Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Susanne Peter Maselle

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea kuhusu athari za upungufu mkubwa wa dawa na chanjo kwa akinamama na watoto. Itakumbukwa kuwa mwishoni mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwaka huu na sina uhakika kama tatizo hilo limekwisha hadi tunapozungumza hapa ndani sasa kwenye Mkutano wa Bajeti, nchi yetu ilikumbwa na ukosefu au upungufu mkubwa wa dawa pamoja na chanjo za magonjwa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ilikuwa mbaya kiasi cha Serikali kujichanganya katika kauli zake za kujitetea na kutaka kuonesha kuwa lilikuwa suala dogo lakini ukweli ni kwamba halikuwa suala dogo ndiyo maana Makamu wa Rais alisema kauli nyingine Wizara wakasema kauli nyingine. Wakati Waziri mhusika, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akisema kuwa hakuna tatizo la ukosefu wa dawa na kwamba hizo ni habari za kwenye mitandao tu, kesho yake bosi wake, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu akiwa pale Mwananyamala Hospitali akakiri kuwa nchi ina tatizo la upungufu mkubwa wa dawa na chanjo lakini eti halitakuwa la muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukiri kule, kauli ile ya Serikali ilikuwa ni ya ajabu na ilikuwa na ukakasi mkubwa sana masikioni mwa Watanzania ni kama vile walikuwa wanaambiwa wavumilie hali hiyo kwa sababu haitakuwa ya muda mrefu. Hivi kuna mahali mnaweza kucheza na maisha ya Watanzania kama kwenye afya na matibabu (uhai)? Hivi mnawezaje kusema ukosefu wa dawa halitakuwa tatizo la muda mrefu bali mfupi tu huku mnajua kuwa wakati huo kuna wagonjwa hospitalini wanahitaji dawa na wanakufa kwa kukosa dawa? Mnawezaje kusema kuwa tatizo hilo halitakuwa la muda mrefu wakati kuna akinamama wajawazito hospitalini wanasubiri matibabu na wengine wamejifungua wanahitaji matibabu na watoto wao wanahitaji chanjo? Huku ni kucheza na maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupata taarifa ya Serikali na wananchi wangu wa Mwanza wanataka kusikia Serikali ikisema hapa Bungeni, je, akina mama wangapi hususan wajawazito na wale waliojifungua na watoto waliozaliwa wameathirika na ukosefu huo wa dawa na chanjo hospitalini? Tumefikia hatua nchi inakosa dawa na vifaa tiba na chanjo za kifua kikuu, polio, surua, lubele, kichaa cha mbwa, manjano na magonjwa mengine hatari kwa afya ya mama na mtoto. Kwa hiyo, Watanzania na kipekee wananchi wa Mwanza wangependa kusikia Serikali ikiliambia Bunge hili athari ambazo Taifa hili limepata na litazipata miaka mingi ijayo kwa kitendo cha akinamama wajawazito kukosa dawa na chanjo, akinamama waliojifungua na watoto wao kukosa dawa na chanjo, nini athari zake kwa jamii yetu ambayo bado inapambana na utapiamlo, udumavu na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ujenzi wa vituo vitatu kila Halmashauri kuboresha huduma na uchunguzi na matibabu ya mapema ya saratani ya matiti na mlango wa kizazi kwa kina mama. Hivi karibuni wakati akizindua kampeni ya bure ya uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi kwa akinamama iliyofanyika mjini Mwanza, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu alisema kuwa Serikali ina mpango wa kujenga vituo vitatu kwa kila Halmashauri nchini kwa ajili ya kuboresha huduma na uchunguzi na matibabu ya mapema ya magonjwa hayo ili kuwanusuru akinamama. Ilisemwa kuwa zimetengwa shilingi bilioni saba na Serikali hii na Benki ya Dunia itasaidia shilingi bilioni tano katika kufanikisha suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimepitia taarifa ya bajeti ya Wizara hii kuangalia utekelezaji wa kauli hiyo ya Serikali sijaona mahali ambapo fedha hizo zimetengwa. Wananchi wa Halmashauri za Mwanza wanasubiri kwa hamu kuona utekelezaji huo ambao utaweza kuokoa karibu wanawake asilimia 60 walioko katika hatari ya vifo vinavyosababishwa na magonjwa hayo huku wakiacha nyuma watoto wanaohitaji malezi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Serikali ituambie hapa imefikia wapi katika kusogeza huduma za magonjwa hayo katika hospitali za Bugando na KCMC kama alivyosema Makamu wa Rais ili kupunguza mahitaji ambayo hospitali ya Ocean Road inakabiliana nayo kwa sasa. Pia naomba kujua maendeleo ya kampeni hiyo ya bure hususan kwa Mkoa wa Mwanza ambayo ingepaswa kwenda sambamba na utoaji wa elimu au kujikinga au kuzuia magonjwa hayo kwa akinamama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kampeni ya malaria na ugawaji wa taulo za usafi wa mwili kwa mabinti kwenye shule zetu. Hivi karibuni taarifa kutokana na tafiti zilizofanyika zilionesha kuwa wasichana walioko shule au walio na umri mdogo wanapata athari kubwa sana kutokana na ugumu wa kupata mahitaji ya taulo za usafi wanapokuwa katika mzunguko wao wa kila mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari hizo ni mimba za utotoni kwa sababu ya kudanganywa ili wapate fedha za kununua taulo; wanashindwa kuhudhuria shuleni na kukosa masomo kwa siku tano hadi saba kila mwezi; kupunguza uwezo wao wa kufaulu kwa kukosa masomo na kuwa katika uwezekano wa kupatwa na magonjwa mbalimbali kutokana na kutumia vifaa visivyo sahihi na visivyo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kumekuwepo na kampeni kubwa dhidi ya malaria ambayo nasikia imefika hadi kwetu Buchosa kwa ajili ya kupulizia dawa ndani na kwenye kuta za nyumba, ni wakati muafaka sasa Serikali ikalivalia njuga na kulipatia uzito mkubwa suala la kuwasaidia hawa watoto na mabinti zetu walioko shuleni wapate taulo hizo ili wabakie shuleni wasome, waepuke mimba za utotoni na magonjwa hatarishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara walione hili na walichukue kwa uzito mkubwa sana. Inaweza hata kwa kuanzia kushirikiana na watu au mashirika ambayo tayari yameanza kampeni hii kama walivyokuwa wakifanya watu wa East Africa Television na East Africa Radio ambao walifanya kampeni kubwa kuhamasisha watu kusaidia mabinti hawa walioko shuleni wanaoteseka kwa sababu ya kukosa taulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, matibabu ya bure kwa wazee, kambi ya wazee wa Bukumbi na kambi ya walemavu Misungwi. Wazee wangu wa Mwanza, maeneo ya Buchosa, Sengerema, Ilemela, Nyamagana, Magu, Sumve, Ukerewe, Kwimba na Misungwi bado wanasubiri lini Serikali itatekeleza kwa dhati huu mpango badala ya kuwa kwenye makaratasi na maneno ya hapa Bungeni na kwenye mikutano au semina au warsha na makongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati lilifanyika zoezi la kutoa vitambulisho kwa wazee wanaotakiwa kutibiwa bure, naomba Serikali kupitia Bunge lako iwaambie Watanzania zoezi hili limefikia wapi na wazee wangapi wamepata hivyo vitambulisho hususan kwa Mkoa wetu wa Mwanza ambako wazee wetu waliotumikia Taifa letu wakiwa wakulima, wafugaji, wafanyakazi Serikalini sasa wamestaafu wanahangaika sana kupata matibabu. Tunaomba mtuambie kama mtaweza kuitekeleza kwa vitendo sera hiyo ambayo tunajua haikuwa ya kwenu. Kama imewashinda tuwaambie wazee wetu na watu wengine ambao tu wazee watarajiwa kuwa hilo litawezekana tu pale ambapo Serikali ya UKAWA itaingia madarakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Mwanza wanapata shaka sana iwapo Serikali itaweza kutekeleza kwa vitendo sera hiyo wanapoangalia kambi ya wazee wasiojiweza ya Kigongo, pale Misungwi namna ambavyo wazee wale wametelekezwa na Serikali, hawana dawa, wanasumbuliwa na magonjwa na hawawezi kutibiwa, wanapangiwa bajeti isiyotosheleza kwa chakula wala matibabu. Hali hiyo mbaya ya kituo cha wazee cha Misungwi ambayo hata Mama Janeth Magufuli aliishuhudia mwenyewe haijaishia hapo pekee, kuna kilio kikubwa pale shule maalum ya walemavu wa ngozi ya Mitindo iliyoko Misungwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii ambayo inashirikiana na Wizara zingine kuhakikisha watoto wale wanapata stahili za kulinda afya zao. Vinginevyo iko siku tutaona machozi mengine humu Bungeni kuwalilia watoto wale kama ambavyo Waziri Mkuu aliyepita alitoa machozi kwa ajili ya albino.