Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Vyuo Vikuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii. Pamoja na kwamba dakika ni tano lakini mimi kama Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii sitaacha kuipongeza Serikali yangu pamoja na Mheshimiwa Waziri kwa juhudi kubwa walizozifanya kwa muda mfupi katika kuboresha huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tumejionea, ukiangalia pale Ocean Road akina mama wengi wanafariki kwa sababu ya cancer lakini kumeboreshwa kwa hali ya juu. Sasa hivi kusubiri mionzi sio miezi mitatu ni wiki sita na tunaelekea wiki mbili, huduma ya dawa kutoka asilimia nne mpaka asilimia 60 bado vifaa vya kupima pamoja na PET Scan ambayo itapunguzia gharama Serikali lakini pia kuokoa maisha ya Watanzania hususan wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri atusaidie Mkoa wetu wa Morogoro, ni mkubwa sana tuna Wilaya nane, lakini Hospitali za Wilaya ni chache sana. Kwa hiyo, ili kupunguza vifo vya akina mama inabidi kwa kweli uliangalie suala hili ingawa kwako inakupa shida sasa inabidi uende TAMISEMI ndiyo maana tulisema kama inawezekana Waziri wa Afya ashuke mpaka chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijikite kwenye Idara ya Maendeleo ya Jamii. Idara hii inachukuliwa kama kitu ambacho hakina umuhimu na mpaka kuna viongozi wa kitaifa wakisimama wanasema hawa walioajiriwa hawaoni kazi yao, lakini wanasahau kwamba Idara ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ndio engine ya maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Sasa hivi Tanzania wananchi hawaelewi, hamna mtu wa kuwaunganisha wananchi na Serikali yao, utakuta wanaunganishwa na wanaharakati. Mwanaharakati hata siku moja haisaidii Serikali, kazi yake ni kukosoa lakini hawa Community Development Officer na Social Workers ndio kiini na ndio hasa engine ya maendeleo. Kwa hiyo, tunaomba hii fedha sasa iliyotolewa itolewe yote muende kufufua sekta hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, watu wanafikiri kwamba uchumi unaletwa na wanauchumi na sayansi asilia, siyo kweli. Baada ya industrial revolution watu walipata social problem nyingi, wana-commit suicide, wanatumia dawa za kulevya, family breakdown, watoto wa mitaani, maadili, sisi tunabaki kupiga makelele lakini kazi kubwa ni hii ya Idara ya Maendeleo ya Jamii. Tukiweza kuiboresha wao ndio wanaotafuta solutions kwamba wafanye nini katika jamii yao. Utakuta sasa hivi hata barabara ikiharibika wanasubiri Serikali, kujenga vyoo wanasubiri Serikali kwa sababu hakuna mtu wa kuwaongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, sana Idara hii ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ipewe kipaumbele. Ikiwezekana sasa tuboreshe vyuo vyetu kama cha Tengeru, kule kumechakaa, hakuna training, watu hawana new skills, tunategemea maendeleo yatatoka wapi? Tusione kwamba maendeleo ni kitu kingine hapana, tuanzie hapa chini. Kwa hiyo, naomba sana Serikali yangu Tukufu iweze kuangalia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba sasa niongelee suala la UKIMWI. Wale watu wanaoishi na VVU tunaomba halmashauri iwasaidie wapate CHF ili waweze kupata septrin wanaumia sana kule, hakuna dawa na vitu vingine. Kwa hiyo, ombi lao kubwa dawa hizi za septrin ziweze kupatikana ingawa ni sehemu ya Halmashauri, lakini sasa ndiyo bado tunarudi kwenye changamoto ileile kwamba Wizara ya Afya kama itaishia kwenye sera haiwezi kuangalia utekelezaji wa sera zake mpaka huku chini bado tutaendelea kupata matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.