Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda nimshukuru sana Mwenyenzi Mungu aliyenijalia wakati huu kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia kwa unyenyekevu mkubwa sana niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Madaba ambao kwa umoja wao wamenituma nifanye kazi yao wakiamini kwamba nitawatendea haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kupongeza sana hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa kwa Bunge lako Tukufu. Hotuba hii imejaa hekima kubwa lakini pia imejaa matumaini makubwa sana kwa wananchi wa Tanzania na hasa kwa wananchi wa Jimbo langu la Madaba. Hotuba ya Mheshimiwa Rais kwa sehemu kubwa imetoa mwelekeo wa Taifa letu kwa kipindi cha miaka mitano. Kwa hakika hotuba yake imeshakwishaanza kutafsiriwa kwa vitendo kupitia utekelezaji wa kazi hizo, lakini pia kwa kupitia Baraza lake la Mawaziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Mawaziri wote wa Awamu ya Tano, wanafanya kazi kubwa kwa ajili ya Watanzania. Kwa namna ya pekee sana naomba sana niwashukuru sana Mawaziri ambao tayari wameshakuja kwenye Jimbo langu na tayari wameanza kufanya kazi na wananchi wa Jimbo langu. Kwa namna ya pekee nimshukuru Mheshimiwa Ummy Mwalimu, tayari amekuja kuangalia changamoto za afya na sasa yupo kwenye mchakato wa kuhakikisha kwamba tunapata hospitali ya Wilaya, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa heshima kubwa nimshukuru sana Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini katika mazingira magumu na muda mgumu alifika katika Jimbo langu kuangalia changamoto ya umeme na kuipatia majibu pale pale. Namshukuru na kumpongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika uchangiaji wangu nitajikita katika maeneo machache muhimu yanayohusu maslahi ya Taifa letu. Moja ni eneo la viwanda. Katika hotuba ya Mheshimiwa Rais toka ukurasa wa 13 – 16 anaeleza ni namna gani Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuifanya sekta ya viwanda iwe sekta mama itakayotoa ajira za uhakika kwa Watanzania. Mheshimiwa Rais anakwenda mbali zaidi na kueleza namna gani hiyo sekta ya viwanda inakwenda kujibu matatizo ya masoko ya mazao, mifugo pamoja na uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii kwa uzito ambao Mheshimiwa Rais ameupa na kwa hali halisi ya Tanzania ni sekta muhimu sana. Nitumie nafasi hii kupongeza hatua ya Mheshimiwa Rais kuzingatia viwanda lakini naomba nitoe tahadhari kwa wale ambao wamepewa kusimamia utekelezaji wa jukumu hili. Moja, lazima tujue kwamba sekta ya viwanda ina mahusiano makubwa sana na sekta ya biashara lakini pia kwa sababu hivyo viwanda vinahusu kilimo, uvuvi na mifugo, sekta hizi zote zinafanya kazi kwa karibu sana. Sera ya kuimarisha viwanda ndani ya Tanzania siyo sera ngeni, kigeni katika Awamu hii ya Tano ni mikakati mipya ambayo Mheshimiwa Rais amekuja nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tujifunze ni nini kilisababisha viwanda vyetu vya miaka ya 1980 na 1990 na kuelekea mwaka 2000 vikafa. Mikakati ya ndani ni mizuri, mitaji ilipelekwa lakini naomba wanaohusika na maandalizi na usimamizi wa eneo hili wakubali kurudi tena kwenye kusoma uzoefu hasa unaogusa sera zetu za nje, mikataba yetu na makubaliano ya kibiashara na mataifa mbalimbali zikiwemo jumuiya mbalimbali zenye maslahi ya kibiashara na Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia kwa undani pamoja na jitihada za ndani za kuzalisha mazao ya viwandani, mazao yetu yameendelea kukosa soko kwa sababu tumefungulia kiholela mazao ya viwandani yanayotoka mataifa mengine. Ndani ya Mkoa wa Ruvuma nimepambana sana kwa miaka zaidi ya sita kuhakikisha kwamba sekta ya mazao ya mafuta yakiwemo alizeti inakuwa sekta tegemezi kwa uchumi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuhakikisha kwamba tunazalisha mafuta ya kula ya kutosha yatakayoweza kukidhi mahitaji ya mkoa. Hata hivyo, jitihada hizo zimeangamizwa na mafuta ya bei rahisi yanayoingizwa toka Malaysia na nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo eneo halitaangaliwa vizuri, Watanzania tutaenda kuwekeza kwenye viwanda na tutafilisika na tutabaki maskini wa kutupwa kwa sababu Tanzania mpaka sasa imeendelea kuwa soko kubwa la mazao ya viwandani yanayotoka nchi zingine. Kwa hiyo, nashauri sera yetu inayohusiana na maeneo hayo iangaliwe vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ni mama kwa uchumi wetu ni kilimo na mifugo. Niishukuru sana Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Waziri Mwigulu na timu yake wananchi wa Madaba kwa namna fulani wamefaidika sana na Wizara hii kwa asilimia 75 ya wakazi wake kufanikiwa kupata pembejeo za ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu wa ruzuku siyo endelevu. Msimu wa mwaka jana wananchi wa maeneo yale hawakupata pembejeo za ruzuku iliathiri sana uzalishaji wao. Najua mfumo huu umechukua uzoefu kutoka Malawi na maeneo mengine na hapa tunau-apply. Naomba Wizara inayohusika na kilimo na mifugo tuchukue hatua za makusudi kujifunza mifumo mingine inayopendekezwa na wadau mbalimbali wa kilimo. Najua kumekuwa na miradi mbalimbali ya wadau wa kilimo inayojaribu mifumo mbalimbali ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata pembejeo kwa namna endelevu. Naomba sana Wizara hii iandae utaratibu maalum wa kufanya utafiti wa mifumo inayofaa. Mfumo huu hauna uendelevu kwa sababu unategemea asilimia 100 ruzuku ya Serikali, ruzuku ambayo hatuna uhakika nayo. Kuna mifumo ya kuwaunganisha wasindikaji, wanunuzi wa mazao, wasambazaji pembejeo pamoja na vikundi vya wakulima kwa kupitia mfumo wa mikataba ambayo itawasaidia kupata mikopo ya pembejeo, uhakika wa masoko ya kilimo na uhakika wa uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mengi nyeti yanayowagusa wananchi wa Jimbo la Madaba, eneo la soko la mazao ni mgogoro sana kwa sababu mpaka sasa tunategemea Serikali pekee kununua mahindi kupitia NFRA. Nashukuru sana Wizara ya Kilimo wamefanya jitihada kubwa sana kukarabati maghala ya kuhifadhia mazao wakati wa mavuno. Hata hivyo, maghala yale yametengenezwa kwa pesa za wakandarasi, wakandarasi hawajalipwa, hawajamaliza na mwezi wa sita wananchi wanaanza kuvuna hawana mahali pa kuhifadhia mazao yao, tunaomba hilo nalo liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo gumu sana kwetu Madaba ni maji. Wananchi wa Madaba hawana maji, Jimbo la Madaba ni jipya, Halmashauri ya Wilaya mpya, Makao Makuu maji ni mgogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunisikiliza. (Makofi)