Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa sababu imeonyesha mwelekeo wa wapi Serikali inatakiwa itekeleze katika vipaumbele vyake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufugaji wa nyuki, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kukuza ufugaji wa nyuki lakini bado Watanzania hawana elimu ya kutosha ili wayatumie mapori yetu kupata asali kwa ajili ya biashara. Serikali itoe elimu kwa Watanzania waweze kufuga nyuki kisasa na wayatumie mapori yetu vizuri ili wapate kipato. Wizara iwasaidie vijana, wafugaji kwa kuwapa elimu, mikopo na vifaa vya kufugia nyuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwindaji haramu; pamoja na Serikali kuendelea kupinga biashara hii haramu, ujangili na mauaji ndani ya mbuga zetu, nahitaji kufahamu mambo haya na nisipopata majibu nitashika shilingi.

(i) Kuna Mchina alikamatwa na lori la meno ya tembo katika mbuga ya wanyama Katavi. Mchina yule akaachiwa eti alikuwa hajui Kiswahili. Je, hamuoni kwamba kuwaachia maharamia hawa ni Serikali imeshindwa kusimamia uharamia huu? Naomba majibu Mchina alifanywa nini na kesi ikoje?

(ii) Kuna taarifa kuhusu majangili kutoka nchi jirani za Rwanda, Kongo na Burundi wanaingiza makundi ya ng’ombe mbugani wanajifanya wanachunga au wamepotea njia na kuingia hifadhini. Je, Usalama wa Taifa kuhakikisha upotevu na uharamia huu haufanyiki uko wapi kuyasemea haya? Je, hamuoni ujirani huu tusipokuwa makini tutapoteza rasilimali zetu? Mkakati wa Serikali kuhakikisha mnazuia hawa maharamia wafugaji kuingia na kuvuna pembe za ndovu ukoje?

(iii) Rushwa kwa wawekezaji katika mbuga zetu. Serikali imeweza kudhibiti rushwa hizi na kulinda uwindaji haramu, waliokamatwa na pembe za ndovu kuachiwa Wizara ya Maliasili imeshindwa kusimamia hili.

(iv) Wafanyabisahara (wa China) wa meno ya tembo kuendelea kuisaidia Serikali kutoa misaada ni kujificha nyuma ya pazia.
(v) Usimamizi wa ukataji miti hovyo Kibaoni, Nkasi leo hii ni jangwa kabisa. Serikali ione namna ya kuzuia uharibifu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuboresha mbuga za Mikoa wa Kusini; Lindi/Mtwara (Selous), Katavi (Katavi), Rukwa (Rukwati), kuna kigugumizi gani kuzitangaza mbuga hizi? Mnaitangaza Serengeti kila leo wakati kuna mbuga kubwa hamzitangazi kuna nini hapo? Katavi kuna twiga mweupe na tembo wakubwa lakini Serikali haina mkakati kabisa wa kuzitangaza mbuga hizi kuna nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa miundombinu, Serikali iboreshe viwanja vya ndege Katavi, Kigoma na Mwanza ili watalii wasipande ndege zaidi ya mbili kufika Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua ni namna gani Serikali itaitangaza Katavi angalau tupate watalii kutoka Zambia? Kwa nini Mikoa ya Kusini hamuitangazi mnaendelea kuzitangaza mbuga ambazo zimetosha kutangazwa kama Serengeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa operation tokomeza ujangili, ni lini mtawafidia wananchi waliochomewa nyumba zao, biashara zao, wakabakwa, wakateswa nje ya utaratibu wa kutafuta majangili? Ni lini mtawalipa hawa wananchi fidia zao kwa mateso waliyopewa; na huku Askari Wanyamapori wapo wanaishi kwa furaha huku wananchi hawa wakiishi katika mazingira magumu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvunaji wa misitu, magogo na mbao, kuna uharibifu wa misitu unafanyika katika mapori yafuatayo:-

(i) Ipole – Tabora;
(ii) Inyonga – Mpanda;
(iii) Lyamgoloka – Mpanda Vijijini; na
(iv) Jimbo la Nsimbo – Kata nyingi zinafanya biashara hizi na watendaji wa Kata kuuza magogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati gani wa kuwawajibisha hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhifadhi wa viboko katika Mbuga ya Katavi unahatarisha uhai wa viboko kutokana na kukithiri kwa vizibo vya umwagiliaji na viboko kukosa maji.