Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante awali ya yote naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nje ya uhifadhi haya yote tunayoyazungumzia hayatakuwepo, tunayaona haya kwa ajili ya uhifadhi na sisi tukiwa binadamu mzigo tunamtwisha Waziri wetu Maghembe na watendaji mbalimbali, lakini nafasi ya uhifadhi ni ya kila mmoja na ndio maana hata kwa kupitia kitabu cha Mwenyezi Mungu kitabu cha Mwanzo binadamu alipewa wajibu wa kuja kuitawala dunia na viumbe vilivyopo hapo ikiwa ni misitu na vitu vingine vya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba kuna kauli ambayo huwa naiongea mara zote nikipata nafasi, mazingira yaliyoharibiwa hayana huruma, yatatuadhibu tu hata kama ni miaka 50 ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nitajikita zaidi kwenye utalii na uhifadhi. Nafahamu kwanza tunapoangalia matatizo tusiangalie kana kwamba hatujawahi kuwa na wakati tulivu tuyaangalie matatizo kwa namna ya kuyatatua, nikilisema hilo kwa kitabu cha wenzetu wa wanyamapori tunaambiwa kuhusu umuhimu wa maeneo yaliyohifadhiwa. Wanasema hivi; “Maeneo yaliyohifadhiwa yana umuhimu mkubwa nchini kiikolojia, kiuchumi na kijamii, aidha maeneo haya huchangia ustawi wa sekta nyingine kama vile mifugo, kilimo, nishati na maji,” hilo eneo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikilisema hilo nataka kumaanisha nini, leo hii tukihifadhi asili itatulinda na tunapewa nafasi ya kuamua ni lipi lifanyike na kwa wakati gani. Mfano, wapi tuchunge, wapi tulime, wapi tujenge na tusipohifadhi tutakimbizwa na matukio kwa mfano ukame wa kutisha, mafuriko, mimea vamizi na magonjwa pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna watu tunaweza tukaona ni kwa nini wataalamu wanatuambia ikiwezekana tusichanganye mifugo na wanyamapori, kuna magonjwa ya ajabu, magonjwa ambayo baadae binadamu huyu kumtibia ni kazi ya ziada kutokana na hiyo ya kuwachanganya hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wakati mwingine tuendelee kuheshimu maelekezo ya kitaalamu, na mimi naamini sisiwote lengo letu ni kuijenga nyumba moja, kwa hiyo tusigombee fito kama tatizo ni la mifugo turudi kwenye ufumbuzi. Je, tunasemaje mimi nafarijika sana, majuzi nikienda Dar es Salaam nilipita Kongwa pale kwenye ile ranchi nikabahatika kupata nyama nzuri kupelekea familia. Kwa maana ya ranchi tunasemaje kuwasaidia watu hawa wakati fulani kulikuwa na ajenda hiyo kwamba wakulima tuendelee kuangalia namna ya kuwasaidia kuwa na ranchi ndogo ndogo ili kuepukana na tatizo hilo. Kwa hiyo twende kwenye kutatua matatizo tusiwe walalamikaji twende kwenye kutatua matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda Kilombero, nikafurahia uumbaji alioutenda Mwenyezi Mungu na katika hili niseme, bonde lile nilifurahi kusikia kwamba hata maji wanayokunywa Dar es Salaam kumbe ni kwa sababu kuna watu wengine wametunza mazingira yao, kwa hiyo, mmoja amefanya kazi kubwa ya kutunza lakini kwa msaada wa watu wengine kwa hiyo nilikuwa naendelea kuliomba hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikiwa mjumbe wa Kamati hii majuzi nilikwenda Ngorongoro nikaenda Loliondo nilifurahishwa sana na ule usemi wa kiingereza unaosema seeing is believing, niliweza kuona na nikaamini maajabu ya uumbaji aliyoyafanya Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,Ngorongoro na Loliondo ile tuamue tunataka nini kama kweli tunahitaji uhifadhi sheria na taratibu nyingine zizingatiwe, nje ya hapo kama hatulitaki hili tuamue jambo lingine. Sisi politicians kwa maana ya political will tuna nafasi kwamba sasa tunasema uhifadhi, utalii kwa ujumla wake ukae pembeni tutafanya mambo mengine, lakini ukirudi kwa maana ya vyanzo vya mapato fedha zinazoingizwa katika maeneo hayo ni habari isiyofichika kwa mfano ukiangalia ukurasa huu unasema kwamba katika mwaka wa fedha 2013/2014 utalii pekee ulichangia takribani17.2% ya Pato la taifa ikilinganishwa kwa mfano na michango kutoka GDP kwa mwaka huo ya mazao ya kilimo ilikuwa 17.8%, mifugo 8.4% na uvuvi 2.4% kwa miaka miwili mfululizo utaliona hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mi naendelea kusema tukiacha hilo la pato la Taifa kwa kupitia utalii mimi nina ushauri ufuatao, tusiwe kwamba tunafanyia kazi msaada wa Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hapa tulipo. Tumechukua hatua gani sisi kama binadamu baada ya msaada wa Mwenyezi Mungu kwa maajabu haya ambayo ametupa kuwa na Ngorongoro nzuri, Mlima Kilimanjaro na mbuga nyingine, initiative sisi kama sisi tumefanyaje Mheshimiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna watu wanaenda kufanya utalii kwa sababu binadamu amehangaika kujenga jengo refu, mnaenda kushangaa jengo refu lakini vipi sisi ambao Mwenyezi Mungu pekee ametupa maajabu haya why can’t we work on it? Kwa nini tusifanyie kazi?

Kwa hiyo, mimi naendelea kusisitiza ndugu zangu bila ya uhifadhi itabaki kuwa gumzo, na leo hii kuna mtu unatamani hata kwamba bora nimpeleke ng’ombe pale kwa sababu ni eneo limehifadhiwa ni eneo limetunzwa, turudi tu kama kuna tatizo ya usimamizi wa sheria tujikite hapo, tusimamie sheria, taratibu na kanuni, mimi ushauri wangu ni huo. Lakini eneo jingine tena nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri kwa maana…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.