Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi niungane na wenzangu katika kuwapongeza Mawaziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwangu la kwanza, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Michezo, tunacho kiwanda cha kuzalisha wataalam wa michezo nchini, Chuo cha Michezo Malya. Wataalam hao ni walimu wanaotoka kwenye shule za misingi wanakwenda kujifunza namna ya kufundisha michezo mbalimbali kwenye shule zetu za misingi na sekondari, ndiyo maana nakiita ni kiwanda. Ili upate wachezaji wazuri wa fani zote, huwezi ukaanza na vijana wa sekondari wala vyuo, lazima uanze na shule za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, chuo hiki malengo yake nafikiri anayafahamu na bahati nzuri juzi alifika akaona miundombinu yake, jinsi tulivyo-invest siku zote.

Sasa ni vizuri zaidi pale walipoishia wenzake hebu na yeye akanyage sasa huo moto ile accelerator asitoe mguu wake ili ipae zaidi, chuo kile ikiwezekana kiondoke na kutoa certificate, diploma kiende kwenye degree ya michezo. Tukifanya hivyo Mheshimiwa Waziri chuo kile tutakuwa tumekisaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimuombe Katibu Mkuu, tuna upungufu kadhaa hasa upande wa maji, kipo kisima kikubwa tulitumia pesa zaidi ya shilingi milioni 230 kwa ajili ya kujenga kisima cha maji kwa ajili ya Malya ambayo mnufaika mmoja wapo ni Chuo cha Michezo Malya, tumepungukiwa mambo madogo madogo. Bahati nzuri kama sikosei Mkuu wa Chuo cha Malya yupo, nafikiri anaweza akamweleza Katibu Mkuu, hili tatizo la upungufu wa maji linaweza likaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niruhusu kwa sababu vinginevyo sitajitendea haki nimpongeze sana Naibu Spika kwa kuweza kuchukua baadhi ya wachezaji wa michezo ya ngoma za asili kwenda kupata mafunzo ya ziada kwenye chuo chetu cha Bagamoyo. Ni chuo kizuri na sisi Waheshimiwa Wabunge nafikiri si vibaya tukaiga utaratibu huo mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Baraza la Michezo la Taifa. Mimi sijui Bwana Malinzi ni Malinzi yupi sasa, Baraza hili ndilo linalosimamia michezo yote. Sijaona wala kusikia Baraza limekwenda limekemea eneo fulani penye mgogoro, lipo lipo tu. Nilisema kipindi kile na leo nasema tena kwa sababu Baraza hili ndiyo mlezi wa vyama hivi vya michezo. Sina uhakika kama Baraza hili linafanya kazi yake ile ambayo tuliitunga humu Bungeni. Mimi nasema kama upo upungufu kwenye utaratibu wetu hebu tuje hapa tubadilishe. Kwa sababu haiwezekani leo hii Baraza kila mnapoenda iwe kwenye vilabu, iwe kwenye riadha, kuna migogoro. Sasa kazi ya Baraza hili ni nini? Naomba Baraza hili hebu lijipange vizuri kwa sababu michezo hii ni mingi kama walivyosema wenzangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Uwanja wetu wa Taifa tubadilike sasa tuache kuutumia kwa ajili ya mechi za Simba na Yanga na hizi mechi la ligi. Uwanja ule tunaweza tukaugeuza ukawa ni uwanja wa kibiashara na ukawa ni uwanja wa kuleta watalii kutoka nje hasa michezo ya kimataifa. Nilisikia juzi juzi hapa Mheshimiwa Waziri sijui timu gani inakuja utasema, tuna uwanja mzuri, tuna mbuga za

wanyama, wachezaji hawa wa kigeni wakija kucheza michezo ya kimataifa Tanzania kwenye uwanja wetu wa Taifa baada au kabla ya michezo ile wanatembelea mbuga zetu za wanyama, tunapata watalii kupitia michezo na kupitia uwanja ule, ni jambo linalowezekana. Naomba Mheshimiwa Waziri akae na Katibu Mkuu wake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ili kusudi uwanja ule unufaishe pande zote mbili, kwenye upande wa michezo na kwa upande wa utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije upande wa timu zetu hasa hizi timu kubwa za Simba na Yanga lakini kuna mtu mmoja amechangia hapa anauliza kuhusu waamuzi. Mimi nishauri, tuwe wanasiasa au tuwe watu gani, tukitaka mpira wetu uendelee kwa timu zetu hizi Simba, Yanga na timu zingine sisi wanasiasa hebu tukae pembeni kidogo. Kwa sababu kama sisi wanasiasa tutaingia ndani tukajifanya sisi ndiyo waamuzi namba 12 au 13 kinachofuata ni kuharibu ile test ya mpira wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunavurunda humu ndani kwa kutumia urafiki na wanasiasa tukienda huko nje hatufanikiwi. Watani zangu Yanga ndani humu wanacheza vizuri sana, lakini wakienda huko nje na bendera yetu ya Taifa wanarudi na rundo la magoli. (Makofi)

Sasa tujiulize hivi kwa nini humu wanaweza na kwa nini nje hawawezi? Ni kwa sababu ya mambo yetu ya siasa. Tukiacha siasa tukafanya mpira uwe mpira, wakacheza mpira bila kupendelewa na watu fulani fulani whether ni viongozi wa kisiasa au linesman, nina uhakika hata huku nje watashinda kwa sababu kule nje hamna kubebwa, mbeleko kule nje hakuna, ziko hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Baraza la Michezo tukiendelea kwa utaratibu huu wa kuzibeba timu zetu, tukienda nje ni aibu, tutaendelea kuwa wasindikizaji. Nirudie Baraza la Michezo hebu fanyeni kazi yenu. Hivi sisi kweli maandalizi yote hayo kwa timu zetu, tuna wachezaji wazuri lakini tukitoka hapa tukienda nje tunafungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata timu yetu hii ya vijana nina uhakika kama haitaingiliwa na wanasiasa kwenda kuwa-lobby wale wachezaji wazuri waliomo mle ndani, maana yake tutaanza wewe ni wa kwangu, wewe ni kwangu tutawapa vichwa watashindwa kufanya kazi yao ya kuchezea mpira uwanjani. Tuwaache wao na makocha wao na wataalam wao ili kusudi wacheze mpira, watuletee sifa Tanzania, kwamba Tanzania sasa sio Tanzania kama ile ya zamani. Tukianza sasa sisi wanasiasa kuingia ndani nina uhakika timu ile itarudia njiani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, wewe najua ni mpenzi mzuri wa mpira hasa wa miguu na ni kiongozi na humu tuko wapenzi wengi wa mpira wa miguu na michezo mingine, niwashauri sana Wabunge wenzangu pamoja na ushabiki wetu, pamoja na Mzee Mkuchika pale na Yanga yake tuache ushabiki usiokuwa na utaratibu kwa manufaa ya timu zetu. Nina uhakika hata timu ya sasa inayokuja kwenye ligi kuu ya Singida United mtakuja kuniambia na kukumbuka maneno yangu kwa sababu wanasiasa wanaingia kutafuta umaarufu, pesa zikishawaishia wanakaa pembeni ile timu inabaki peke yake. (Makofi)

Wameshaanza kuingia wanasiasa kujipendekeza. Muda utakapofika wakikaa pembeni ile timu itabaki peke yake. Naomba Singida United ibaki kama ilivyoanzishwa kwa mapenzi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.