Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. JULIANA D. SHOZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwanza kuishukuru Serikali kwa kukubali ombi la kupandisha hadhi Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na hatimaye kuwa na hadhi ya Hospitali ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri machache. Hospitali hii inapandishwa hadhi ikiwa na changamoto nyingi. Idadi ya Manesi na Madaktari ni ndogo mno ukilinganisha na mahitaji yaliyopo, ukizingatia kuwa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi inahudumia Wilaya ya Momba, pia kutokana na kwamba Wilaya ya Momba mpaka sasa hakuna Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hiyo ya kuwepo kwa uhaba wa Madaktari inapelekea Madaktari kufanya kazi kwa muda wa ziada huku ulipwaji wa on call allowance wakicheleweshewa kupatiwa hivyo kupunguza ufanisi. Naomba Serikali katika ajira mpya zinazotarajiwa kutolewa, basi na Hospitali ya Wilaya ya Mbozi iliyopandishwa hadhi iongezewe Madaktari, kwani mpaka sasa kuna MD watano tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, changamoto ya dawa bado ni kubwa pamoja na jitihada za Serikali ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017 fedha za dawa zilizokuwa zimetengewa ni Sh. 143,937,133/= na zilizopelekwa mpaka Aprili, 2017 ni sh. 165,144,778/=. Hivyo Serikali ilivuka malengo, tunaishukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya dawa katika mwaka huu 2017/2018 ambapo tayari hospitali hii imepandishwa hadhi ni Sh. 173,938,158/=. Ongezeko hili ni dogo ukizingatia kuwa tayari hospitali hii imepandishwa hadhi na kuwa ya Mkoa. Hivyo, naomba bajeti ya dawa iongezwe pia MSD wahakikishe wanaleta dawa kulingana na bajeti ya fedha waliyopewa ili kupunguza tatizo la uhaba wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Hospitali ya Wilaya ya Mbozi imepewa hadhi ya Mkoa, lakini katika Bajeti ya mwaka huu sijaona mahali popote kuhusu mchakato wa ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Songwe. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha Bajeti yake, aniambie ni lini mchakato wa ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Songwe utakamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufahamu kuwa ni lini Wilaya ya Momba ambayo iko mpakani mwa Tanzania na Zambia itapatiwa Hospitali ya Wilaya, ukizingatia kuwa Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni yake Mjini Tunduma, 2015 aliahidi kutupatia majengo yaliyoachwa na Wakandarasi kuwa Hospitali ya Wilaya? Ni lini ahadi hiyo itatekelezwa ili wanawake na wananchi wa Wilaya ya Momba wapate haki yao ya kupata huduma hiyo muhimu ya kiafya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba kufahamu, ni lini Serikali itafikiria kuwa wagonjwa wa kisukari nao wapatiwe kadi bure kama ilivyo katika wagonjwa wa UKIMWI? Pia Serikali ijitahidi dawa za wagonjwa wa kisukari ziwe zinapatikana kwa wingi katika hospitali zetu ili kuwapunguzia mizigo wagonjwa wa kisukari kwa kununua katika maduka binafsi ambapo zinauzwa ghali.