Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa nami nitoe mchango wangu kwenye sekta hii ya maji. Nami nachukua nafasi hii pia kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Engineer Lwenge na Naibu wake, kwa kweli wanafanya kazi kubwa kwa ajili ya Watanzania. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni; wametembelea sana Mkoa wetu wa Manyara, wameona changamoto mbalimbali; pale palipowezekana, walitatua na kule ambako hapawezekani tunaendelea kuwaomba watusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna asiyekubali kwamba changamoto kubwa katika nchi yetu ni uhaba wa maji. Kilio cha Waheshimiwa Wabunge hakijaanza leo, ni miaka mingi huko nyuma na hadi sasa tumewasikia Waheshimiwa Wabunge. Kama kungekuwa na mahali pana nafuu, tungeelezwa humu ndani. Bado changamoto inayokabili Taifa letu ni uhaba wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachosikitisha ni kuona kwamba kila mtu anaeleza kwa ufasaha, anajua changamoto ni uhaba wa maji. Penginepo wanaeleza pia ni namna gani tuondokane na tatizo hili, lakini bado hatuna majawabu. Tuna program nyingi za maji, tuna mikakati, tuna mipango kadhaa, lakini hakuna ambacho tunaweza kutamba nacho leo kusema kwamba mipango hii na program hizi na mikakati hii imeweza kuleta unafuu wa uhaba wa maji kwa kaya pengine hata laki mbili kwa mahali fulani. Hiyo hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tuendelee kuweka mikakati madhubuti ambayo ni halisia. Tufanye nini ili kuondokana na uhaba wa maji? Tuache kulia sana hapa, wapanga bajeti ni sisi wenyewe, mipango yote tunatengeneza wenyewe; kwa hiyo, tukiendelea kulia hapa kwa miaka mingi, nadhani hatuna majawabu. Ni muda muafaka sasa tuweze kupata majawabu, nini kifanyike ili tuweze kuondokana na tatizo hili la uhaba wa maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kuona sura ya umaskini, tembelea kijiji ambacho hakuna hata tone la maji, halafu ukitoka pale tembelea na kijiji ambacho kina maji. Ukitoka hapo utakubaliana nami kwamba kusema kweli maji ni uhai, maji huondoa umaskini, maji huondoa maradhi na maji ni kila kitu; maji ni viwanda na uchumi wa kati katika nchi yetu. Kama hivyo ndivyo kwamba maji ni kila kitu, iweje sasa bajeti ya maji ya mwaka 2016 ambayo ilipangwa shilingi bilioni 900 ikatolewa shilingi bilioni 180 tu kwa ajili ya Sekta ya Maji, hapo ndiyo unakuja mchanganyiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naweza nikawa nimesahau kidogo takwimu naomba radhi, lakini ukweli ni kwamba fedha zinayotolewa kwa ajili ya miradi ya maji ni kidogo sana kulingana na bajeti inayowekwa. Kwa ajili hiyo, naomba tupange bajeti yenye uhalisia, tusiwadanganye wananchi kusoma matrilioni ya pesa hapa, lakini fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi muhimu sana kama ya maji ni kidogo kama ambavyo tunaiona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumza sana kuhusu mikakati ya kuondokana na uhaba wa maji, lakini tunajua kwamba nchi yetu ni tajiri sana, tumejaaliwa na Mwenyezi Mungu, tuna mito, tuna maziwa tuna wataalam waliobobea, nadhani tunakosa ubunifu. Tuanze kubuni ni namna gani tunaondokana na tatizo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa ushauri ambao nilishautoa hata kwenye michango yangu ya huko nyuma, kwamba, tuangalie sekta ambazo tumeshafanya vizuri kiasi fulani kama Sekta ya Barabara, tu pull resources za sekta hiyo pamoja na nyingine ili tuelekeze kwenye miradi ya maji. Tukimaliza kuondokana na tatizo hilo, tunaweza tukarudi kuendelea na sekta zetu za barabara na nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni jambo muhimu ambalo naona pengine litakuwa ni suluhisho pamoja na mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge wameweza kuzungumzia. Ni lazima tuwe wabunifu ili tuweze kufikia mahali tuseme sasa basi tumechoka na kulia kilio hiki cha uhaba wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukikosa chakula unaweza ukaagiza hata kwa jirani yako ukaomba msaada, ama ukaagiza hata nje ama nchi jirani, lakini kwa vyovyote vile huwezi kuomba msaada wa kupewa maji kutoka nje ama kwa nchi jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni sisi wenyewe, majawabu tunayo wenyewe tuone ni namna gani tuweze sasa kukaa chini na kuona tunasaidiaje katika kuondoa changamoto hii ya maji inayotukabili. Kama hivyo ndivyo, iweje bajeti ya mwaka 2016 sasa iwe imeshuka mwaka huu wakati bado tunasema kwamba changamoto yetu kubwa ni uhaba wa maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na wenzangu wote kusema kwamba, tozo ambayo tunaweka kwenye petrol na diesel iweze kuongezwa hadi sh.100/= ili na yenyewe isukume. Siyo hiyo tu, nilikuwa nashauri kwamba tuangalie hata maeneo mengine kama EWURA, TANESCO na kwingineko tujaribu kuona ni namna gani tunajizatiti, tufanye maamuzi magumu kuweza kuondokana na tatizo la uhaba wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumza sana kuhusu changamoto hii, hebu sasa Wizara iweze kukosa usingizi kuhakikisha kwamba inafanya ubunifu kuondokana na tatizo hili la uhaba wa maji. Tukiacha bajeti ya kushuka, Hazina inathubutuje kuchelewesha fedha zinazokwenda kwenye miradi ya maji? Kuchelewesha fedha za miradi ni tatizo sugu la Hazina. Tunataka pia wakati Wizara inafanya majumuisho, ituambie kuna tatizo gani Hazina kuchelewesha fedha za miradi, ikiwepo na miradi ya maji kama ambavyo tunaiona? Tunaomba hili tatizo sugu nalo liweze kuondoka, tusiwachanganye wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mipango yetu na programs za maji, nashauri tuweke benchmarks ili tuweze kupima mipango yetu tunayotengeneza, tuweze kujua kwamba mwaka 2016 tulipanga mipango hii na sasa hii ndiyo benchmark, tumefikia hatua hii, lakini kusema kwamba tunajizatiti ama tunaendelea kupanga mipango ambayo haitekelezeki, ama inatekelezwa lakini haina majawabu, nadhani hatutafikia muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nioanishe uhaba wa maji na maisha ya wanawake wa Tanzania hasa wa vijijini. Kwa bahati mbaya teknolojia ya kisasa haijaweza kumsaidia mwanamke aondokane na tatizo la kubeba maji kichwani huko vijijini. Siyo hilo tu, usafiri wa mwanamke wa kijijini kwa bahati mbaya, teknolojia haijamsadia, bado anatembea kwa miguu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuweze kuwasaidia wanawake hawa wa vijijini hasa wanawake wa jamii ya kifugaji. Wanawake hawa wanaotafuta maji, siyo maji tu kwa ajili ya binadamu, ni pamoja na mifugo.

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.