Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yale yote niliyochangia hapo awali, naomba kutumia fursa hii kuchangia yale niliyoshindwa kwa sababu ya muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza ina changamoto kubwa ya mimba za utotoni na uzazi usio na mpangilio. Jambo hili limezua uwepo wa wategemezi wengi kuliko wanaotegemewa. Hivyo basi, nipende kuiomba Serikali kuliangalia suala hili kwa ukaribu
zaidi na kuweza kuweka mkakati wa campaign ya masuala ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana AMREF kwa kudhamini theatre za vituo vya afya vya Kata za Muriti na Kagunguli ndani ya Wilaya ya Ukerewe. Tayari miundombinu imekamilika bado tu ukamilishaji wa vifaa husika. Wasiwasi wangu upo kwenye Kituo cha Afya cha Kagunguli ambacho bado hakijapata huduma ya maji salama na katika ziara ya Makamu wa Rais Wilayani Ukerewe, Waziri wa Maji aliagizwa kusimamia suala hilo. Kweli mradi ulianza kwa kasi kubwa na cha kushangaza mradi huo umesimama sasa kwa takribani miezi miwili. Naomba Waziri mwenye dhamana ya maji asikie kilio hiki na atuondoe katika hali ya sintofahamu tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto niliyochangia hapo awali ya ukosefu wa hospitali ya Wilaya ya Ilemela, lipo tatizo lingine la Wilaya ya Ilemela kukosa vituo vya afya vya kutosha. Jimbo la Ilemela lina kata 19 ila cha ajabu ni kwamba lina zahanati tatu tu ambazo hata miundombinu yake haijakamilika. Kwa mfano, Kituo cha Afya cha Buzuruga hakina wodi ya wanaume wakati kinahudumia maelfu ya wananchi kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Ilemela. Napenda kuiomba Serikali kukiangalia Kituo hiki cha Afya cha Buzuruga kwa jicho la pekee na kama nilivyosema kuwa hakuna hospitali ya wilaya na vituo vya afya ni vitatu tu wilaya nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Kwimba, Jimbo la Kwimba, kipo Kituo cha Afya cha Mwamashimba ambacho hakina theatre na kusababisha wananchi kukosa upasuaji na wengine wamekufa kwa kukosa huduma ya upasuaji pale kunapotokea dharura. Naiomba Serikali kufanya maarifa ili kituo hicho cha afya kiweze kupata theatre ili kunusuru maisha hasa ya akina mama wajawazito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Kwimba ipo Zahanati ya Buyogo ambayo kwa kweli ni ya mfano. Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waganga na Wauguzi wa zahanati hii kwa kazi nzuri. Wamekuwa wakihudumia wananchi wengi kuliko hata hospitali ya wilaya na huduma zao ni nzuri. Mimi leo naungana na Mbunge wa Kwimba kuomba Serikali kuipandisha hadhi zahanati hii ya Buyogo kuwa Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, naomba Wizara itutatulie matatizo ya ukosefu wa maduka ya MSD katika hospitali za wilaya za Mkoa wa Mwanza na tatizo la ukosefu wa Waganga na Wauguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante.