Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Yosepher Ferdinand Komba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuunga mkono hoja ya hotuba ya Kambi ya Upinzani. Ninaamini yapo mazuri mengi ambayo Serikali ikiamua kuyafuatilia na kuyatekeleza tunaweza tukafikia lengo la Tanzania yenye Watanzania wenye afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuzungumzia vifaa tiba. Kumekuwa na tatizo kubwa sana, Dada yangu Waziri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu unafahamu, wewe ni wa Mkoa wa Tanga, unafahamu hali ya Hospitali ya Bombo, unafahamu kwamba kuna changamoto kubwa sana ya vifaa, kuna changamoto kubwa sana ya mashine za x-ray, kuna changamoto kubwa sana ya vifaa. Lakini pia mmeweka duka la MSD pale, lakini mara nyingi na lenyewe pia linakosa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pana duka la MSD ambalo mmeliweka pale lakini inafikia hatua mgonjwa anatibiwa Bombo anaambiwa atoke akanunue dawa nje ya Bombo, kwa hiyo niwaombe sana na pia tumesikia tunaomba Waziri utakapokuja kuhitimisha utuambie, tumesikia jamii ya Mabohora wametoa msaada wa CT Scan, we are not sure utakuja kutuaminisha, lakini inasemekana kwamba hakuna eneo la kufunga zile mashine. Kwa hiyo, mashine zimetolewa zimewekwa pending, wananchi wanahitaji huduma hakuna pa kuweka mashine. Tunakuomba Waziri utakapokuja hapa utuambie kama kweli hakuna eneo, ni lini na mkakati gani mmepanga kwa ajili ya kujenga jengo kwa ajili ya kufunga hizo mashine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni bima ya afya. Kumekuwa na changamoto kubwa sana kwa watumiaji wa bima ya afya, pamoja na kuwa bado idadi ya watumiaji ni ndogo, ni asilimia nane tu ya Watanzania. Bima ya afya ukichukulia Wilaya ya Muheza wananchi wanachangia shilingi 10,000 ambapo wanatumia kwenye zahanati na kwenye Hospitali ya Wilaya, lakini katika ile bima ya afya tunaomba Serikali kupitia Wizara iandae utaratibu wa kuwa na maduka katika kila Hospitali ya Wilaya ambayo yatasaidia wale ambao wanakosa dawa kwenye hospitali kwenda kupata dawa kwenye maduka ambayo yanaweza kupokea bima. Kwa sababu ukikosa dawa kwenye hospitali kwa kutumia bima hakuna namna unaweza kupata dawa nje ya pale na wananchi wanapotumia bima wanaamini hakuna namna wanaweza kutumia hela zaidi ya kupata ile huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna magonjwa ambayo siyo ambukizi yanazidi kuongezeka kwenye nchi yetu kama kisukari, pressure, magonjwa ya wanawake yanayoambatana na uzazi, shingo ya kizazi na mambo mengine. Ninaiomba Wizara ije ituambie ina mkakati gani wa dhati kwa ajili ya kushughulikia suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee hapa kuhusu watoto wa kike, masuala yanayoambatana na uzazi. Kumekuwa na hilo tatizo kubwa tunaita fibroid kama sikosei, imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa wanawake, kwa watoto wa kike kuanzia miaka 18 mpaka 25 wengi wanapata hilo tatizo, inavyosemekana kwenye jamii yetu kwa sababu hakuna elimu ya kujua hasa chanzo cha hilo tatizo, wengine wanasema ukiwa na hilo tatizo wewe ulikuwa unajihusisha na ngono na watu wengi, wengine wanasema wewe ulitoa mimba sana kwenye usichana wako. Kwa hiyo, hata wale wanaougua huu ugonjwa wanajificha kwa kuogopa jamii inavyochukulia huo ugonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kupitia Wizara mtoe elimu kwa Watanzania wajue kwamba ugonjwa huu sababu zake ni hizi ili yule anayeugua ule ugonjwa awe huru kutoa na kusema kwamba mimi naugua hiki. Wengine tunaogopa, wale wasichana ambao hawajaolewa wanaogopa kusema hilo kwa sababu inaweza ikapelekea kukosa watoto kwenye ndoa, kwa hiyo anakaa kimya, anaolewa, anaendelea na matatizo yake. Ninaomba Wizara itoe elimu katika haya masuala, pia watoe elimu ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua wananchi, wafanyakazi wa Serikali, mashirika binafsi wanakuwa na mazingira magumu ya kufanya mazoezi, pia wanakuwa na mazingira magumu ya kuwa na diet nzuri. Niombe kupitia Wizara yako, tengenezeni vipeperushi, tengenezeni utaratibu wowote ambao utasaidia kutoa elimu kwa wafanyakazi hasa wa Serikali, katika masuala ya mazoezi na chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu afya ukila vizuri, ukifanya mazoezi magonjwa mengi yatakuwa mbali na wewe. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara itumie fursa hiyo, itoe elimu kwa wananchi, itoe elimu kwa viongozi, tuwe na tabia ya kufanya mazoezi, tuwe na tabia ya kujali afya katika chakula. Itasaidia kupunguza gharama nyingi ambazo tunazitumia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.