Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nitoe pole zangu za dhati kwa wananchi wote wa Tanzania na wana wa Arusha kwa msiba mkubwa uliowapata kwa watoto wetu. Pia naomba nipongeze hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitangulize maneno haya, kwa macho ya kawaida tunawaona walimu wanayo furaha, lakini katika mioyo yao walimu hawa wanaandamana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wetu wa elimu ni mfumo ambao hauna tija kwa maslahi ya Taifa hili. Kumekuwa na mitaala mbadala kila Waziri anapokuwa kwenye sekta hiyo. Kila Waziri anayepewa Wizara anakuja na mitaala yake. Sasa sijui Bodi hiyo ya Elimu ina kazi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hatuwezi kupata elimu bora bila kuwa na afya, maji na lishe bora lakini pia na miundombinu bora ya elimu. Ni ukweli usiopingika kwamba tuna uhaba wa walimu, nyumba za walimu, matundu ya vyoo lakini pia shule nyingi za sekondari za kata hazina maabara na mabweni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kutaratibu kwa wanafunzi wa shule za kata kwenda kupanga kwenye nyumba za watu binafsi hususan vyumba vinavyoitwa geto. Unawezaje kupata elimu bora kwa kumweka mtoto ambaye ana umri wa miaka chini ya 13 au 18 amepanga, anaishi mwenyewe, anaishi group na vijana wa kiume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wenyewe ni mashahidi watoto hawa ukweli ni kwamba wako kwenye foolish age, unatarajia nini? Unatarajia “A” na zero ngapi? Mazingira haya yaboreshwe, kama Serikali ilivyoamua kujenga shule za kata wahakikishe mabweni yanakamilishwa ili wanafunzi wetu wapate elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo la uhaba wa nyumba za walimu. Kwa macho yangu nilishawahi kushuhudia walimu wanakaa kwenye nyumba za udongo. Nyumba yenye room tatu wanakaa walimu sita mpaka tisa, wakike watatu na wanaume sita. Hebu niambieni walimu hawa wakiingia darasani wanafundisha nini kama siyo wanawaza mazingira yale mabovu ya makazi yao na mishahara midogo na kutokulipwa pesa zao za sitahiki zao halali lakini Waziri akija hapa akiulizwa swali anasema wamelipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache kudanganyana, hawa ni Watanzania, tumewapa kazi hii. Sisi zote humu ndani ni kazi ya walimu, lakini leo hii wenzetu wa upande wa pili mnafanya siasa juu ya afya na akili za Watanzania. Kumekuwa na Taifa la vuguvugu si Taifa la watu wasomi kwa sababu kila mtu ana yake kichwani akija ni kubadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye viwango vya ufaulu. Hebu tuelezane ukweli wa mambo, mwanafunzi kutoka darasa la kwanza mpaka la saba ameshindwa kupata marks 100, unampeleka form one kufanya nini? Ana tofauti gani na baba yake anayefuga ng’ombe na yeye jioni akirudi anakunya maziwa, maana hata kusoma hajui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuanze na form one mpaka form four mmepandisha daraja la ufaulu mnasema division four mpaka point 35, mmelenga kufanya nini? Mmeipeleka huko ya nini? Tunafuga watu ambao watatulemea katika Taifa hili. Tunalia na ajira za vijana, mnasema East African Community haiajiri vijana wa Tanzania, unaajirije Mtanzania mwenye vyeti kama hivi? Tumebaki kuwa walalamikaji, tumebaki kufanya siasa kwenye maisha ya Watanzania, kila kitu ndiyoooo, mpaka lini, hata kwenye elimu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa ambalo watu wake hawajali elimu hakuna uchumi, maendeleo na hakuna afya. Madaktari hawa hawa leo mnakuja na uhakiki wa vyeti fake nani kawatengeneza kama sio ninyi? Alikuja Mungai nikiwa darasa la pili alifuta michezo, leo mnalia na michezo? Kwa nini mnakuwa mnakana vivuli vyenu, mnakimbia vivuli, Serikali inakimbia kivuli chake. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naombeni niende kwenye elimu ya mtoto wa kike. Tunaomba tuelimishe watoto wa kike, mtoto wa kike ni hazina. Angalieni akina mama ambao hawajasoma, kila mwanaume aliyesimama hapa mbele yake kuna maendeleo ni mwanamke amemshauri vizuri. Je, hawa wanawake wakisoma, natumai asilimia ya maendeleo itaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iache utaratibu wa kutuletea elimu ya vuguvugu. Kulikuwa na mpango wa vodafaster, mmetuzalishia watoto wengi kupitia hao walimu wa vodafaster leo hii mnasema watoto hawa ni mbulula na ni vilaza, ukilaza huu mmetengeneza ninyi Serikali. Nani kautengeneza kama sio ninyi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vyeti fake, wadau wakubwa wa kuzalisha hivi vyeti feki ni Baraza la Mitihani, hizi namba fake ni Baraza linagawa. Anzeni kule msianze na wale ambao siyo wahusika, alipataje namba ya mtihani, nani aliyemuandikia zile marks na nani aliyempa kile cheti bandia ambacho hakina alama ya twiga, ni watu wa Baraza. Mheshimiwa Waziri usimung’unye maneno ulikuwa mama mzuri sana lakini wamekuweka kwenye mtego na wamekuweka mtu kati kwenye siasa, acha siasa kwenye elimu ya Watanzania. Tunahitaji Watanzania wenye elimu na afya ya kutosha kwa sababu madaktari wanatokana na elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema hata wale walimu wa UPE waliofukuzwa Serikali imewatendea dhambi. Serikali wenyewe ndiyo iliwaajiri wale walimu, leo unasema sio walimu, wameishia ngazi ya diploma, wametumikia Taifa hili na walifundisha vizuri, kuna watu waliotokana na walimu hawa wa UPE, leo unasema hawa walimu sio? Muogopeni Mungu mkawalipe wale watu na wengine wameshastaafu wapate stahiki zao. Msitujengee Taifa linalobeba laana kwa sababu utakapokuwa umejiwekeza kwenye laana na uhakikishe kwamba laana hiyo itakuwa inakutafuna wewe. Hatuhitaji laana ya walimu hao, walipwe pesa zao. Ahsante.