Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natoa pongezi kubwa sana kwa spidi na kasi nzuri sana ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano. Naunga mkono juhudi zote anazozifanya na kasi hii inatakiwa iungwe mkono na viongozi wote na wananchi wote kwa ujumla. Anatibu majipu, anatibu matatizo ambayo yamekuwa sugu katika jamii na kwa namna hii, natabiri kwamba, nchi yetu sasa hivi italeta mapinduzi makubwa sana kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipitie hotuba ya Waziri Mkuu kuwasilisha ombi la Mji Mdogo wa Namanyere kuomba kuwa Mamlaka ya Mji wa Namanyere. Wilaya ya Nkasi iko pembezoni na mara zote mmekuwa mkitutolea mfano kwamba tuko pembezoni na maendeleo yetu yako chini. Namna ambayo mnaweza kutusaidia na kutuimarisha ni kutusogezea maeneo ya kiutawala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Namanyere una zaidi ya watu 135,000, eneo la kilometa za mraba zaidi ya 16,000, ina bajeti zaidi ya shilingi milioni 359, ina Makao Makuu ya Tarafa, Makao Makuu ya Wilaya, Polisi, Sekondari saba, Chuo cha St. Bakhita kinachokusanya watu karibu 1,000 na ina Hospitali ya Wilaya. Kwa msingi huo, tunakidhi vigezo vingi vya kuwa Halmashauri ya Mji.
Tunajua mkitupa Halmashauri ya Mji mtakuwa mmetusukuma na kutusaidia katika matatizo mengi yanayotukabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupitia nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, niwasilishe ombi rasmi na lishughulikiwe na maombi tumeshapeleka mezani. Tuna Kata 10 tayari na Madiwani tumeshafanya uchaguzi. Kwa hiyo, kwa sasa tuna uwezo kabisa wa kuwa Halmashauri. Hilo ni ombi la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni sekta ya kilimo. Mimi wapiga kura wangu wengi ni wakulima. Miaka mitano yote niko Bungeni lakini sijaona mabadiliko makubwa katika sekta hii. Tumekuwa tunazungumza tunagusagusa na matatizo sugu hayajawahi kushughulikiwa inavyotakiwa. Kwa mfano, suala la utawanyaji wa pembejeo sijaliona kama limekuwa likienda vizuri na nimekuwa nikichangia hapa kila mwaka mabadiliko sijawahi kuyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wanapelekewa pembejeo muda sio muafaka, wananchi wetu wanaoitwa walengwa pembejeo za ruzuku hawapati. Namwomba mtumbua majipu aelekeze nguvu zake eneo hili la pembejeo za wakulima wanyonge. Haki yao haifiki inavyostahili, haifiki hata kidogo.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Nashangaa hata ruzuku ya mifugo haifiki inavyotakiwa, wavuvi hawapati ruzuku yoyote, hii sekta yote ni kilimo kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kuwaombea wakulima ruzuku ipatikane kwa wakati. Pia mtafute mwenendo mzuri, mbuni mbinu nzuri kama mnavyobuni za kukamata hawa mafisadi, mnavyokamata wauza madawa ya kulevya sasa hivi, hii Serikali ina mbinu ambazo hata hatukuzitegemea kuwepo, ni kama kitu kimekuja ambacho hatukukitarajia, naomba muelekeze nguvu hiyo kwenye kilimo ili mboreshe kilimo. Kilimo kinatuajiri Watanzania 75%, kilimo kinatuchangia hela nyingi za kigeni, kilimo kinaleta utulivu na amani ya nchi kwa kuwepo kwa usalama wa chakula, kwa hiyo, kina kila umuhimu. Sisi Mkoa wa Rukwa ni wakulima na maeneo yote ambayo yanalima wasaidiwe kuangalia kwamba vigezo kama hivi vinazingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya ya kilimo yanahitaji kupata miundombinu ya usafiri. Barabara zinazoelekezwa katika maeneo ya kilimo bado ni mbovu. Barabara ya kutoka Sumbawanga kwenda Mpanda inayojengwa kwa kiwango cha lami imekuwa ikicheleweshwa tu.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Miaka saba tuko hapa Bungeni hatuioni hiyo barabara inakwisha kwa nini? Tukitembea sehemu nyingine nchini tunakuta kuna wakandarasi wenye nguvu na miradi inakwenda kwa speed zinazotakiwa, kwa nini kwetu kwa sababu ya upembezoni? Naomba mliangalie, Sumbawanga, Rukwa, Mpanda kote huku barabara haziendi vizuri kwa sababu ya upembezoni wake, lakini sasa ni awamu nyingine mtazame wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni maji. Matatizo ya maji katika Jimbo langu na vijijini kwa ujumla ni kubwa sana mliangalie kwa umakini. Nikitolea mfano katika Jimbo langu kuna mradi wa kutoka Kate kupeleka maji Isale ambayo yangeweza kusaidia vijiji karibu saba vya Ntemba, Ntuchi, Isale katika mtiririko mzima wa njia hiyo ya maji. Naomba mradi huu pamoja na miradi mingine iliyoko King’ombe ambayo haijakamilika, tumepeleka zaidi ya shilingi milioni 500 amesema Mzee Keissy hapa kwamba kuna pesa zinatumika visivyo, zaidi ya shilingi milioni 500 lakini huoni maji hata kidogo yanatoka. Nafikiri muangalie yapo majipu kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa maji Vijiji vya Nkundi na Kalundi bado haujakamilika, upo mradi Kijiji cha Chala bado haujakamilika, Kijiji changu cha Kasu hakuna mradi wa kutosha wa maji kakamavu kama tunavyoweza kuona katika sehemu nyingine. Kijiji cha Wampembe, Kijiji cha Namansi bado kote huko kuna matatizo ya maji naomba mtusaidie kupitia bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia bajeti hii naomba pia suala la mtandao wa mawasiliano. Nashukuru Serikali kwa kazi nzuri iliyofanyika katika Kata ya Ninde na ya Wampembe. Bado kuna dosari ndogo ndogo ili kukamilisha kazi hiyo, lakini Kata ya Kala ambayo ina tatizo kubwa zaidi bado kuna nini? Bahati nzuri Waziri ni yule yule ambaye alikuwepo. Sasa nakwambia katika bajeti yako siwezi kupitisha kama huwezi kupeleka au kunipa majibu mazuri ya kupeleka mtandao Kala. Sehemu zingine hizi umejitahidi vya kutosha lakini nataka kujua Kala kwa nini? Pembezoni kila siku tunakuwa wa mwisho, kwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni suala la umeme. Mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika Vijiji vya Kata ya Wampembe, Ninde na Kala hazijafikiriwa kabisa katika suala zima la umeme. Katika Jimbo langu la Nkasi Kusini maeneo kama vile Vijiji vya Kate, Katani, Nkomolo II, Kisura na Malongwe tulikwishasema kwamba sasa hivi wangeweza kupata umeme, lakini mpaka sasa navyosema umeme haujawashwa. Wanapelekwa Wakandarasi goigoi hawafanyi kazi inavyotakiwa. Naomba muwabadilishe mlete wenye nguvu ili waweze kuleta matarajio ya wananchi haraka. Kilimo hakiwezi kwenda vizuri kama hata umeme wenyewe unasuasua namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa kupeleka umeme mkubwa katika mikoa ya pembezoni ikiwa ni pamoja na Rukwa, Kigoma na Katavi kutoka kwenye grid ya Taifa. Naomba isiishie maelezo tu ambayo tunayasikia hapa kwamba utafiti unaendelea. Tunataka tuone angalau katika bajeti hii umeme mkubwa ufike Sumbawanga ili mazao na mahindi yaliyopo ya wakulima wale yaweze kuchakatwa vizuri, ili samaki ambao wako mwambao mwa Ziwa Tanganyika minofu yake iweze kuchakatwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunakuwa watumwa wa watu wa Zambia, minofu yetu inapelekwa Zambia, halafu inasafirishwa Afrika Kusini kwa sababu tu hatuna umeme wa kutosha. Wavuvi wetu kule wanakuwa maskini wakati hawastahili kuwa maskini kwa kweli wanacheleweshwa kwa nini? Naomba umeme safari hii ufike Kirando, Wampembe, Ninde, Namansi kwani itakuwa ni ukombozi mkubwa sana wa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni barabara za Halmashauri. Zipo barabara ambazo nilikuwa nasaidiwa sana na Mheshimiwa Rais ambaye alikuwa Waziri. Barabara ya Kitosi – Wampembe, barabara ya Ninde, barabara ya kutoka Kasu - Katani - Nyula, barabara hizi Halmashauri haiziwezi. Tunaomba msaada zaidi kwa sababu sasa hivi karibu zitafunga, bila juhudi za ziada kutoka Serikalini tutaaibika. Naomba ni maeneo ya wakulima wengi na tunatakiwa kuhakikisha kwamba barabara zinapitika. Hii ni pamoja na barabara kutoka Milundikwa - Kisula pamoja na Malongwe. Ni barabara sumbufu na zinasumbua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa sababu muda unaniruhusu ni suala la zahanati. Tumesema kila kijiji kipate zahanati, lakini zipo zahanati ambazo zilishajengwa hazijafunguliwa bado kuna nini? Ipo Zahanati ya Nkomolo II na Msilihofu bado hazijafunguliwa rasmi ili ziweze kuwekwa kwenye utaratibu wa kuletewa dawa hizo zinazoweza kupatikana kwa njia ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuangalie sana Hospitali ya Wilaya ya Namanyere. Hospitali ya Namanyere ni DDH, iko chini ya Kanisa la Roman Catholic. Utaratibu wa huduma umezorota kupita kiasi. Naomba Serikali itimize wajibu wake kwa hospitali hii lakini na wale wanaohusika juu ya uchunguzi na uangalizi…
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako ndiyo huo, tunakushukuru sana.

Whoops, looks like something went wrong.