Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Godfrey William Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya, vilevile kushukuru sana Serikali na Wizara kwa ujumla kuanzia Mheshimiwa Ummy, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kuzifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mambo machache sana, jambo la kwanza ningependa kuanza na suala la mkanganyiko ambao upo kati ya TBS na TFDA. Tatizo tunaloliona hapa ni mkanganyiko au muingiliano wa kazi kati ya taasisi hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwamba katika maeneo mengi taasisi hizi mbili zinaingiliana katika utendaji wake wa kazi, na katika kutenda kazi unakuta kuna mambo ambayo yanaendelea katika taasisi hizi ambazo zipo kwa mujibu wa sharia, kwamba unakuta wakati kwa mfano, misaada inatolewa kutoka kwa wahisani mbalimbali nje ya nchi, misaada ile inapokuja nchini kunakuwa kuna mkanganyiko hapa, TFDA wataingia, TBS wataingia vilevile, TFDA kuna charge nyingine ambazo wanaziweka kwa ajili ya misaada hii ambayo tunapewa kutoka kwa wahisani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nchi yetu tuinajua, bajeti iliyoelezwa ni bajeti kubwa lakini ni lazima tuwe wazi kwamba bajeti iliyopita ilikuwa finyu sana vilevile haikutekelezeka kwa asilimia nyingi, sasa tunapopata fedha hizi au tunapopata misaada hii kutoka kwa wahisani halafu inavyofika bandarini inatozwa kodi kubwa, kwa mfano, magari ya wagonjwa, vifaa tiba na kadhalika, inapofika wakati Serikali inatoza kodi za namna hii, inarudisha nyuma maendeleo katika sekta hii ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaona kabisa kwamba hata wananchi wetu kule vijijini wanakosa huduma hizi kwa sababu ya urasimu ambao upo katika taasisi mbalimbali za Serikali hasa pale TRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambaye hata hivyo kipindi cha nyuma aliliongelea hili suala akatoa majibu kuhusu tatizo hili, ningependa sana kumsihi tena kwa mara nyingine Waziri wa Fedha aweze kuliangalia suala hili ili tunapopata misaada kutoka kwa wahisani iweze kupita bure katika bandari zetu na huduma hizo ziweze kuwafikia wananchi moja kwa moja, kwa sababu tatizo la afya bado ni kubwa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nigusie sasa suala kubwa ambalo lipo Jimboni kwangu Kalenga. Nimeongea sana na ninaomba nirudie tena kwamba Jimbo la Kalenga na Jimbo la Isimani katika Wilaya ya Iringa Vijijini tuna tatizo la gari la wagonjwa. Narudia tena kwa sababu tatizo hili ni kubwa. Wilaya ya Iringa Vijijini ina zaidi ya watu 300,000, tuna gari la wagonjwa ambalo ni hiace, kwa kweli kwa miundombinu tuliyonayo halikidhi mahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mwezi, akina mama ambao wanajifungua ni zaidi ya 200 ambao wanatoka maeneo mbalimbali lakini inahudumia majimbo mengine hata Jimbo la Mheshimiwa Mwamoto pia lipo katika huduma hii, hivyo ningependa sana Serikali iweze kuona uzito wa kutupatia ambulance katika Hospitali ya Ipamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea hili suala kwa muda mrefu na ninachokiomba zawadi pekee ambayo nitaiomba kutoka kwenye Wizara, Mheshimiwa Dada Ummy, Mheshimiwa Kigwangalla zawadi ambayo mtanipa mimi katika miaka hii mitano naombeni mnipe ambulance katika Hospitali ya Ipamba ili tuweze kuokoa maisha ya wananchi katika Jimbo letu, tuweze kuokoa maisha ya Watanzania katika Jimbo la Kalenga, tuweze kuokoa maisha ya Watanzania ambao wapo katika Wilaya ya Iringa vijijini. Ni muda mrefu kwa kweli inasikitisha sana kama Serikali ambayo tumeona kwa namna moja au nyingine maeneo mbalimbali ambulance zimepelekwa, ninaamini kabisa Serikali itafanya namna tunaweza tukapa ambulance katika Jimbo la Kalenga, katika hospitali hii ya Ipamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kuongea sana, nimshkuru sana Mheshimiwa Waziri Ummy pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Kigwangalla kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Kigwangalla ulikuja Jimboni, umefanya kazi nzuri na wananchi bado wanakukumbuka na wamenipa salamu kwamba wanaomba yale uliyowaahidi waweze kutekelezewa. Na mimi nitaendelea kuongea haya na kuendelea kuwapongeza Serikali kwa sababu ninaamini Serikali hii ya Awamu ya Tano imejizatiti vizuri kabisa katika kuhakikisha sekta hii ya afya inakua na inaenda kuwafikia wananchi moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana niweze kukushukuru na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.