Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia machache katika mjadala unaoendelea.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka salama na kunipa nguvu za kusimama mahali hapa asubuhi ya leo ili niweze kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, pia naungana na Watanzania wengine wote kutoa pole kwa familia za marehemu waliopoteza maisha mwishoni mwa juma hili na tumwombe Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, lakini atupe nguvu na subira sisi wafiwa katika kipindi hiki kigumu.

Mheshimiwa Spika, nianze na TBC. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumza mambo mengi ya kuona namna gani anaweza kuiboresha TBC, lakini kwa maana ya kupanua usikivu wake na muonekano wake na kuiboresha yenyewe mambo ambayo yanahitaji sana fedha. TBC hii haihiitaji tu maboresho kwenye mambo ambayo yanatumia fedha inahitaji pia maboresho ya weledi na kujituma kwa wafanyakazi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TBC imekuwa kituko na inashindwa kubeba hasa ile nafasi yake kama chombo na chanzo cha kutoa habari kwa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, habari ambazo zinarushwa na TBC kwanza zinakosa mvuto, watangazaji wenyewe ile kuchangamka tu, kwa sababu kuchangamka hakuhitaji Wizara ikutengee fedha ili uchangamke ukiwa studio. Mtangazaji anafanya kazi kama kalazimishwa, matokeo yake hata wanapozungumza habari za burudani ambazo ni za kufurahisha bado zinaonekana kama habari za msiba ambazo zinatia huzuni.

Mheshimiwa Spika, haya ni mambo ya kiweledi ambayo yanahitaji tu usimamizi mzuri na wafanyakazi hawa waambiwe kwamba TBC ndiyo chombo kinachotegemewa na wananchi. Kama hakuna mvuto wa kuingalia television hiyo, hivi mtu ata-tune vipi kwenye television ambayo haimfurahishi hata kwenye mambo yale ya kawaida? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukweli wa habari ambazo zinatangazwa na TBC, hivi juzi juzi hapa tulishuhudia kabisa habari ya kupikwa kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump amesifia na kupongeza kazi zinazofanywa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Ni jambo zuri, lakini ukweli wenyewe wa habari ile ilikuwa ni ya kupikwa haikuwa ya kweli kutoka Marekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sasa unajiuliza, hivi jambo dogo kama hili TBC wanashindwa ku-cross check, kuthibitisha kwamba habari hiyo ni ya kweli! Tuna Ubalozi wa Marekani kutoka Bamaga kwenye Ofisi za TBC kwenda Ubalozi wa Marekani hazifiki hata kilometa tano. Hivi TBC ilishindwa kitu gani kwenda Ubalozi wa Marekani kuthibitisha kama kweli kuna habari hiyo ili watulishe habari ambazo ni za kweli na uhakika badala ya kutulisha habari za kupikwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kabisa na wewe habari za kukanushwa kwa taarifa ile ulizipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya sasa ndiyo yanawafanya Watanzania waache kuitegemea TBC kama chanzo cha taarifa na badala yake sasa tumejikita kwa ITV na Azam TV kwamba sasa zimekuwa kama television za Taifa badala ya TBC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vizuri tu wakajitazama wenyewe ili waaminike na watu wengi wa- tune kwenye TBC, ni lazima wabadilishe namna ambavyo wenyewe wanafanya kazi zao za kila siku katika kituo hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni la ving’amuzi; wakati tunaimba kwamba tunabadilika kutoka analogue kwenda digital, zilikuja concerns kwamba watu watakaposhindwa kulipia ving’amuzi vyao watakosa kuangalia television na Serikali ilituaminisha kwamba kila muuza ving’amuzi atalazimika kuhakikisha kuna local channels angalau tano ziwe zinaonekana hata pale ambapo king’amuzi kitakuwa kimemaliza bundle lake. Kitu hiki sasa hivi hakipo.

Mheshimiwa Spika, usilipolipia king’amuzi huna channel utakayoiona na hata vile ving’amuzi vichache ambavyo wanaweka channel, basi hazizidi mbili. Ving’amuzi vingi usipokuwa na bundle hakuna channel yoyote utakayokuwa unaiona.

Mheshimiwa Spika, sasa Watanzania wanakosa fursa ya kuangalia television kwa sababu tu tumeingia kwenye digital. Sasa hili jambo ni la kisheria, linahitaji tu kusimamiwa kuhakikisha kwamba hizi sheria zinatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanaouza ving’amuzi mnawafahamu, TCRA wako wapi? Kwa nini wasiangalie kama kweli zinakidhi hayo matakwa ya kuwa na local channels angalau tano ili ziwe zinaonekana pale ambapo watu watakuwa hawajalipia ving’amuzi vyao?

Mheshimiwa Spika, maisha yamekuwa magumu sana, siyo kila mmoja anaweza kulipia king’amuzi kila mwezi. Kuna miezi mingine mtu anashindwa kulipia. Sasa anaposhindwa kulipia, basi asikose uhuru wake wa kuangalia television. Kwa hiyo, tuwasaidie Watanzania hawa waendelee kuangalia television zao zisiendelee kubaki kama mapambo ndani ya nyumba zao.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni usalama wa waandishi wa habari. Kumekuwa na matukio hapa karibuni ya kuvamiwa waandishi wa habari wakiwa wanafanya shughuli zao.

Mheshimiwa Spika, najaribu kunukuu uvamizi uliofanyika katika kituo cha Clouds, lakini pia tukio lingine la kuvamiwa waandishi wa habari kwenye mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Chama cha Wananchi, CUF kule Mabibo. Matukio haya siyo ya kuyabeza, kwa sababu hao waandishi maana yake sasa hivi usalama wao wanapokuwa kazini umekuwa ni wa mashaka sana. Haturidhishwi kabisa na namna ambavyo Serikali ina-react katika kuyakabili matatizo haya. Serikali ina-react very light kama vile haya matukio siyo mazito kiasi hicho.

Mheshimiwa Spika, tunapowafanya waandishi wawe na wasiwasi katika kutekeleza majukumu yao, tunapoteza zile nguvu zao na commitment zao katika kufanya kazi zao kiweledi zaidi. Ni lazima Serikali iwe na mpango madhubuti kabisa kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira yaliyo salama kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni hapa kwenye suala la michezo, kwenye ukurasa wa 44 Mheshimiwa Waziri ameelezea sana michezo lakini amejikita zaidi kuelezea mpira wa miguu. Serikali isituaminishe kwamba tunapozungumzia michezo kwenye nchi hii, basi tunazungumzia mpira wa miguu pekee. Kuna michezo mingi katika nchi hii na ni lazima Serikali iisimamie yote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa Mheshimiwa Waziri anazungumza tu hamasa za kuhakikisha Serengeti Boys inafanikiwa. Kuna michezo mingi zaidi ya huo ambao Serengeti Boys wanaucheza, sasa hao wanamichezo wengine Serikali inawasaidiaje? Tusisubiri tu mtu kashinda mbio huko, ndiyo tunamchukua tunamleta Bungeni hapa tupige naye picha. Tumewekeza nini katika kufikia mafanikio hayo?

Mheshimiwa Spika, tunawekeza kwa Serengeti Boys lakini sifa tunataka kuzichukua kwa watu wanaokimbia riadha, hili haliwezekani. Ifike mahali tukubali kabisa huu mchezo wa mpira wa miguu umeshatushinda, hatuwezi kufanikiwa, figisu zilizopo TFF ni nyingi. Tazama sasa hivi kuna mbinu za makusudi zinazofanywa na TFF kuhakikisha kwamba Simba inapata nafasi ya kushiriki kwenye mashindano ya Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yaani limetengenezwa zengwe kwa sababu TFF inaelekea kwenye uchaguzi wake, wameambiwa kwamba kwa sababu kwa miaka minne Simba haijashiriki mashindano ya Kimataifa, mtakosa kura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa hivi TFF na wenyewe wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha eti Simba iwakilishe Taifa kwenye mashindano ya Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya yana ushahidi usiofichika. Duniani kote matokeo ya uwanjani yanaheshimika, hata kama kuna matatizo yametokea, wanaadhibiwa waliosababisha matatizo hayo, lakini siyo kuhamisha point kutoka timu moja kuzipeleka kwenye timu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuchezea haya matokeo ya mezani, yanaonekana tu hapa Tanzania, lakini huko kwingine kote mpira wa miguu watu wanaheshimu matokeo ya uwanjani.

T A A R I F A....

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, kwanza naipokea kabisa taarifa aliyotoa Mheshimiwa Bulaya, naipokea kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Spika, jambo hili siyo hapo tu. Siyo kwenye point tatu za KageraSugar, hawa Simba wameonyeshwa kubebwa kwenye maeneo mengi. Mechi ya kwanza Simba imecheza na Mbao, zikaongezwa dakika nne na refa akazidisha dakika mbili tena. Mechi ya pili, Simba imecha za na Mbao, refa akaongeza dakika saba, lakini kwenye kucheza zikaongezeka dakika kumi zaidi. Leo hii Mbao FC imeingia fainali na Simba kwenye Kombe la FA tayari viwanja vimebadilishwa mara mbili zaidi.

T A A R I F A...

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi tunachotaka kumtaarifu ni kwamba ukimpa mtu kadi tatu mfululizo anatakiwa a-miss mechi moja mwishoni. Kingine, pilipili usiyoila wewe yakuwashia nini? Kwa sababu Kagera siyo Yanga. (Makofi/Kicheko)

Taarifa......

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, naamini kabisa kwamba pamoja na madaraka makubwa uliyopewa na Kanuni ya tano, lakini pia unaitumia hiyo Kanuni ya tano kwa kuheshimu pia Kanuni ambazo zinanilinda mimi katika uchangiaji na unafahamu tunapochangia hapa tunakuwa tumejipanga, tumejiandaa kwa muda mrefu ili tufikishe kilio cha Watanzania na Serikali iweze kukifanyia kazi. (Makofi)

Pili, zimetoka taarifa hapa sasa sijui unanipa nafasi na zenyewe kwanza nizipokee au nizikatae japo kwa dakika moja au unanisaidiaje katika hili?