Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na ardhi kwa kunijaalia uzima hatimaye nami nimepata fursa ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu katika Wizara hii ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, napenda nianze kuchangia kwenye Wizara hii kwa kuzungumzia Hospitali ya Mwananyamala. Hospitali yetu ya Mwananyamala imepandishwa hadhi na kuwa hospitali ya rufaa, lakini kwa masikitiko makubwa bado Serikali haitoi ruzuku ya kuiendesha hospitali hii, badala yake, mzigo wote wa uendeshaji umeachiwa Manispaa ya Kinondoni peke yake. Kwa ukubwa wa hospitali, Manispaa inatumia kiasi cha Shilingi milioni 69 kwa wiki jambo ambalo ni mzigo mzito kwa Manispaa ya Kinondoni yenye changamoto lukuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, namwomba Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini basi Serikali itaanza kutoa ruzuku ya uendeshaji wa Hospitali ya Mwananyamala kwa sababu sasa siyo Hospitali ya Manispaa ya Kinondoni tena? Aidha, kwa kuwa Hospitali ya Mwananyamala imepandishwa hadhi: Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Mabwepande hasa ukizingatia kuwa Hospitali ya Mwananyamala imezidiwa na mlundikano na wagonjwa, bila kusahau wakazi wa maeneo ya pembezoni, itakuwa ni mkombozi wao hasa kutokana na umbali na msongamano wa foleni za magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali yetu ya Mwananyamala ina changamoto na matatizo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida Hospitali ya Mwananyamala inahudumia wagonjwa 2,500 kwa siku, wagonjwa wa kawaida na wagonjwa 1,500 vijana walioathirika na madawa ya kulevya. Hivyo kufikisha jumla ya wagonjwa 4,000 kwa siku, jambo ambalo limepelekea upungufu wa Madaktari na Wauguzi, vifaa tiba na hata uhaba wa vitanda. Hivyo tunaiomba Serikali ituongezee Madaktari Bingwa 10 ili tuwe na 26; Madaktari wa kawaida (General Medical Officer) 20 ili tufikie 100 na Wauguzi 100 ili tuwe na Wauguzi 350.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba haya kwa kuwa hospitali hii inatuhudumia watu wote wa kutoka mikoa yote kwa sababu Kinondoni ndiyo Dar es Salaam na Dar es Salaam ndiyo Tanzania. Hivyo basi, Kinondoni ndiyo Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa zinazotumika kwenye hospitali zetu, zinatoka katika maghala ya MSD. Wakati mwingine MSD inakuwa haina dawa inayotakiwa kwa wakati muafaka, hata kupelekea maduka yetu na hospitali (za Serikali) kukosa dawa. Kwa bahati mbaya, hakuna ushindani katika jambo hili kwa maana ukikosa dawa MSD, basi unaweza kuzinunua kwa wengine kama Wakala wa Serikali, badala yake unatakiwa ufuate utaratibu wa kawaida wa Manunuzi ya Umma, jambo ambalo lina mlolongo mrefu wa kuchukua muda mwingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kwamba, kwa nini isiweke ushindani katika biashara hii ya dawa ili kurahisisha upatikanaji wa dawa kwa wakati? Mfano MSD iwepo na Wakala mwingine kama MSD. Aidha, kwa nini Serikali isiweke masharti nafuu ya kununua dawa bila ya kufuata mfumo wa manunuzi wa kawaida endapo MSD haina dawa inayotakiwa kwenye hospitali zetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Mwananyamala haina mashine ya CT-Scan na nyingine kwa ajili ya kupima baadhi ya wagonjwa. Wote tunajua hali za hospitali zetu na Serikali kwa ujumla. Aidha, hospitali ya Mwananyamala wanataka kumaliza jengo la Bima ya Afya na kununua mashine ya CT-Scan kwa mkopo kutoka Shirika la Afya kwa makubaliano ya kulipa kidogo kidogo kutokana na kukusanya malipo ya kuchangia gharama za matibabu hospitalini hapo: Je, Serikali iko tayari kuidhamini Hospitali ya Mwananyamala ili iweze kukopesheka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vifaa vya vipimo ni ghali sana; na vinahitajika sana hasa katika Hospitali yetu ya Kinondoni: Je, Serikali iko tayari sasa kutumia mfumo wa PPP (Public Private Partisanship) ili wafanyabiashara na wanaotaka kushirikiana na Taasisi zetu za Umma waruhusiwe kwa makubaliano ya kugawana faida inayopatikana kutokana na uchangiaji wa gharama za vipimo?

Mheshimiwa Spika, mwisho, naomba Serikali ya Awamu ya Tano ifanye ujasiri kama ilivyofanya kwa uchangiaji wa gharama za elimu, yaani kufuta uchangiaji wa gharama ya matibabu ya msingi iwe bure. Naomba hayo kwa sababu zifuatazo:-

(1) Idadi kubwa ya wagonjwa wetu katika afya ya msingi ni kutoka katika makundi maalum, yaani watoto wa chini ya miaka mitano, wazee wa zaidi ya miaka 60 na akinamama wajawazito. Hawa wote wametibiwa bure.

(2) Wagonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Kisukari wote wanatibiwa bure. Hili nalo lina idadi kubwa.

(3) Vijana walioathirika na madawa ya kulevya, nao wanatibiwa bure.

(4) Maskini wanapaswa kutibiwa bure kwani asilimia 70 ya Watanzania ni maskini, wanaishi chini ya dola moja na hasa Watanzania wa Vijijini, wanastahili kupata huduma ya afya bila malipo.

(5) Serikali inatoa dawa (fedha za dawa) kwa Vituo vya Afya nchi nzima, dawa ambazo zinaweza kuwatibia wagonjwa bure.

(6) Utaratibu wa Bima, wananchi wengi wakijiunga na Bima inatosha kugharamia wachache waliobaki kuweza kupata huduma bure.