Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Ester Michael Mmasi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa muda nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanaoifanya. Mama yangu Mheshimiwa Ndalichako, Profesa wangu mwema, kwangu katika mchango wangu hata siku moja katika Bunge hili, tofauti na ilivyochangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengine, mimi sitamwomba aache legacy, legacy ameiacha tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakumbuka katika Baraza la Mawaziri wote, mtu wa kwanza aliyekuwa na uthubu ni yeye. Alikubali kukana nafsi yake, akajitwisha msalaba wake, akafuta GPA bila kungoja makelele ya Waheshimiwa Wabunge, kwenye hili alisimama mwenyewe. Nampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, alisimama akaona kero ya wanafunzi wanaohangaika mitaani kutafuta hifadhi, alisimamia hili ndani ya miezi minane alituonesha kwa mfano, mimi pamoja na Mheshimiwa Mwenyekiti tulikuwa mashahidi. Tulikuja kwenye ufunguzi wa hostels za Chuo Kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu. Mimi ni Mbunge wa kwanza katika Bunge hili jipya kulia kwamba naomba miundombinu iliyowekwa pale UDOM ijae, tunapoteza pesa nyingi lakini Mheshimiwa Waziri hukunipa nafasi nije kulalamika mara ya pili. Jana nimeona umetoa waraka kwamba Central System Admission ifute ile process kwamba vyuo visidahili ila TCU iweze kudahili wanafunzi kwa maana ya kwamba kwa kufanya vile vyuo vingi vilikuwa vinabaki empty, tunaweka resources nyingi lakini pia hatuna matumizi nayo. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye mchango moja kwa moja katika Wizara hii muhimu. Nianze tu kumwambia Mama Ndalichako, tunafahamu na Tanzania inafahamu na sisi wadau tunafahamu kwamba changamoto kubwa katika Wizara yake imekuwa ni urejeshaji wa masuala mazima ya mikopo Elimu ya Juu. Mheshimiwa Mwenyekiti tunakiri hilo.

Mheshimiwa Mwenyikiti, pia kama utaangalia, juzi tukiwa Mei Mosi tulipata taarifa kwamba katika mwaka huu wa fedha tunaomaliza, deni ambalo limekuwa halijalipika mpaka leo ni seven trillion, deni tulilotakiwa kulirejeshwa Bodi ya Mkopo ni seven trillion lakini mpaka leo ni shilingi bilioni 400 tu zimerejeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama yangu Mheshimiwa Ndalichako, legacy ameiacha tunataka tuilinde. Naomba asikilize yafuatayo, kwamba sisi Tanzania mwaka 1999 tulituma delegation yetu kwenda nchi ya Kenya kujifunza wenzetu wanafanya nini, lakini kule tulichokiona, asilimia 40 na ni practice ambayo mpaka leo ndivyo ilivyo. Asilimia 40 ya tengeo la fedha ya Bodi ya Mkopo ndiyo Serikali ina-meet lakini asilimia 60 ni other key players, kwa maana ya kwamba ni financial sectors ndiyo ina-dish-out pesa katika kusomesha wanafuzi. Mimi siombi tufike huko, lakini angalizo lipo moja; tusipoangalia, tunaweza tukashindwa kufikisha tumaini letu kwa wananchi wetu walio wengi wanaotutegemea sisi kuweza kusaidia vijana wao waweze kwenda shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia leo tatizo kubwa ni ajira. Tulikaa hapa kwenye Miscellaneous Amendment tukasema kwamba tukate asilimia 15 ili fedha hii iweze kurejeshwa, lakini Mheshimiwa Mwenyekiti tunasahau kwamba tulisema tukate asilimia 15, wakati tunaangalia entry qualification, eligibility qualifications ya mtu ambaye anaweza kupata mkopo, cha kwanza tuliangalia uhitaji. Kama ni uhitaji, ni obvious kwamba wanafunzi hawa wametoka kwenye familia maskini. Sasa kama wametoka kwenye familia masikini na ajira hakuna, tunategemea hii asilimia 15 tunam-task mwanafunzi au mzazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tupate muda tutafakari upya. Asilimia 15 ni rahisi sana kuwekwa kwenye majarida yetu, ni rahisi sana kuja kuijengea hoja Bungeni, lakini watakaoteseka ni wananchi wetu wa vijijini wasiokuwa na uwezo. Kama hivi ndivyo tupate muda tutafakari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa nakuomba, unao wenzako hapo, kila siku wanawasilisha ripoti zao na kusema ni kwa namna gani wanaenzi masuala mazima ya Sera ya Ajira, lakini vitu havikutani. Hatuoni direct linkages. Wewe ni shahidi, tulikaa hapa juzi, mama huyu Mheshimiwa Mama Kairuki, Waziri wa Utumishi, alituambia kwamba ameahidi kutoa ajira 58,000 nchini Tanzania lakini absorption capacity bado haikidhi tija. Wanafunzi wanaomaliza ni 250,000 lakini unaona absorption capacity, ajira ni 58,000 kwa mwaka. Hatuwezi kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Wizara Ardhi, inastawi, inashamiri, ni vema tumempata kiongozi mahiri, ni sawa; lakini pia ukiangalia vijana wanaomaliza Chuo cha Ardhi wanakosa kazi kupitia hata sheria tunazoleta Bungeni. Tulileta hapa Valuation and Valuer Registration Act ambayo ni sheria ya masuala mazima ya wapima na wathamini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi tuliyopewa na Mheshimiwa Waziri ni kwamba Wizara yake itasajili makampuni 57 ambayo yataingia kwenye suala zima la kupima ardhi. Tukamwuliza hapa, akasema pia vijana kupitia zile three categories ambapo kuna full valuer na temporary registration valuer walisema kwamba hata vijana graduate wanaruhusiwa kuingia na kuweza kufanya kazi za uthamini katika muktadha wa masuala mazima ya ardhi. Katika makampuni 57 yaliyoingia na kusajiliwa hakuna hata kampuni moja ya graduate wa nchi hii, mzawa wa nchi hii aliyeweza kuingia na kuweza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, masuala ya ajira bado yamekuwa ni changamoto. Ninyi ni mashahidi kwamba vijana hawa wanahangaika, vijana hawa wanatulilia, tutawapeleka wapi? Mwaka 2020 unafika, tutajibu nini? Ilani imeeleza, Sera ya Ajira inaeleza, lakini vijana wamelia kwa kila sauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, akae na Wizara nyingine wamsaidie tuweze ku-link na kuweza kuzalisha ajira. Leo tunavyoongea, ukuaji wa Sekta ya TEHAMA ni mkubwa, lakini wanafunzi wa DIT wanatumika wapi? Hawatumiki! Angalieni mifumo inayotumika katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye financial sector, 40 percent ya kazi za ICT inafanyika nchi ya India na Kenya. Watanzania hawashiriki katika muktadha mzima na masuala ya ajira. Legacy tutailinda pale ambapo tutaweza kufanikiwa kwenye mtihani huu wa urejeshaji wa mkopo wa Bodi. Sisi kutunga sheria ngumu bado siyo jibu kwa sababu bado tunampelekea mzigo mkulima, fukara na masikini kule kijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo masuala mazima ambayo sisi kwetu bado tunahuzunika sana. Sisi kama akinamama, wewe ni shahidi, tumekuwa na kesi nyingi sana kwenye masuala mazima ya ngono katika Vyuo Vikuu vya Tanzania yetu. Leo ngono inatumika kama kipimo na kigezo cha ufaulu katika shule zetu ama vyuo vyetu nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mama Ndalichako ni shahidi, tumekuwa na kesi nyingi. Atakumbuka juzi hapa, Mhadhiri wa Chuo cha NIT, huyu anaitwa Bwana Samsom Mahimbo, alidiriki kumshawishi mwanafunzi na TAKUKURU walimkamata kwamba ili afaulu mtihani wake wa supplementary ni lazima atoe rushwa ya ngono.

Mheshimiwa mwenyekiti, sisi ni wazazi, matumbo yetu yanatuuma. Hatuwezi kuangalia dhambi hii! Hatuwezi kuangalia udhalilishaji wa wanafunzi wetu. Imesemwa hapa na waliowasilisha kwenye ripoti zao hapo mbele, imesemwa kabisa, ukimsomesha mwanamke umesomesha Taifa. Tumechoka kuona kudhalilishwa kwa watoto wetu mashuleni. Walimu hawa wanachukuliwa hatua gan? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri akija aniambie Bw. Samson Mahimbo alichukuliwa hatua gani? Asisahau, aniambie Bw. Kelvin Njunwa, ni Institute of Accounts, Dar es Salaam alichukuliwa hatua gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu, kaka yangu mpendwa Mheshimiwa Simbachawene alienda hapa Hombolo kwenye kesi kama tatu alienda na ku-rule out za masuala ya ngono. Hawa watu wanachukuliwa hatua gani? Hatuwezi kusema tunatengeneza rasilimali ya nchi hii kwa kutumia vigezo ambavyo havina ushindani. Hatuwezi kutengeneza rasilimali ya nchi kwa kuwa na watu ambao hatujielewi wala hatujithamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda kwenye uchumi wa kati, tunaandaaje rasilimali watu ya nchi yetu ya Tanzania? Tunaenda kwenye uchumi wa viwanda, tumejiandaaje kuingia kwenye uchumi wa viwanda endapo utafaulu mtoto mwanafunzi wa Chuo Kikuu unapimwa kwa utoaji wa ngono? Tutaenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni mama, amezaa, Wizara yake inasimamiwa na akinamama, Semakafu ni activist mzuri, ananijua na ananisikia. Semakafu Kamishna wake ni activist mzuri; namwomba alipo atusaidie. Tutaangalia haya mpaka lini? Tumechoka, macho yetu yanaumia, nafsi zetu zinauma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu. Nilikuja kwenye Bunge lako hili Tukufu, niliongelea sasa wanafunzi wa Chuo cha NIT, nikaomba unisaidie kwamba tumejipanga kwenda kwenye uchumi wa kati, tumejipanga ku-promote Tourism Sector yetu kwa kufufua usafiri wa anga, well and good. Tume- invest a lot kununua ndege, well and good, lakini tumejipangaje kuandaa rasilimali watu katika muktadha mzima huu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu hata maandiko ya dini wanasema atakayeshindwa kushukuru, huyo ni mnyang’anyi. Namshukuru sana, nilikwenda nikamwomba kwamba watoto hawa wa NIT waruhusiwe kufanya mitihani. Milioni kumi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.