Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. JOHN J. MNYIKA: Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ina wajibu mkubwa wa kujenga Taifa linalohabarishwa, lililoshamiri kiutamaduni, lenye kazi bora za sanaa na lenye umahiri wa michezo. Hata hivyo, wajibu huu haujaweza kutekelezwa mpaka sasa na bajeti ya mwaka 2017/2018 haielekei kujenga msingi mzuri wa kuwezesha azma hiyo kutekelezwa ifikapo 2025.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maendeleo ya Sekta ya Habari, Taifa linarudi nyuma kwenye kuwezesha uhuru na haki kwa mujibu wa ibara ya 18 na 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ibara ya 19 ya mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa wa mwaka 1966 ambao Serikali imeridhia. Hivyo, Serikali ifanye marekebisho ya Sheria zote zilizotungwa katika Bunge la Kumi na Bunge la Kumi na Moja zenye kukwaza uhuru na haki wa/ya habari. Aidha, Waziri katika majumuisho aeleze hatua ambazo Serikali imechukua kwa viongozi na watendaji wa Serikali walioingilia uhuru wa habari ikiwemo juu ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuvamia Clouds Media akiwa na watu wenye silaha.

Maendeleo ya utamaduni wa nchi yetu yanategemea sana ukuaji wa lugha ya Kiswahili na matumizi yake. Katika majumuisho Wizara ieleze Serikali imefikia hatua gani katika kuwezesha lugha ya Kiswahili kutumika katika ngazi zote za mahakama nchini. Aidha, Serikali inapoleta Miswada ya Sheria Bungeni inaleta Miswada hiyo kwa lugha za Kiingereza na Kiswahili ambayo inafanya kisheria lugha rasmi ya sheria hizo kuwa Kiingereza, Wizara ishawishi katika Baraza la Mawaziri na ngazi zote za Serikali ili Miswada yote iletwe ikiwa katika lugha ya Kiswahili pekee.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika aya ya 45 ya Hotuba ya Waziri ukurasa wa 25 imetajwa Kamusi kuu mpya ya Kiswahili. Ni vyema Wabunge tukapatiwa nakala ya kamusi husika.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa TFF kuandaa vituo vya ufundi vitakavyokuwa na vifaa stahiki kila mkoa kwa madhumuni ya kulea vipaji ni muhimu katika kuchangia maendeleo ya michezo. Hata hivyo, kwa Mkoa wa kiserikali wa Dar es Salaam idadi ya vijana wenye vipaji ni kubwa kwa mkakati kuweza kutekelezwa kwenye ngazi ya mkoa. Hivyo ni vyema mkakati huo ukatekelezwa kwenye ngazi ya Wilaya na nawasilisha rasmi ombi kwa TFF kwa kituo kuwekwa katika wilaya mpya ya Ubungo katika Jimbo la Kibamba.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa upande wa maendeleo ya soka la wanawake, TFF itoe majibu kwa Wizara ni kwa kiwango gani imeifaidia timu ya Mburahati Queens ambayo inatoa wachezaji wengi kwenye timu ya Taifa ya wanawake kama ilivyoahidi kwa nyakati mbalimbali.