Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia. Wakati naongea, naomba ni-declare kwamba mimi pia ni msanii wa nyimbo za injili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu mwaka 2005 nilichaguliwa kuingia ndani ya Bunge hili na nilipoingia ndani ya Bunge hili, hapakuwa panazungumzwa habari za sanaa ndani ya nyumba hii, lakini mpaka sasa hivi ni hatua kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka wakati huo kabla sijawa Mbunge tulikuwa tumeanzisha uanaharakati kwa ajili ya kutetea haki za wasanii. Kwa hiyo, nilipoingia kwa kweli niliendeleza na ndiyo maana mpaka leo hii tunamshukuru Mheshimiwa Rais ambaye ameweza kugundua umuhimu na kuingiza sanaa kwamba ni mojawapo ya Wizara maalum kabisa. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe pamoja na dada yangu kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya na Katibu Mkuu. Tumeiona kwa sababu sisi tunaelewa tulipotoka mpaka hapa tulipo. Kwa hiyo, nawatia moyo muendelee kufanya kazi pamoja na kwamba bajeti yenu kwa kweli hairidhishi, lakini ninaamini kwa utendaji wenu mzuri hakika mta-perform vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi Singida. Naomba nichukue nafasi hii kupongeza sana timu yangu ya Singida United ambayo imeweza ku-perform vizuri na kuweza kuingia ligi kuu. Nampongeza sana Rais wa Singida United, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Mwenyekiti wa Singida United, Ndugu yetu Yusuph Mwandami na viongozi wote wa Singida United walioisaidia ikafikia hapa ilipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe tahadhari na tangazo moja kubwa sana kwamba Dar es Salaam tunaomba mjiandae, nyang’anyaneni kombe hili, yoyote atakayepata tutunzieni. Singida sisi tunaenda kubaki na kombe hili, hamtaliona tena huko. Natoa salamu hizo.

Yah, lazima libaki Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nishukuru sana TFF. Namshukuru Rais wa TFF, Ndugu Malinzi, Katibu Ndugu Mwesiga na Ndugu Salum Madadi ambao wamekuwa karibu sana na sisi kutusaidia na kutuelekeza ni namna gani tunajenga uwanja wetu uweze ku-qualify ili mechi iweze kucheza Singida. Na sisi Chama cha Mapinduzi tumejipanga, naipongeza Kamati yangu ya Siasa ya Mkoa ya Chama ambayo wamesimama kidete kuhakikisha uwanja ule unakamilika. Nawapongeza sana, big up sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wadau tushirikiane kwa sababu Kanda ya Kati hakuna timu nyingine ya Ligi kuu zaidi ya Singida United, tuisaidie ili kombe liendelee kubaki Makao Makuu ambayo ni Kanda ya Kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, pia nisisahau kumpongeza Alphonce Simbu, kijana ambaye anatoka Singida, ametupa heshima kubwa sana kwa kazi nzuri aliyoifanya na kupata medali ya dhahabu na alipoenda London Marathon ameshika nafasi ya tano, tunamtia moyo, ame-improve, tunaamini mwakani atashika nafasi nzuri na tumtakie heri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze, nimesha-declare interest, nataka niseme kuhusu jambo moja ambalo lipo mitaani sasa hivi, hasa kwenye tasnia ya filamu. Vijana wapo mitaani hawana kazi, filamu zao ambazo wamezicheza zimebaki kwenye makabati, siyo kwamba hazina ubora, lakini kuna tatizo kubwa sana ambalo nashukuru sana Wizara ilishaanza kushughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana muelewe wazi kwamba taratibu zinazotumika siyo sahihi kwa sababu ushindani umekuwa ni mkubwa. Kazi za nje zinazoingia ndani, tena zinatafsiriwa kiswahili na kazi hizi za nje zikija zikitafsiriwa kiswahili, watu wa nchi za Magharibi wanakuja kununua kwa sababu wanazungumza kiswahili. Kwa hiyo, kazi zetu sisi hazipati soko kwa sababu ya bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za ndani kutengeneza filamu moja inatumia zaidi ya shilingi milioni 18. Kuanza tu kuandika andiko kwenda kwenye Bodi ya Filamu ni shilingi 500,000, urudi COSOTA, sijui ikaguliwe, ukiigiza, maudhui, maadili, yote ni hela mpaka COSOTA, uende TRA ni hela. Process hii ni ndefu na ni hela nyingi, kwa hiyo, msanii huyu auze shilingi ngapi? Ndiyo maana unakuta soko za filamu hizi zinakuwa hazinunuliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, hizi kazi za nje wala hakuna haja ya kuwafungia watu. Wekeni utaratibu na wafuate taratibu wanazofuata hawa wa kazi za ndani. Wakishafuata, hakuna tatizo kwa sababu bei itakuwa ni moja na kazi zitanunuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie, Tanzania ni nchi ya pili kwa ubora wa kazi za filamu ikitanguliwa na Ghana, lakini kwa sababu ya gharama za uzalishaji, ndiyo maana unakuta kazi hizi hazipati wateja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumze suala la Sera ya Filamu. Sera ya Filamu kama tutaipitisha hapa itakwenda kurekebisha sheria na taratibu ambazo zitaweza kuwabana hata wale maharamia. Kwa sababu Sheria ya COSOTA sasa hivi ilivyo, mtu akikutwa na kazi haramu za shilingi bilioni moja, akipelekwa Mahakamani ni shilingi milioni tano, lakini kazi ni shilingi bilioni moja au jela miaka mitano. Obviously yule mtu yupo tayari kulipa gharama hizo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe namwamini sana kaka yangu, atakwenda kushughulikia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nashauri, kwa sababu tuna chuo chetu cha Bagamoyo lakini hatuna Chuo cha Filamu, hebu naomba hilo, bado vijana hawa hawawezi kukopesheka. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, wasanii hawa wapo takriban milioni tisa Tanzania. Afanye research ataona, ni ajira na ni kiwanda kikubwa sana kama tutawawekea mazingira mazuri ambayo Mheshimiwa Rais wetu amekusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Sera ya Filamu, Mheshimiwa Waziri aende BASATA akashirikiane nao wampeleke kwenye yale mashirikisho manne ambapo kuna Shirikisho la Filamu, Shirikisho la Kazi za Ufundi, Shirikisho la Muziki na Shirikisho la Sanaa za Jukwaani. Akienda kule kuna vyama, ndiko wasanii walipo ili wawawezeshe BASATA waweze kufanya kazi na mashirikisho haya kuwasaidia Watanzania wote. Maana tukisema kazi za ufundi; wapo vinyago, wapo akina tingatinga, wapo wachoraji, kuna waandishi na watu wengine, ni kiwanda kikubwa sana! Naomba sana Mheshimiwa Waziri aende BASATA akashirikiane nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba tu nimalizie kwa kusema kwamba, hebu niwapongeze wale wadau wote ambao wamekuwa wakiwasaidia wasanii. Nianze na Ruge Clouds, Msama; wote hawa ndio wamehangaika na wasanii kufika hapa. Nakumbuka wakati tunaanza sanaa, Ruge alianza na Clouds FM kwenye chumba kimoja; lakini wasanii tulikuwa tunaenda kujibanza pale. Ameendelea kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Serikali iwe inawaangalia watu hawa ili muwasaidie waendelee kuwasaidia wasanii. Mwangalie Msama anavyohangaika kukamata kazi za wasanii, anaishia tu kuwapeleka Polisi, hakuna sheria, hakuna nini. Kwa hiyo, naomba washirikiane na wadau hawa ili waweze kuwasaidia wasanii. Kwa mfano,...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.