Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niombe kuchangia kwa maandishi kama ifuatavyo:-
Mheshimwia Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja asilimia 100. Pili nitoe shukrani zangu za dhati kwa Wizara hii hususan Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu na Naibu wake kwa msaada mkubwa walioutoa kwenye vituo vya afya viwili; kituo cha Bulungu kupewa ambulance na kituo cha afya cha Nguruka nacho kilipatiwa ambulance. Tunaishukuru sana Wizara kwa msaada huo na tuiombe Wizara pale ambapo ambulance zinapatikana basi nitaomba kukiombea kituo cha afya cha Kalya ambacho kiko kilometa 270 kutoka Makao Makuu ya Halmashauri ya Lugufu. Wakina mama wajawazito wanapata taabu sana tena sana pindi wapatapo shida ya kujifungua kwa kupasuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe pia Wizara itupitishie ombi letu maalum la shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, tayari tumetenga eneo la hekari 30 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Uvinza ina jumla ya zahanati 33, kati ya vijiji 61 tunavyo vituo vya afya vitano katika ya kata 16 hivyo tuna upungufu wa vituo vya afya 11. Kwa sasa tunaendelea na ujenzi wa vituo vya kata za Kazura Mimba, Basanza pamoja na Mwakizega. Hivyo Mheshimiwa Waziri utaona ni jinsi gani hali ya afya bado haijaimarika ndani ya Wilaya ya Uvinza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea na ujenzi wa zahanati zifuatazo; katika kijiji cha Mazugwe ujenzi umekamilika. Kuna jitihada ya uanzishwaji kupitia Mfuko wa Jimbo na Halmashauri na kumalizia; zahanati za Lufubu, Ikubuvu, Kalilani, Msiezi, Kajije, Katenta, Malagarasi, Humule. Zahanati zote hizi tisa zinajengwa kwa nguvu ya Mfuko wa Jimbo na nguvu za wananchi. Tunaiomba Wizara kutuletea pesa kwa wakati ili tuweze kuunga mkono jitihada hizi za mimi Mbunge wao pamoja na nguvu za wananchi. Sambamba na jitihada za ujenzi wa zahanati tuiombe Serikali kutupa upendeleo kituo cha afya cha Nguruka kwani kinahudumia wakazi wapatao 80,000 ndani ya kata nne na kata moja ya jirani, kata ya Usinge Wilaya ya Kaliua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya vifaa tiba si nzuri kabisa. Kuna zahanati hazina vitanda wala magodoro, tunaiomba Wizara itusaidie vitanda, magodoro pamoja na vifaa tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi wa sekta ya afya kwa asilimia 70. Tunaiomba Wizara itakapoanza kuajiri basi Wilaya ya Uvinza iangaliwe kwa jicho la huruma, hali inatisha. Tuna mtumishi wa zahanati ya Mwakizega anaitwa Zainabu Hassan Salim, hivi karibuni nchi nzima ilishuhudia jinsi wananchi walivyoandamana kupinga nurse huyo kuhamishwa. Hebu Wizara iwe na utaratibu wa kutoa motisha kwa watumishi kama huyo; na kwa kuanzia si vibaya wakaanza na nurse Zainabu Hassan Salim wa zahanati ya Mwakizega.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia haya naomba kumpongeza tena Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri kwa Mheshimiwa Waziri Ummy kwenye maeneo kama ya Jimbo langu, si vibaya kuwa na ambulance za speed boat ili kuokoa vifo vya mama na mtoto kwenye Ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa mara nyingine niunge mkono hoja.