Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Sixtus Raphael Mapunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Naomba nichangie kwenye maeneo mawili, eneo la kwanza nitachangia eneo la michezo na eneo la pili nitachangia kwenye eneo la utamaduni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kuu inayoikabili Wizara hii katika kukuza sekta ya michezo, sekta ya habari, sanaa na Utamaduni nchini ni changamoto fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 161 cha Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 kinasema yafuatayo:-

“Katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani hii, Serikali itaimarisha sekta ya michezo nchini kwa kuifanya sekta ya michezo kutoa fursa ya ajira hususan kwa vijana kwa kupanua wigo wa vyanzo endelevu vya fedha za uendeshaji na ugharimishaji wa maeneo ya michezo hapa nchini kwa kuanzisha bahati nasibu ya michezo.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo ilikuwa commitment ambayo tuliitarajia sasa, baada ya miaka miwili ya kuwa madarakani Wizara ingekuja na mkakati wa kuanzisha hicho chombo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri ufuatao; badala ya Serikali kwenda kuanzisha chombo kingine cha bahati nasibu, ni vyema sasa ingetumika hii Bodi ya Bahati Nasibu ya sasa, isipokuwa iboreshwe kidogo. Sasa inafanya kazi zake ikiwa chini ya Wizara ya Fedha na ukiangalia kwa ujumla wake, Wizara ya Fedha ina majukumu mengi, haiwezi ikafanya kazi vizuri na ikaifanya hii Bodi ya Bahati Nasibu ikaleta mapato yale tunayoyatarajia ukilinganisha na nchi nyingine waliyowahi kufanya mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara ya Fedha na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, mkae mkubaliane ihame huku ije kwenye Wizara ya Michezo. Nasema hivyo kwa sababu nne zifuatazo:-

Kwanza, msingi mkuu wa kuhamisha majukumu kuyapeleka kwenye Wizara ya Habari ulishaainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi; la pili, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ina miundombinu inayojitosheleza ya kuifanya ikafanya kazi vizuri kuliko ikikaa kwenye Wizara ya Fedha. Kwa sababu ili bahati nasibu ilete mapato mazuri inahitaji hamasa. Wizara ya Fedha haina room ya hamasa, ila kwenye michezo kuna hamasa. Tukiiweka hii italeta picha nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya tatu, wanaocheza hii michezo wana uhusiano wa moja kwa moja na michezo, kwa hiyo, ukiiweka kule kwenye Wizara ya Fedha inakuwa ime-hang, umeweka kitu kama mtoto mkiwa hana baba wala mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne na la mwisho, the best practice kutoka nchi nyingine, kuna nchi zimefanikiwa kwa kuweka hii kwenye Wizara ya Michezo na wakapata pesa nyingi za kuendesha Wizara. Brazil wanafanya hivyo, Australia wanafanya hivyo, Uingereza wanafanya hivyo na hata majirani zetu Kenya wanafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiombe Serikali isipate kigugumizi, isianzishe Bodi nyingine ya Bahati Nasibu, isipokuwa hii iliopo iondoke Wizara ya Fedha ikasimamiwe chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka kulichangia ni kuhusu utamaduni. Taifa lolote duniani linatambulika kutokana na utamaduni wake na hata kama zile nchi zilizokuwa na utamaduni wa pamoja unaoeleweka kama nchi yetu Tanzania tukiongea kiswahili tunaeleweka kama Watanzania, nchi nyingine zina alama nyingine zinazotambulisha mataifa yao. Nchi yetu ukiondoa lugha ya kiswahili, ina mambo mengine ambayo yanalitambulisha Taifa letu.

Jambo la kwanza, ni Bendera ya Taifa; jambo la pili, Wimbo wa Taifa; jambo la tatu, Mwenge wa Uhuru na jambo la nne ni Ngao ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf alikwenda mbali sana katika kuchangia, alifika hatua ya kusema Mwenge wa Uhuru uondolewe upelekwe kwenye makumbusho. Naomba nichukue fursa hii kuyasema yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzito wa Mwenge wa Uhuru ni ule ule, sawa sawa na Wimbo wa Taifa; uzito wa Mwenge wa Uhuru ni ule ule sawa sawa na Ngao ya Taifa, uzito wa Mwenge wa Uhuru ni ule ule sawa sawa na wimbo wa Taifa. Kwa nini nasema haya? Hayo mambo yote ni package moja.

T A A R I F A...
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba unilindie muda wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa lolote duniani na mifumo yoyote ya sheria duniani inatokana na mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo sheria inayotungwa inaweza ikatokana na the best practice. Jambo hili limefanyika katika jamii kwa muda gani? Limekubalika katika jamii kwa muda gani? Hapo ndipo linapopelekea kwenye kutunga sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie kitu kimoja, mila na desturi za Taifa lolote lile zinatokana na historia yake. Huwezi ukauondoa Mwenge wa Uhuru kwenye historia ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe kidogo, mwaka 1961 tulipopata uhuru tulikuwa na ajenda mahususi, tulisema mambo yafuatayo: “Sisi tunataka kuuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimajaro umulike hata nje ya mipaka yetu ulete tumaini pale ambapo hapana matumaini, ulete upendo pale ambapo pana chuki na ulete heshima pale ambapo pana dharau.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu mniambie haya mambo yote mazuri, hivi kweli yapotee hewani! Huo ndiyo msingi wa historia ya utu wa Watanzania. Kwa hoja hiyo ninashangaa, kwa nini Mwenge wa Uhuru haukuwahi kutungiwa sheria! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo lilinikwaza jana, kuuita Mwenge wa Uhuru ni ibada. Kila jambo tukilifanyia ibada hatutafanya hata moja. Mwaka 2016 nilikuwa Jimboni, mwananchi mmoja akaniambia, Mheshimiwa Mbunge kwa nini mkiingia Bungeni mnafanya ibada? Nikamuuliza ibada gani? Akasema, ninyi mkifika si kwanza siwa mnaliinamia, hamfanyi kitu bila siwa na mkiondoka kama Bunge kwenda kwenye Kamati, siwa mnaifunika ndani, mkirudi wote mnasimama mnafanya ibada ya siwa. Jamani, wote tungesema hizi ni imani, tungefika? Kitu kimoja ninachotaka kusema, nchi yoyote unaitambua kwa vitu vingi; alama ni moja ya ishara ya kuitambua nchi. Ninamshangaa sana ndugu yangu, Mheshimiwa Tundu Lissu, amesema Ngao ya Taifa imetungiwa sheria, lakini hakujipa muda wa kutosha kuangalia Ngao ya Taifa imeundwa na nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambieni, kwenye Ngao ya Taifa ina mambo yafuatayo, kuna bibi na bwana, kuna pembe za ndovu mbili zikichunguliana, kuna mwenge wa uhuru umekaa katikati, chini yake kuna bendera, sasa sioni kipya hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo tunaweza tukafika sehemu tukaelewana, jambo ambalo tunaweza tuka-discuss tukaelewana kuhusu mwenge wa uhuru ni modality ya kuukimbiza mwenge wa uhuru. Hili liko open to discussion. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuupeleka mwenge wa uhuru kwenye makumbusho, ni kuipeleka historia ya Taifa la Tanzania kwenye makumbusho. Haya mambo anayeweza kuyafanya ni yule ambaye sio mzalendo wa Taifa hili, ni yule ambaye hajui mambo matatu yanayoongelewa katika moto wa mbio za Mwenge ndiyo unayotengeneza utu wetu? Nani anapenda dharau humu ndani? Nani anapenda chuki humu ndani na nani ambaye hapendi heshima humu ndani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaombe ndugu zangu, mwenge wa uhuru ni jambo jema sana, ni jambo ambalo inabidi tulienzi, tuliheshimu, tukiudharau mwenge tutapata shida. Mimi najua kwa nini wanadharau mwenge. Siku zote historia ni nzuri hata kama aliyeandika ile historia… (Makofi/ Vigelegele)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.