Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Ummy kwa kuwa na Wizara ambayo ni ya muhimu sana kwa maisha yetu na pia kwa afya zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee katika ule ukurasa wa 16, ibara ya 43 katika hotuba yake, hapa anazungumzia uzazi wa mpango. Ukizungumzia uzazi wa mpango watu wanakimbilia labda kufikiria ni vidonge, ni njiti, ni sindano, sio lazima, kuna uzazi wa mpango wa kuhesabu. Naomba watu waandaliwe katika kuhesabu namna ya kutenganisha watoto miaka mitatu, mitatu ili wawe na watoto ambao wana afya bora toka utotoni wawe watu wazima ambao wana afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalizungumza hili kwa sababu kasi ya kuongezeka Watanzania ni kubwa, ni kubwa zaidi ya maendeleo yetu. Tunapozungumzia watu na maendeleo watu ndiyo wanaotawala na kuendeleza maendeleo. Unakuta kwamba idadi ile inaongezeka kwa kasi kuliko maendeleo yanayopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo sahihi, ninaomba Wizara hii sasa iangalie jinsi gani itaelimisha watu ili tuende tukiongezeka taratibu na hapo nina maana, familia ikiwa na mtoto mmoja, wawili au sana wale waliotangulia kama sisi watatu, inatosha. Yale mambo ya familia kuwa na watoto sita, kumi yamepitwa na wakati. Najua maandiko yanasema zaeni mkaongezeke, lakini tukiongezeka holela pia tunakufa kiholela, ifikapo mwaka 2025 ongezeko hili litakuwa limepitwa kabisa na maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chonde chonde, nimuombe Mheshimiwa Ummy atakapopita mashuleni aende akatoe elimu na pia wale wanaohusika watoe elimu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda watoto na sasa hivi natarajia wajukuu, nawapenda sana wawe wengi, lakini siyo hovyo hovyo tu, nataka vitoto vyenye afya, vitoto vitakavyoweza kukidhi nchi yetu hapo tunapoenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nani hao ninaotarajia waelimishwe, ni ile ofisi ya maendeleo ya jamii. Ile ofisi imekaa choka mbaya, ina wasomi wazuri wana degree, wana masters, wengine wana postgraduate, wengine nilikutana nao mashuleni, lakini hawana vitendea kazi kabisa. Ofisi ya maendeleo ya jamii popote ilipo labda kwingine huko miji mikubwa lakini kule kwenye miji midogo midogo hata gari lenyewe la kuwafuata ile jamii wakatoe elimu halipo. Naomba sana Mheshimiwa Ummy, imezungumzwa jana na mimi nasisitiza, ofisi hiyo ipatiwe vitendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taasisi zetu, likiwemo Kanisa Katoliki, lina Vyuo vya Nursing lakini vyuo hivyo vimekosa walimu wa kutosha na hivyo naomba atakapokuwa anazungumza Mheshimiwa atauangalie ni jinsi gani atatoa pia walimu katika Chuo cha Nursing kule Kibosho, chuo ni kizuri katika Hospitali ya Kibosho, ni chuo ambacho najua nae ana ndoto ya kwenda kukiona, lakini viko vyuo vingi tu na hospitali nyingi tu ambazo hazina Madaktari wa kutosha ikiwemo Bambo kule Same na vituo vingi vya afya. Hata kile kituo cha afya ambacho alikijenga Lucy Lameck, Moshi Vijijini miaka hiyo kiko Shimbwe, kiko mbali sana hakuna hata usafiri wa kufika mjini, bado watu wanabebwa na chekecheke kuletwa mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kukumbushia Hospitali ya KCMC, hospitali hii sasa inataka kusaidiana na Ocean Road, hospitali hii sasa inakwenda kutoa huduma Kaskazini na Mikoa yote inayozunguka katika kutibu kansa. Hili ni eneo ambalo linahitaji gharama kubwa, wadau wamechangia vya kutosha, tunaiomba Serikali iweze kuangalia eneo hilo ili tupunguze ule msongamano pale Ocean Road ili huduma hii ya kansa ya mionzi na nyingineyo ya chemotherapy itolewe vizuri pale KCMC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kila mmoja wetu anapojifikiria anafikiria afya yake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.