Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na taasisi inayoshughulika na kutoa asilimia 25 zinazotokana na fedha za wawindaji katika vitalu vya utalii katika maeneo yetu. Wilaya ya Manyoni tuna vitalu vya utalii lakini Manyoni kuna Halmashauri za Wilaya mbili, kuna Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vitalu 11 katika Wilaya yetu lakini vitalu saba vipo katika Halmashauri ya Itigi na vitalu vinne tunashirikiana pamoja na Halmashauri Mama ya Wilaya ya Manyoni. TAWA tumewapelekea taarifa siku nyingi na mipaka wanaijua, wamekuwa wakipeleka pesa za mgao zile asilimia 25 moja kwa moja kwa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni wakati Halmashauri ya Itigi ipo na akaunti zilishapelekwa kwao, lakini kumekuwa na kizungumkuti hatuelewi. Mpaka sasa hivi Halmashauri yangu ya Wilaya Itigi inaonekana inasuasua katika makusanyo ya ndani kwa sababu tu ya uzembe wa watu ambao hawataki kuwajibika katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri awasiliane na hawa watu na anipe majibu mazuri, kwa nini watu wenye maeneo hawapelekewi pesa katika eneo lao. Tuna Halmashauri kamili na tunatakiwa pesa zile ziende kwetu. Hivi tunavyozungumza pesa za mwezi huu ambao umekwisha hawajapeleka, lakini miezi ile iliyokwisha walipeleka milioni 128 katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na pesa za Itigi zikiwemo. Sasa ni kitu gani hawajui au hawataki, kama hawataki kutupa waseme tu basi ninyi mkae kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki na usawa huu Halmashauri kama ile tuanze kuhangaika wakati tuna kitu chetu pale. Naomba hawa wataalam, sasa sijui ni Mkurugenzi au ni nani kwenye hicho kitengo amweleze Mheshimiwa Waziri. Mimi nitalia na Mheshimiwa Waziri kwa nini sisi hatupati hizi pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tuna vitalu vya utalii, tuna mbuga ya Rungwa, Muhesi lakini na mbuga ya Kizigo. Rungwa, Muhesi iko katika Jimbo langu na kuna changamoto kadhaa zinazotokana na wanyama hawa kuwemo katika maeneo yetu, wamekuwa wakivuka mipaka yao na kwa sababu wanyama hawana akili wanaingia maeneo ya watu na wanafika mahali wanaua watu wetu, lakini wanakula mazao ya wananchi ambayo wameyalima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukitoa taarifa hapa katika Bunge hili, wapiga kura wangu wawili wamepotea, kwa hiyo nimepoteza kura za watu waaminifu kabisa, lakini wakati huo huo sasa tulitoa taarifa kwa Mheshimiwa Naibu Waziri hatua zilichukuliwa kidogo hazikuwa na uzito naomba mara nyingine tukiwapa taarifa kuna watu wa Rungwa pale, kuna kikosi kikubwa kabisa cha KDU pale Manyoni, hawachukui hatua hata kufika kwenye eneo la tukio kuwafukuza wale wanyama warudi katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara hii wazingatie kuwa karibu na wananchi ambao wanawachunga wale wanyama lakini wanapodhuriwa basi wafike haraka na tutoe kifuta machozi hicho ambacho wamekianisha japo ni kidogo sana, lakini kifike kwa wakati, ili watu kabla hawajaanza kuchoka na kujisika huzuni kwamba Serikali yao inawatelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi katika Sekta ya Misitu. Wizara hii niipongeze kwa kazi nzuri ilizofanya lakini kuna upungufu kadha wa kadha. kuna baadhi ya Maofisa wao ni wala rushwa sana. Suala hili tumelisemea sana na Mheshimiwa Waziri anajua, nilishamwona na nikamwambia, walishafikishwa hadi Mahakamani, wamekamatwa na rushwa katika check point, lakini viongozi wa pale TFS pale Makao Makuu waliamua kumtoa yule mtu pale. Badala ya kumtoa Mheshimiwa Waziri kamrudisha matokeo yake sasa lile eneo lote linanuka rushwa. Ni vizuri mtu anayetuhumiwa kwa rushwa akakaa nje ya mfumo wa makusanyo kodi au maduhuli kwa sababu tu atasababisha na ataambukiza, samaki akioza Mheshimiwa Waziri ataambukiza na yeye atanuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote samaki akioza katika tenga, anaweza akasababisha ukatupa tenga zima. Sasa ni vizuri ukawahi kutoa ili wale samaki wengine wazuri tuwapeleke katika masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kumekuwa na matukio machache ambayo Wizara hii lakini hasa wadau hawa wa TFS wamekuwa wakiyafanya, mengi ni ya kupongeza lakini kuna changamoto kadha kidogo. Bei ya TIKI katika minada kama hivi hapa majuzi juzi, katika mnada wa Mtibwa kulikuwa na shida lakini bahati nzuri Lunguza niwapongeze wamefanya vizuri, wameuza vizuri na wamepata bei nzuri, kwa hiyo wanaisaidia Serikali yetu katika kukusanya maduhuli, kuna changamoto kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnategemea viwanda vya misitu vifanye kazi kwa maana viwanda vile vina matatizo sana ya Saw Doctor, hapa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 85 Chuo cha FITI hajakipa uzito, hatuna Saw-Doctor kabisa nchi hii na wachache wale mnaozalisha wengi wanachukuliwa na Serikali. Sekta binafsi hii ambayo inategemewa ndiyo watakaokuwa wana- process haya mazao ambayo mnayauza, hawana Ma- Saw Doctor. Je ni utaratibu gani mtatumia hao watu mnaowazalisha pale FITI japo ni wachache, kwa sababu katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri, ameonyesha ni watu 80 tu na kitu hawafiki hata 100 kwa mwaka ambao anawazalisha katika soko la ajira, Serikali hao hao inawahitaji, na wengi wanapotoka FITI hawaajiriwi kama wataalam wa misumeno matokeo yake wanarudi kuwa Forester na kazi kubwa wanapewa ya kukusanya maduhuli. Mheshimiwa Waziri ajitahidi kutuonyesha na wale wadau wa misitu wanapataje wataalam wanaozalishwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa hivi hakuna chuo kingine mbadala cha kuzalisha Saw Doctor, katika nchi hii. Inafika mahali makampuni mengi wanaanza kuajiri wageni kwa sababu upande wa Serikali ikishawazalisha inawaajiri wao, lakini upande wa sekta binafsi hamna. Hatukatazi ajira kwa vijana wetu tunafurahia sana, wanapoajiriwa na soko kuu ambalo ni rasmi, lakini watoe basi fursa kwa watu ambao wanahitaji kupeleka vijana wao pale FITI basi gharama ziwe rafiki ili Saw Doctor kutoka katika viwanda binafsi nao waweze kuhudumiwa na chuo hiki ambacho ni cha umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ya mkaa, Serikali imekuwa ikizuia mkaa kutoka eneo moja kwenda lingine, wameanzisha magulio kama walivyosema, lakini haiwawezeshi wadau ambao wanataka kutengeneza hata mkaa mbadala. Mkaa mbadala unaotokana na nyasi, mkaa mbadala unaotokana na vumbi la mbao, yote hii Serikali haijaonesha dhamira ya dhati, inapozuia mkaa unaotokana na miti. Ni vizuri sasa basi tutafute katika Mfuko wa Misitu au mahali unapoona.

Mheshimiwa Waziri hata mimi akiniwezesha nitazalisha mkaa, mimi ni mdau wa mazao ya misitu najua vizuri. Sasa watuwezeshe sisi wadau tuweze kuzalisha mkaa tuondokane na kukata miti. Wakati huu hakuna mbadala unaooneshwa, hata bei ya gesi bado siyo rafiki sana kwa wananchi wetu, wakulima wa vijijini. Watanzania walio wengi wanatumia mkaa tukiacha wale wa miji mikubwa tunatumia sisi wa vijijini pia. Sasa siyo rafiki, mtungi wa gesi unakaribia laki moja, Sh. 65,000 - 70,000 mpaka 90,000 ule mtungi mkubwa, sasa ni vigumu sana kwa mtu wa kawaida uweze kutumia. Tusaidieni sisi tuweze kusaidia hilo ambalo litatufika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ufugaji nyuki halijatiliwa maanani kabisa, Mheshimiwa Waziri amelizungumza juu juu, hakuna mizinga angalau anaweza akatupa; kila Mbunge akapata hata mizinga 100 tu akapeleka katika maeneo yake. Maeneo ya misitu tunayo mengi, ili tuondokane na umaskini huu. Katika Tanzania ya viwanda ameonesha kiasi kidogo cha nta kilichouzwa katika soko la nje, lakini Serikali inaweza ikawekeza na namna ya kuwekeza ni kidogo tu, ana wadau wengi, asaidie wananchi... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.