Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba maji ni tatizo nchi nzima kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kuchangia wameeleza. Natambua jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji kama mahitaji muhimu.

Maji ni kila kitu. Bila kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za maji katika maeneo yetu, hata baadhi ya mipango mingine ya maendeleo kwa ajili ya nchi yetu yanaweza yakakwama. Maji ni viwanda, maji ni kilimo, maji ni afya, maji ni mazingira na maji ni uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana mkono na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kusema kwamba bajeti hii ya Wizara iweze kuongezewa fedha angalau kuweza kufikia bajeti ya mwaka 2016. Ni kwa nini nasema hivi? Kwa bajeti ya mwaka unaoishia sasa 2016/2017, katika Jimbo langu la Ngara nilikuwa nimetengewa shilingi 2,000,045,000 kwa ajili ya mradi wa maji, kukamilisha miradi ambayo ilikuwa ikiendelea na ikiwezekana kuanzisha miradi mipya. Mpaka dakika hii ninavyoongea ni shilingi milioni zisizozidi 400 ambazo zimeshapelekwa kati ya shilingi 2,000,045,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye umwagiliaji zilikuwa zimetengwa shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu katika mabonde mawili; Bonde la Mgozi na Bonde la Mhongo, lakini mpaka dakika hii hakuna hata senti moja ambayo imekwenda kule. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba ni vizuri tukaangalia kuongeza bajeti hii ili tuweze kuangalia mahali ambapo bado panahitaji kupata huduma hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji ukurasa wa 122, amekiri kupungua kwa rasilimali za maji katika maeneo mbalimbali; lakini ameendelea akakiri kwamba yapo maeneo ambayo yana maji mengi na maeneo mengine hayana maji. Nashauri kwamba kama kuna maeneo ambayo yana rasilimali kubwa ya maji, basi maeneo haya yaweze kupewa kipaumbele kwa ajili ya kujenga miundombinu ya maji na vyanzo vya maji viimarishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba usambazi wa maji ni endelevu kulingana na ongezeko la idadi ya watu, lakini tukishajenga katika maeneo yale ambayo tunaamini kwamba vyanzo ni reliable, maji ni mengi halafu tukaendelea kusambaza taratibu kwa kadri tunavyopata fedha, tutaweza ku--cover maeneo mengi ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkutano wa sita, niliuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji nikasema Jimbo la Ngara ni Jimbo ambalo lina vyanzo vingi vya maji. Tuna mito miwili, Mto kagera na Ruvuvu ambayo haikauki; ni maji mengi ambayo yakitumiwa vizuri yanaweza yakasambazwa kwenye mikoa mitatu, Mkoa wa Kagera, Geita na Shinyanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na jiografia ya Jimbo la Ngara kwamba liko kwenye mwinuko wa juu, actual ni kati ya mita 1,200 mpaka 1,800, kiasi kwamba ukiweza kuweka chanzo cha maji pale ukajenga matenki makubwa, tuna mlima mrefu kuliko milima yote Mkoa wa Kagera. Unaweza ukapeleka maji kutoka pale kwa mtiririko kwa gharama nafuu ukasambaza katika mikoa hiyo mitatu niliyoitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme na naendelea kusisitiza Mheshimiwa Waziri kwamba ajisumbue na siyo kujisumbua ni kutekeleza wajibu wake kwamba tunapomaliza Bunge hili, hebu atume team yake ya wataalam kufika Jimbo la Ngara waone vyanzo vilivyopo. Bahati nzuri Naibu Waziri, TAMISEMI tarehe 30, Desemba mwaka 2016 alifika katika Jimbo la Ngara akaona, nikamwonesha mito ile, nikamwonesha mlima huo, nikasema ukitumia vyanzo hivi tutatatua tatizo kubwa la maji katika eneo kubwa la nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado yapo maeneo ambayo mengine hayahitaji pesa nyingi, lakini unakuta ni kero ya muda mrefu. Kwa mfano, kuna eneo la K9 ambalo nimekuwa nikiomba maji kwa muda mrefu, linahitaji shilingi milioni 26 tu kwa ajili ya mtambo wa kusukuma maji na
kusaidia jamii ya wananchi waliopo pale. Kuna taasisi mbalimbali; Sekondari mbili, Kambi ya Jeshi na wananchi walioko pale. Ikipatikana shilingi milioni 26 mtambo unapatikana, unasukuma maji, kero inaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa umwagiliaji, hakuna namna ambavyo tunaweza tukaongeza uzalishaji kama tusipoweza kuboresha scheme za umwagiliaji. Jimbo la Ngara ni jimbo ambalo lina utajiri wa mabonde oevu na tayari kuna mabonde matano ambayo yaliainishwa na Serikali kwa ajili ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, bonde moja lilishaanza scheme ya umwagiliaji; Bonde la Bigombo tangu mwaka 2012. Mradi huu ulikuwa ukamilike 2013, lakini mpaka sasa hivi mradi ule haujakamilika na inaonekana hata Wizara imesahau kabisa kwamba mradi huo upo kwa sababu Mkoa wa Kagera ni wilaya mbili tu; ya Muleba na Karagwe ambayo imeonesha kutengewa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi inayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Jimbo la Ngara kwenye mradi huu wa Bigombo hakuna hata senti iliyotengwa na wala haiko hata kwenye program, maana yake ilikuwa imesahaulika. Kwa hiyo, naiomba Wizara kwa sababu tayari tumeshawekeza pesa shilingi milioni 715 zilitengwa kwa ajili ya mradi huu na karibu zote zimesha-exhaust lakini bado mradi haujakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Wizara husika iweze kufuatilia na kuona ni namna gani ambavyo inaweza ikakamilisha mradi huu kwa sababu tumesha-dump pesa pale na wananchi wanahitaji kunufaika na mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Wizara na nimeanza na Mhandisi wa Maji wa Wilaya, kwamba lazima tutengeneze profile za maji katika maeneo yetu. Najua kwamba jiografia inatofautiana hata kwenye Halmashauri zetu kati ya kijiji na kijiji, kati ya kata na kata. Kuna mahali unaweza ukatumia scheme ya maji ya mtiririko, kuna mahali huwezi, inabidi utumie visima.

Mheshimiwa Naibu Spika,asa tukitengeneza profile hizi, tukajua kwamba mahitaji ni nini kwenye kila kijiji na kata, uwezekano wa scheme ipi itumike katika maeneo hayo, tukawa na profile hii na pengine tukawa hata na makadirio roughly itaweza kutusaidia katika kupanga na kuonesha vipaumbele ili kusudi kile kinachowezekana, kama ni kijiji kina scheme ya kisima, shilingi milioni 20 au 30 zinatosha, basi hilo lifanyike na ndipo hapo ambapo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naunga mkono hoja, lakini naomba kwamba suala la kuongeza bajeti ya Wizara hii lizingatiwe.