Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyenzi Mungu muumba mbingu na ardhi kwa kunijalia uzima.

Pili, nikushukuru nawe kwa kunipa fursa hii adhimu nami kuchangia katika Wizara yetu hii muhimu sana. Nimpongeze kidogo Mheshimiwa dada yangu Ummy Mwalimu kwa kazi kubwa anayofanya, hasa kwa uwasilishaji mzuri aliyoufanya jana. Kwa kweli wakati anawasilisha Dada Ummy niliamini kabisa kwamba matatizo yetu yamekwisha. Vilevile nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati kwa kutuonyesha wazi kwamba pamoja na maelezo mazuri ya Mheshimiwa Dada Ummy lakini Wizara hii bado ina matatizo lukuki, hata bajeti waliyopewa haikufika zaidi ya asilimia 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kabisa kabisa hotuba ya Kambi ya Upinzani. Nimpongeze Dada yangu Mheshimiwa Ester kwa uwasilishaji mzuri na kuonesha matatizo yaliyopo kwenye Wizara yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina Sera ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo imetolewa mwaka 2007. Katika sera yetu hii ukienda ukurasa 10 ambao unaeleza afya ya msingi ukienda kwenye ukurasa wa 11 nitayasoma madhumuni ya sera yetu hii. Madhumini ya sera yetu hii ni kupanua dhana ya afya ya msingi na kuwa na huduma bora za afya zinazoendana na wakati, endelevu na zinazowafikia wanachi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye tamko la sera namba moja na namba mbili, tunaambiwa Serikali itahakikisha wananchi na sekta mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya katika ngazi zote ili kuboresha afya.
Pili, Serikali itaimarisha uendeshaji na usimamizi wa huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera hii imeingizwa kwenye utendaji kwa kutumia Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Tumeambiwa mara nyingi hapa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesema itajenga zahanati kila kijiji. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesema itajenga kituo cha afya kila kata. Tumeambiwa mara nyingi hapa kwamba hii Ilani ndiyo imefanya wananchi kukiamini Chama cha Mapainduzi. Na mimi kwa kweli nitakuwa Wakili wa wananchi kuhakikisha Chama cha Mapinduzi wanatekeleza Ilani yao hii, Ilani ambayo ilikuwa ndiyo sababu wananchi kuwaamini. Wasipotekeleza tafsiri yake wamewarubuni wananchi, wamewalaghai wananchi, hawatekelezi yale ambayo ilikuwa ndiyo sababu ya kupewa madaraka ya kuongoza nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makubaliano ya Abuja ya mwaka 1989 Serikali zetu za Afrika walikubaliana Wizara ya Afya itengewe walau basi asilimia 15 ya bajeti, bajeti yetu hapa ni shilingi trilioni 31, asilimia 15 ni shilingi trilioni
4.5. Sisi tumetenga shilingi trilioni 1.1. Kwa utaratibu huu hivi kweli tuna malengo ya dhati ya kuhakikisha tunapunguza vifo vya akina mama? Hivi kweli tuna malengo ya dhati ya kuhakikisha tunapeleka afya ya msingi kwa wananchi wote kama sera yetu ilivyosema?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwe wakweli, tuhakikishe basi walau niungane na senior kaka yangu Mheshimiwa Mbatia pale, bajeti hii basi walau tufanye asilimia tano ambayo itakuwa ni shilingi trilioni 1.5, na hii asilimia tano tukiiweka tuongeze madaktari, tuna madaktari wanazungukazunguka tumewasomesha kwa gharama kubwa, kwa nini tusiwaajiri madaktari na wahudumu wa afya, wafanyakazi wote wa idara za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tushirikiane na Halmashauri kuhakikisha tunajenga hizo zahanati kila kijiji, tuhakikishe tunajenga vituo cha afya kila kata. Kama tuna nia ya dhati ya kumsaidia mama na mtoto, kuwasaidia watu wetu hawa, tuwe na zahanati kila kijiji kwa sababu kule ndiyo huduma itamfikia mwananchi. Vifo vya akina mama vinasababishwa na kutokwenda kliniki, hawapati huduma za kliniki, huduma ya kliniki zahanati isipokuwepo kijijini ataipatia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, hospitali yetu ya Mwananyamala, mimi ni Mbunge wa Jimbo Kinondoni, hospitali ya Mwananyamala imepandishwa hadhi, imekuwa ya rufaa, jambo la kusikitisha Serikali hawatoi fungu lolote la uendeshaji wa hospitali ile, badala yake imekuwa gharama kwa Halmashauri na Manispaa ya Kinondoni. Uendeshaji wa hospitali ya Mwananyamala inatugharimu karibu shilingi bilioni 6.9 kila wiki. Mbaya zaidi tumepewa tena jukumu, kwa kuwa hospitali yetu imekuwa ya rufaa tunatakiwa tujenge hospitali ya Wilaya. Serikali ipo kimya haitusaidii chochote kwenye ujenzi ya Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali yetu ya Kinondoni kwa maana ya Mwananyamala katika Jimbo letu na Wilaya yetu ina zaidi ya watu milioni moja. Msongamano umekuwa mkubwa na msongamano ukubwa wake unatokana na kwa sababu hatuna Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, naomba Wizara ije kutuambia ama wapeleke fedha za ruzuku kwenye Hospitali ya Mwananyamala au watusaidie kujenga hospitali ya Wilaya ambayo ipo Mabwepande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hali ngumu sana katika Hospitali yetu Mwananyamala. Dawa tunapata MSD, wakati mwingine dawa tunazozitaka wakati mwingine MSD hawana, Wanapokuwa hawana MSD hamna njia mbadala. Hakuna chombo kingine kinafanya ushindani na MSD. Ukitaka kununua dawa nje ya mfumo wa MSD unatakiwa ufuate mfumo wa manunuzi. Hivi leo dawa tunatumia kama tunataka kununua kipuli cha gari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima Wizara ituletee njia mbadala ama MSD ipate mtu wa kufanya naye kazi mbadala wake au itupe kibali tunapokuwa tunahitaji dawa tusifuate utaratibu huu wa manunuzi ambao unatupa taabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hatuna vifaa na gharama za hivi vifaa vya upimaji ni gharama kubwa, Serikali ituambie ina mpango gani wa kutumia utaratibu wa PPP (Public Private Partnership) kwamba watu binafsi hasa hospitali zetu za Mjini, watu wana fedha wanataka kutibiwa matibabu mazuri, wako tayari kuchangia gharama na watu binafsi wanaweza wakatoa kununua mitambo kwa gharama zao, tukafanya partnership. Serikali inasemaje, imeshindwa hilo basi Serikali kutudhamini kwenye mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu ukitaka kununua kitu kwa mkopo, ukitaka kukopa banki lazima upate dhamana kutoka Serikali, Serikali inasemaje katika hili, lazima Serikali itudhamini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni afya ya msingi. Elimu ya msingi Mheshimiwa Magufuli amesema bure namshukuru sana na nampongeza. Je, afya ya msingi kwa nini isiwe bure? Hivi wananchi hawa wanaoenda kutibiwa kwenye zahanati kuna shida gani hawa wakitibiwa bure? Ukiangalia kundi kubwa ambalo linakwenda hospitali mara kwa mara tayari linatibiwa bure, wanawake, watoto chini ya miaka mitano, wazee wanatibiwa bure, wagonjwa wa kifua kikuu, wagonjwa wa HIV, kisukari, wanatibiwa bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile watu tunachangia huduma katika Mifuko ya Kijamii ya Afya. Sasa ukiangalia ukiondoa makundi hayo ambayo ndiyo yako mengi hospitali huyo anayelipia ni nani? Kwa nini Serikali sasa isikubali kwa afya ya msingi watu wetu wakapata huduma ya bure? Na kwa sababu tayari tunatoa bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Hospitali yetu Mwananyamala tunataka tuongezewe wafanyakazi. Sisi kwa kutwa tunahudumia watu 2,500 ukiondoa watu 1,500 wa methadone jumla tunahudumia watu 4,000.