairobi mpaka hapa halafu inafika hapa Tanzania haiwezi kufanya kazi iliyokusudiwa inasema hakuna dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujue hivi katika awamu ijayo wanafanya nini kuhakikisha kwamba hata kama bado wanakodi ndege lakini dawa ipo na maandalizi mengine yamefanyika vizuri.
Nakushukuru sana Mheshimiwa Jenista pia kuagiza sasa waende wakafanye tathmini katika vijiji vyangu vya Bahi ambavyo vimeathirika, vijiji 15 wananchi wale wamerudi kabisa nyumbani mashamba yameliwa ndege wamewashinda kwa hiyo nakushukuru sana na ni matumaini yangu kwamba tathmini hiyo itafanyika mapema kwa sababu wale wananchi chakula walishamaliza toka mwaka uliopita walikuwa wanatarajiwa wavune sasa wapate hicho chakula hawana chakula, siyo kwamba mnakwenda kuwafidia lakini waende wakasaidiwe na Serikali kuhakikisha kwamba wanarudisha maisha yao ya kawaida kupitia janga hili la ndege ambalo wamelipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa habari ya umeme tumetoka REA two tunakwenda REA three. Lakini mtakumbuka bahati nzuri baadhi ya Wabunge tuliokuwa hapa, mimi ni miongoni mwa Wabunge waliolalamika sana katika awamu iliyopita kusahauliwa kwa habari ya umeme katika vijiji vyake. Mimi nadhani ndiyo Wilaya pekee katika nchi nzima, ambayo wakati tunahangaika habari ya umeme ndiyo haikupata umeme hata kijiji kimoja cha REA. Hili halikuwa jambo nzuri ilikuwa ni uonevu kwa Wilaya ya Bahi, wakati Kondoa wanaipa vijiji 56, Mpwapwa vijiji 40, Kongwa vijiji 30, Mkoa huu huu Bahi hauipi hata kijiji kimoja. Namshukuru sana Mheshimiwa Simbachawene baada ya kuona malalamiko yangu hapa yeye akiwa Waziri akafanya kila jitihada ambayo inatakiwa nikapatiwa vijiji vitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vijiji ilikuwa ni kama zima moto ya uchaguzi, kweli wale Wataalamu walikwenda, mkandarasi alipewa ile kazi mpaka ilipofika mwezi wa kumi wakati tunapiga kura vile vijiji vimesimama vyote, hakuna hata mashimo yamechimbwa, nguzo zimewekwa leo tunahesabu miezi minane, mradi ule umesimama.
Mheshimiwa Waziri Mkuu nilikuwa naingoja hii siku ya leo ili nije hapa kwako, kwa sababu mimi nimeenda kushukuru vijiji, sijaenda kushukuru hivyo vijiji vitano nimefanya hivyo kwa maksudi. Sijaenda kushukuru kwa sababu nataka yule uliyemwambia au Serikali iliyomwambia afute vile vijiji vitano tuende naye tukashukuru naye pamoja ili kama tutazomewa azomewe yeye na mimi, kwa sababu kwa kufanya hivi kwa kweli ni kutokuwatendea haki watu wa Bahi mmewanyima vijiji kabisa asilimia mia moja, halafu mmewapa vijiji vitano wameanza kazi ya kuchimba mashimo na kuchomeka nguzo mmekwenda kufuta hivyo vijiji vitano!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kwa kweli siyo sawa mimi naomba maelezo Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwa nini vijiji vimefutwa na lini vijiji hivi vitarudishwa kabla ya REA III, naambiwa sasa vimepelekwa kwenye REA III kitu ambacho siyo sawa. Nataka virudi kwenye REA II wakati inamalizika mwezi wa saba kwa kweli na hivi vijiji viwe vimewaka umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji; kama nilivyosema Mkoa wa Dodoma ni kame na sisi kama Wilaya ya Bahi tuna shida kubwa sana ya maji, tumehangaika sana, Bahi ni Makao Makuu, ni Wilaya mpya na mji mpya ambao sasa ilikuwa kijiji tume- promote kile kijiji kimekuwa Mji uhamiaji umekuwa mkubwa ofisi za Serikali zote zimeamia paleā€¦..
MWONGOZO WA SPIKA
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mwongozo wa Mwenyekiti.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, watu mbalimbali wamehamia pale kwa hiyo panahitaji maji. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana nisisitize Mheshimiwa Waziri Mkuu Mji huu wa Bahi utizamwe kwa jicho la umakini.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa!
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Badwel naomba uketi....
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, siikubali taarifa nadhani hajui cheo cha Waziri Mkuu ni nani.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiye Mkuu wa Mawaziri wote, kwa hiyo, hata ninapomueleza hapa atatoa maelekezo kwa Wizara husika kufanya kazi ambayo mimi naisema hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hasa ukizingatia nafasi zetu hapa ni ndogo, unapopata fursa kama hii ni vizuri kuwasemea wananchi. Inawezekana nimechangia hapa nisipate fursa ya kuchangia mahali pengine na mimi ni Mbunge kama yeye na Jimbo na yeye ana Jimbo aniache nifanye kazi walionileta wananchi wa Bahi. Simuingilii kwenye Jimbo lake kama hana cha kusema arudi nyumbani kwake Jimboni akafanyae kazi za Jimbo kule asikae hapa Bungeni lakini sisi tunayo mambo ya kusema nitaendelea kuyasema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza habari ya maji Mheshimiwa Waziri Mkuu, Bahi hakuna maji najua unanisikiliza na kwa kauli hii ya Mbunge ambaye hataki wewe uambiwe juu ya maji, utapeleka maji Bahi ili wananchi wajue kazi niliyoifanya hapa ilikuwa na tija na sikuja kufanya mchezo hapa. (Makofi)
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ilikuwa ni habari ya sheria mbalimbali. Wizara yako Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiyo inasimamia Tume ya Kurekebisha Sheria, zipo sheria nyingi sana zimepitwa na wakati, ni vizuri Serikali ikatafuta utaratibu mzuri wa kuziangalia sheria hizi mbalimbali ili ziweze kufanyiwa marekebisho ziweze kutoa tija iliyokusudiwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunapitia kwenye Kamati zetu hususan Kamati ya Katiba na Sheria, tumeona namna ambavyo Tume ya Sheria inapitia sheria moja kwa miaka mitatu, inafanya uchunguzi wa mapitio ya sheria moja kwa miaka mitatu! Mimi nadhani huu ni muda mrefu sana, unatenga fedha mwaka huu milioni 800 kuipa Tume ya Kurekebisha Sheria kuangalia sheria tatu tofauti, mwakani haijamaliza unatenga tena milioni 800, mwaka unaofuata milioni 800, utakuta zaidi ya bilioni mbili zinatumika lakini yale makusudio ya kurekebisha ile sheria bado hayajafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani mkae muangalie namna nzuri ambapo itaweza kufanya hii Tume ya kurekebisha sheria nyingi kwa wakati mmoja ili ziweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia unasimamia Tume ya Haki za Binadamu. Hii Tume ya Haki za Binadamu imesahauliwa kabisa na Serikali. Ukiangalia katika bajeti ya mwaka huu, Tume hii imepewa pesa ya pango tu kwamba pale wanapokaa waweze kulipia ofisi, sidhani kama hiyo ndiyo kazi ya Tume ya Haki za Binadamu. Tume ya Haki za Binadamu ina kazi nyingi, kama Serikali ipo serious kuhakikisha kwamba haki za wananchi zinapatikana waiangalie hii Tume ya Haki za Binadamu, waipe fedha za kutosha ili iweze kufanya ufuatiliaji mbalimbali wa mambo yanayohusu haki za binadamu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nizungumzie habari ya fedha milioni 50 ambazo tunatarajia kwenda kuzipata katika vijiji vyetu, tunaomba kwa kweli utaratibu uandaliwe vizuri na pengine sisi Wabunge tushirikishwe kuletewa utaratibu huo ili tuweze kujua fedha hizi zinakwenda kugawiwa vipi na zitumikeje katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka yalikuwepo mabilioni ya Kikwete yalikuja hivi tu kwa matamko, lakini baadaye fedha zile zilitoweka hatukujua zimekwenda wapi, tunatamani sana kuona fedha hizi safari hii zinakwenda kila kijiji zinawekewa utaratibu mzuri na Wabunge ambao tunakaa kule tunajua vikundi vyetu tunajua wananchi wetu uchumi wao, tushirikishwe vizuri ili na sisi Wabunge tuweze kutoa ushauri kusaidia yale madhumuni ya milioni hamsini kupelekwa katika kila kijiji yaweze kufanya kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana, naunga mkono hoja.