Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, angalau nami nimepata nafasi ya kuchangia Wizara ya Elimu na naomba niseme kwamba mimi ni mdau, ni Mwalimu, kwa hiyo, angalau naelewa mambo mengi ya hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana; kabla sijaanza kuchangia hoja zangu za msingi, lakini angalau nilalamike kuhusu suala moja la Halmashauri yangu ya Songwe. Nilikuwa napitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa kwenye kitabu hiki, naona Halmashauri yangu ya Wilaya ya Songwe haijapata vitabu kabisa katika huu mgao wa vitabu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri wengi wanachanganya ama niseme sijui ni Makatibu Makuu; wanapoandika Mkoa wa Songwe, wanapoanza kuorodhesha zile Wilaya hawaiweki tena Songwe kwamba kuna Wilaya ya Songwe. Naomba watambue, kuna Mkoa wa Songwe halafu kuna Wilaya ya Songwe, Mbozi, Ileje na Halmashauri ya Tunduma na Momba. Kwa hiyo, kuna Halmashauri tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimesoma humu nakuta vitabu vyote vimeenda Ileje, vimeenda Momba, vimeenda Tunduma, vimeenda na kule Momba. Sasa huku kwangu sipati. Kwa hiyo, mwaka huu sijapata vitabu, sasa sijui nimwendee nani. Kwa hiyo, nitakwenda pale Wizarani wanipe vitabu nisafirishe mimi mwenyewe nipeleke, maana naona hii sasa ni hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sasa nichangie hoja zangu zile za msingi. Nianze na kuunga mkono hotuba ya Kamati ya Huduma za Jamii iliyosomwa na Mheshimiwa Bashe pale kwenye kuishauri Wizara kuhusu mambo fulani na changamoto za Wizara ya Elimu. Tukianza na utaratibu wa viwango vya ufaulu katika shule binafsi. Mimi ni mdau, naomba ku- declare interest hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ikifika mwezi wa Kwanza shule za private tunakuwa na joining instruction, wanaandika; ili uingie katika shule yangu, unatakiwa ufaulu asilimia labda 41 ama 50 kama zilivyo Seminari. Shule za Serikali utaratibu huo hamna, ukishafaulu arasa la saba, unaendelea mpaka ukaukute Mtihani wa Taifa wa Form Two na mpaka umalize Form Four. Form Two yenyewe ni alama 30 ambayo mimi kama Mwalimu nasema bado ni alama ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inafika mwezi wa 12, mtoto yule hajafikisha hata wastani wa alama 33 mpaka 35. Wanaambiwa; sasa bwana inabidi urudie darasa. Anayekuja kulalamika mtoto kurudia darasa ni mzazi mwenyewe aliyelipia ada, lakini ukienda kwa Afisa Elimu wa Wilaya na Afisa Elimu wa Mkoa wanasema Serikali imekataa wanafunzi kukariri, wasirudie, lazima waendelee. Sasa unajiuliza, hela ni zangu, mtoto ni wangu, elimu ni yangu, atakuja kuajiriwa, mimi mwenyewe ndiyo atakuja kunilinda, sasa iweje tena unanikatalia mimi mtoto kurudia shule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 nilizungumza kwa uchungu mkubwa hapa. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anamaliza hoja, hebu alitamke hili. Walilizungumza mwaka 2016 lakini hawakulitolea waraka. Tunaomba shule za private ziwe huru kukaririsha, hakuna shida pale mbona! Tatizo ni nini? Yeye alishasema kwamba huyu mtoto ni slow learner akamwacha; nilizungumza na mwaka 2016 hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wale watoto ambao ni slow learners, kama hawajifikisha kiwango fulani cha marks wasiendelee, warudie mwaka ili wasome vizuri na wazazi ndio wanaotaka wenyewe. Sasa wanawakingia nini? Hilo naomba niliongee kwa uchungu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni conflict of interest. Sasa hivi wanaoendesha shule Tanzania ni wadau wanne; Wizara ya Elimu ina shule za mazoezi, za msingi na sekondari zile za mazoezi kwenye Vyuo vya Walimu kwa hiyo nao wanamiliki shule, Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI wanamiliki shule chini ya Mkurugenzi na ni shule nyingi sana, nadhani ndiyo ziko huko kwenye Halmashauri, Sekondari na Primary. TAMONGSCO wanamiliki shule pamoja na TAPIA wamiliki wa shule binafsi, wana umoja wao, wanamiliki shule. Sasa wadau hawa wanne wanaomiliki shule, tunataka tuwe na Regulatory Body ambayo itakaa pale juu kuzisimamia hizi shule kwa sababu kuna conflict of interest.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkaguzi huyu ni mtu wa Serikali, ametoka kwa Mkurugenzi pale pale ama ametoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu; anakwenda kukagua shule ya umma, anaona kuna matundu mawili ya vyoo, anaandika ripoti pale inakwenda kwa Mkurugenzi halafu inakaa tu pale na mambo hayaendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye shule za private, akikagua akakuta kuna matundu mawili, yaani shule inafungwa siku hiyo hiyo. Ni hapo hapo, hakuna mjadala. Kwa nini wanawanyanyasa hivyo? Kwa nini vile vile na sisi tusiwe na chombo kitakachokuwa kinasimamia hizi shule? Wakaguzi wale wametoka Serikalini, wanaandika ripoti inaenda kwa Katibu Mkuu. Ndivyo hivyo hivyo tupate mtu fulani kama zilivyo mamlaka nyingine, tuwe na mamlaka itakayosimamia hizi shule zote, hao wanaomiliki shule kwa pamoja kuliko hali hii ya kuonewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kuna mmiliki mmoja wa shule alilalamika akasema Mheshimiwa Mulugo wanataka kunifungia shule. Nikauliza kuna nini? Akasema, wanafunzi walikuwa 48 darasani, maana sheria inasema angalau wanafunzi 40 mpaka 45. Wanafunzi 48 shule moja ya Kigoma, Mkaguzi ameenda pale kama mbogo, anataka kumfungia shule kwamba kuna wanafunzi 48. Nikamwambia hivi, nyuma geuka! Nenda shule ya Serikali, kuna wanafunzi 120 darasani, fungeni nayo hiyo! Jamani vitu hivi viwe realistic! Wanakuwa mpaka 150 na wenyewe wafunge! Tena angalau mambo ya madawati tumeyamaliza, maana walikuwa hata wanakaa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukienda kwenye shule za private na mmetupa miongozi ninyi wenyewe, tunafuata kila kitu, lakini jamani katika neno la ukaguzi angalau hata asilimia 10 inaweza ikapotea. Watu ni kama wana hasira fulani hivi! Naomba Mheshimiwa Waziri, hebu wasimamie jambo hili, kuna kero nyingi sana kenye shule huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Simbachawene wiki mbili zilizopita, wamiliki wa shule walikuwa Dodoma hapa walikuwa na mkutano wao wa kujadili mambo, tukamualika akawa mgeni rasmi wa kuja kufunga kile kikao. Tukamworodheshea kero zote na kodi zote ambazo tunalipa kule kwenye shule ambapo kero nyingine ni wazazi wenyewe ndiyo wanalipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kibao kinaelekeza labda Mwambao Secondary School kiko pale njia panda. Halmashauri na Mkurugenzi wanakuja wanasema lazima kilipiwe kodi, kwenye shule. Ni huduma ile! Tunalipia kupata vibao ambapo bado unaposajili shule Wizara ndiyo inakwambia kwamba lazima uwe na kibao, tunalipia kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Simbachawene, amekaa na wale wadau, ametulia akaona kwamba kweli hii ni kero. Amesema, kuanzia leo nafuta zile kodi za Halmashauri kwa ajili ya vibao. Tulimpigia makofi na kelele za shangwe na hivi tunasubiri waraka tuweze kufuta ile kodi. Kuna kodi nyingi! Kuna OSHA, property tax; jamani kuna vitu vingine ni vya ajabu kweli kule kwenye shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu yeye ndiye mdhamimi wa elimu, atusaidie. Naomba tafadhali siku nyingine wawe wanakaa na wadau wa elimu kwenye Halmashauri kule na kwenye Wilaya, waweke watu wa Serikali, watu wa TAMONGSCO na TAPIA wawe wanajadili mambo ya elimu kwa pamoja. Sio maadui, wote ni watoto wetu wa Tanzania kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ada za mitihani. Mtihani wa Taifa uko Darasa la Nne, Darasa la Saba, Form Four, Form Two na Form Six. Serikali ya Mheshimiwa Kikwete iliamua toka miaka minne iliyopita kwamba hii iwe ni ruzuku kwa wanafunzi wote kwamba wasilipie mtihani wa Taifa. Baraza la Mitihani litoe mitihani bure, lakini ilipokuja huku kwenye utekelezaji wakabagua kwamba hapana shule za private waendelee kulipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasifikiri wanakomoa shule za private pale, wala siyo hela ya mmiliki, ni hela ya mzazi mwenyewe ndiye anayechangia. Ukienda kwenye joining instruction tumeandika mzazi alipie ada ya mtihani na Waheshimiwa Wabunge asilimia 90 hapa mna watoto wenu wanasoma kule. Hiyo hela mnailipia ninyi wenyewe. Naomba ile ada ya mtihani wa Form Two na Form Four ifutwe kama zilivyofutwa kwenye shule za Serikali. Mzazi abakie kulipa ada tu, ahenyeke kwenye ada lakini siyo kwenye masuala mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona Wizara ya Afya chanjo wanatoa bure! Mbona hawabagui inapokuja kwenye chanjo za Shule za Serikali za Msingi na Sekondari! Kwa sababu ni afya ya pamoja; hata elimu wale watoto ni wa pamoja. Wale watoto wakisoma katika shule za private hawaendi kufanya kazi Uganda, hawaendi Kenya wapo Tanzania hapa hapa, ni huduma ya kawaida hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo inaniuma sana. Nashukuru hata kwenye Kamati ukurasa wa maoni Mheshimiwa Bashe, kwa sababu tu muda umekwisha, lakini wameliandika hili wanapendekeza ada ya mtihani ifutwe Form Two na Form Four na Darasa la Nne, kwenye shule za private, iwe kama ruzuku, (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije lingine ambalo naweza nikatoa machozi kuhusu vitabu. Mungu wangu! Mheshimiwa Susan Lyimo alionesha vitabu hapa lakini nami tayari nilikuwa nimeshafanya search kama Mwalimu. Ninavyo vitabu hapa, Geography for Secondary Schools, Form Three, English for Secondary; Form Four, ni hatari; na hii ni maajabu ya dunia. Ni aibu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna mambo mengine lazima tuseme. Serikali ni ya kwangu, nchi ni ya kwangu, watoto ni wa kwangu, Chama ni cha kwangu tunaposema mbili ongeza mbili, mtu mwingine akasema ni sita wakati jibu ni nne, hatuwezi kumfumbia macho.