Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Nianze mchango wangu kwa sekta nzima ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya utalii imekuwa ikichangia asilimia 17 ya Pato la Taifa ukilinganisha na sekta zingine. Kwa tafsiri nyingine unaweza ukasema Pato la Taifa chanzo chake kikuu ni sekta ya utalii. Sekta hii ya utalii imekuwa na changamoto nyingi ambazo zinazidi kuongezeka. Kama changamoto ni nyingi na zinazidi kuongezeka maana yake sekta hii haiwezi kukua na kuendelea kuongeza Pato la Taifa kwa maana ya kutoka kwenye hiyo asimilia 17 kwenda hata angalau asilimia 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa changamoto zilizopo kwenye sekta hii, imekuwa haitiliwi mkazo kutangazwa ipasavyo. Mikakati ipo lakini inawezekana fedha zinakosekana ya kutangaza kwa upana sekta ya utalii ndani na nje ya nchi, imekuwa ni changamoto ya muda mrefu ndio maana tunabaki palepale hatuwezi kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine Serikali haina ubunifu wa kuongeza vivutio vingine vipya. Tumekuwa na vivutio vya zamani na hivyo vingine vimetelekezwa, lakini hakuna ubunifu wa kuwa na vivutio vipya ambavyo vitawashawishi watalii waweze kuja kuangalia kwa wingi hapa nchini. Kwa hiyo, ni wajibu wa Serikali kuangalia namna gani vivutio vilivyopo mnaviendeleza, lakini mnabuni vivutio vingine ambavyo vitaweza kuhahakisha kwamba watalii wanakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linaifanya sekta hii ya utalii iwe na changamoto kubwa ni masharti magumu kwa wawekezaji ikiwemo suala la kodi. Katika Awamu ya Nne kodi ambazo zilikuwa zinalipwa na wawekezaji katika sekta ya utalii ilikuwa ni kodi kati ya 14 mpaka 16. Leo Serikali ya Awamu ya Tano mmeingia madarakani mmepandisha kodi ambazo wanalipa wawekezaji katika sekta ya utalii zimetoka 14 mpaka 36 na sasa hivi ninasikia tena mnataka kupandisha nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hizi au namna gani kama mnaongeza kodi hakuna mwekezaji ambaye atakuja ku-invest kwenye sekta ya utalii na tukaona inakuwa atakuwa anazikimbia hizi kodi. Kwa hiyo, tunatarajia kwamba muende mkae, mpunguze kodi muweze ku- encourage wawekezaji wengi ili sekta ya utalii iweze kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika haya haya masharti magumu, leo mtu akitaka kupata TALA licence unalipa dola 2000 kwa magari kuanzia matatu. Tunajua huko huko nyuma ilikuwa ni magari matano unalipa dola 2000, mkapunguza mkafanya magari matatu kwa dola 2000, lakini kwa wale vijana wa Arusha ambao maeneo yenye utalii atapambana atapata magari matatu atalipa dola 2000, huyu anashindana na mwekezaji mkubwa mwenye magari 100 naye analipa dola 2000. Kwa mfano, Leopard Tours wana magari kibao, naye analipa TALA licence ya dola 2000. Halafu kijana wa Arusha anajitahidi amepata magari matatu naye analipa dola 2000. Kwa nini Wizara msifikirie kupunguza hii TALA licence mkalipa TALA licence kwa gari ambayo itaiingizia Serikali mapato zaidi; yule mwenye magari 100 atalipa kulingana na idadi yake ya magari na yule mwenye magari matatu naye atalipa kulingana na idadi yake.

Mheshimiwa Waziri hii limekuwa ni kelele ya muda mrefu lakini hatupati majibu ya kuwasaidia hawa. Pia itawasaidia na ninyi kuongeza mapato, kwa hiyo, ni vizuri mkalifikiria hilo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine katika sekta ya utalii ni ushiriki mdogo wa maonesho ya utalii na kutokupewa kipaumbele. Masuala mazima ya maonyesho ya utalii na vivutio vya utalii inaoneka imeachiwa sekta binafsi na Serikali imekaa pembeni, imekuwa ni changamoto ya muda mrefu. Sasa kama ninyi mkaa pembeni mnaziachia sekta binafsi ziende zenyewe zijitangaze, zijipambanue na kuonesha wana vitu gani, ni kwa namna gani sekta hii itaweza kukua. Haiwezi kukua obviously kutakuwa kunaendelea kuwa na changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni vyuo vichache vya utalii vinavyotoa mafunzo ya utalii na imekuwa ikitoa mafunzo duni haiendani na kasi ya ukuaji wa utalii. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali mkafikiria namna gani kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kwamba vyuo vya utalii vinakuwa na ubunifu zaidi, lakini inaendana na kasi ya ukuaji wa utalii duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la migogoro ya vijiji na hifadhi za wanyamapori. Migogoro hii imekuwa ni migogoro ya muda mrefu, ni migogoro ambayo ndani ya Bunge tumekuwa tukisema lakini unachokiona tukipiga kelele kuhusu migogoro, Serikali mnakimbilia kuunda Tume. Mnakimbilia kuunda Tume, mnatuahidi kwamba Tume zikifika maeneo hayo mtashirikisha wadau mbalimbali, wanafanya kazi hizo wanamaliza hatujawahi kusikia ripoti ya Tume hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2009 Bodi ya TANAPA iliunda Tume ya kuchunguza migogoro ikatoa mapendekezo, sijui yamefanyiwa kazi kwa kiasi gani. Mheshimiwa Waziri Mkuu wa zamani Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda aliunda Tume, Mheshimiwa Kagasheki akiwa Waziri aliunda Tume, Mheshimiwa Lukuvi aliunda Tume na sasa hivi nasikia mmeunda tena Tume inayohusisha sekta zote lakini hakuna majibu. Serikali mkisikia migogoro ya wananchi na hifadhi badala ya kutuletea majibu mnakimbilia kuunda Tume zinazotumia fedha nyingi za walipakodi, taarifa ya Tume mnaweka kapuni hamtuambii. Leo hapa msimame mtuambie angalau ni mgogoro gani ambao mmeumaliza? Hamna na migogoro inaendelea! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kila siku kuona wananchi wanashughulikia tu migogoro wanaacha shughuli zingine, Serikali mnakimbilia kuunda tume ambazo hatupati majibu yake. Kwa hiyo, nafikiri ni wakati muafaka sasa Serikali mtuambie kwanza hizi Tume zote ambazo mmeziunda majibu yake yako wapi? Ripoti yake iko wapi? Utekelezaji wa matokeo ya Tume hizo umefanyika kwa kiwango gani? Kwa nini kama ambazo hazijafanyika ni kwa nini imeshindikana kufanyika mpaka sasa hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la mgogoro wa Loliondo. Mgogoro wa Loliondo pia ni kati ya migogoro ambayo imekuwa ni ya muda mrefu. Leo Serikali inataka kuondoa wananchi takribani 54,000 katika vijiji 14 waondoke kwenye eneo la kilometa za mraba 1,500, hivi unawaondoa watu 54,000 unawapeleka wapi? Huko unakowapeleka si ndiyo unaenda kuendeleza mgogoro mwingine wa ardhi? Serikali mtuambie mna maslahi gani na suala la Loliondo, kwa nini mmeshindwa kulipatia ufumbuzi wa muda mrefu? Kwa sababu umekuwa ni mgogoro wa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala mtuletee ufumbuzi wa tatizo la Loliondo, mnakimbilia mnasema NGO’s zilizoko Ngorongoro zinachochea wananchi kuendeleza migogoro hii. Kwanza hizi NGO’s zilizo nyingi zimesaidia kujenga uelewa wa wananchi wa kule, lakini kama kweli kuna NGO’s ambazo zinafanya ushawishi na uchochezi it is okay zichukuliwe hatua lakini siyo kuzihukumu NGO’s zote labda kwa sababu ya baadhi ya NGO’s ambazo zinafanya ndivyo sivyo.

Kwa hiyo, Serikali mtuambie hivi mna maslahi gani na huyu Mwekezaji wa Loliondo huyo OBC huyu Mwarabu mtuambie? Huu mgogoro umekuwa wa muda mrefu, mnaenda mnaunda Tume, sijui Waziri Mkuu ameunda Tume, sijui Waziri umeenda, Mkuu wa Mkoa Gambo ameenda, sijui ataenda na nani labda aje na malaika naye aende, lakini hamtupatii ufumbuzi, kwa nini wananchi wa Loliondo wanateseka kwa muda mrefu? Mtuambie Mheshimiwa Waziri kwanza mna maslahi gani na huyu Mwarabu na kwa nini mgogoro huu haumaliziki?(Makofi)