Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Uchukuzi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara na wataalam wake, naomba nishauri kwamba viwanja vya ndege vikarabatiwe na hasa kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Njombe. Kiwanja hiki kimeharibiwa sana na watu wanaopita katikati ya kiwanja, hata magari yanapita uwanjani. Hii ni kutokana na uwanja kuwa katikati ya mji. Naiomba Serikali itengeneze uwanja huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha watu wa Njombe na kutenga fedha kwa ajili ya barabara ya Itoni – Ludewa – Njombe – Makete – Kibena – Lupembe – Madeke. Naiomba Serikali kuhakikisha kwamba fedha hiyo iliyotengwa inapelekwa ili kazi ianze kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa barabara za vijijini katika maeneo mengi na hasa katika Mkoa wa Njombe ni mbovu, naiomba Serikali kuangalia tatizo la wananchi vijijini hasa wanawake wajawazito ambao wanapoteza maisha kwa sababu ya barabara mbovu. Naiomba Serikali itengeneze barabara za vijijini ili kupunguza vifo vya akinamama na watoto wachanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akinamama wengi ni wakulima wanaojitahidi kuzalisha mazao ya chakula na biashara lakini wanashindwa kusafirisha kwa sababu barabara hazipitiki, hasa wakati wa masika. Kwa mfano wananchi wa Mamongolo, Makowo, Ng’elamo, Matola, Iwungilo. Maeneo hayo yanazalisha kwa wingi viazi, ngano pamoja na chai lakini kipindi cha kifuku hayapitiki. Naiomba Serikali itusaidie ili maeneo hayo yaweze kupitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Mawasiliano. Maeneo mengi katika Mkoa wa Njombe hakuna mawasiliano ya simu. Kwa mfano, katika Wilaya ya Ludewa maeneo yote ya mwambao kama Vijiji vya Lupingu, Ibumi, Lifuma na Kilondo hayana kabisa mawasiliano, naiomba Serikali iweke minara ya simu katika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Wilaya ya Makete, maeneo ya Matamba, Kiteto na maeneo mengine mengi hakuna mawasiliano kabisa, naiomba Serikali kupeleka minara katika maeneo hayo. Kutokana na ukosefu wa mawasiliano husababisha akinamama kupata matatizo
makubwa ya kupata msaada wakati wa kujifungua kwa sababu wanashindwa kuwasiliana na vyombo vya usafiri ili wawahishwe hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.