Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitoe pole kwa Taifa kwa kupoteza wapiganaji hawa wawili, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wa zamani Mheshimiwa Said Mwambungu pamoja na Mzee Paul Sozigwa. Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mchango wangu katika Wizara hii na kwa kipekee kabisa naomba nianze na suala la Chuo cha Ufundi Lushoto. Juzi hapa Mheshimiwa Shekilindi alikuwa na swali linalohusu VETA, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati analijibu nadhani hakuwa anaifahamu Lushoto vizuri, sasa naomba kidogo nimpitishe kwenye jiografia aitambue vizuri Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lushoto ni Wilaya ambayo hali ya hewa ni kama hivi tulivyo humu Bungeni, siku zote tupo hivi hakuna joto, kwa hiyo, tunazaana sana. Population ya Wilaya ya Lushoto ni karibia watu 700,000, tunazo shule za sekondari 85, ikiwemo Kifungiro, St. Mary’s Mazinde Juu, Kongei, hizi ni zile ambazo zinafanya vizuri zaidi. Kwa mazingira hayo tunahitaji kuwa na vyuo vya ufundi. Bahati nzuri huko nyuma tulikuwa na Chuo cha Ufundi cha Kanisa KKKT cha Magamba Trade, baada ya wenye chuo kubadilisha matumizi sasa hivi kimekuwa ni Chuo Kikuu cha SEKOMU hivyo, hakuna chuo cha ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika kata ya Lushoto Mjini pale tulikuwa na karakana ya RRM - Rural Roads Maintanance zile za zamani zile, hapa palikuwa na mitambo mpaka sasa hivi ipo na yale majengo yanamilikiwa na Halmashauri na pana mitambo mbalimbali ya kufanya ufundi selemala, kufua vyuma na kadhalika.

Kwa hiyo, tunapozungumza suala la VETA Lushoto hatuna maana kwamba tukatafute mapori. Zipo karakana ambazo tayari zipo kimsingi ni namna tu ya kuziboresha. Pia KKKT hawa wana shule ya ufundi ambayo ni kwa watu wenye mahitaji maalum, hata Mheshimiwa Marehemu Dkt. Elly Marco Macha amesoma katika shule hii inaitwa Irente, pale pana chuo cha ufundi cha watu wenye mahitaji maalum.

Kwa hiyo, ninakuomba Mheshimiwa Waziri ama Naibu Waziri, ujipe nafasi ya kuja Lushoto uweze kuona haya mambo, tunapolizunguza VETA tuna maana kwamba population iliyopo ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tukisema tuende mpaka Tanga bado sisi wenyewe katika ndiyo Mkoa wa Tanga tunaongoza kuwa na sekondari nyingi, eneo lile peke yake linatosha kuwa na Chuo cha VETA na maeneo yapo, tupo tayari kukupa majengo ambayo yapo tayari. siyo ya kuanza kujenga.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uchapishaji wa vitabu. Serikali ilipoamua kuifuta Bodi ya EMAC tulikosea. Kama kulikuwa na makosa ilipaswa turekebishe, lakini kuifuta na hili jukumu kuipa Taasisi ya Elimu pekee ni suala ambalo kwa kweli linakinzana hata na kauli mbiu hii ya Serikali ya viwanda. Tunavyozungumza sasa yapo makampuni ya sekta binafsi yalikuwa yanafanya kazi hii ya uchapishaji, kampuni za kizalendo wapo kampuni ya Ujuzi, wapo Mkuki na Nyota, Mture, Education Book Publisher, E&D pamoja na AIDAN ambapo mwanzoni walikuwa wameungana na Macmillan. Haya makampuni sasa hivi hayawezi yakafanya biashara kwa sababu Serikali imechukua ili ifanye yenyewe biashara, Serikali imeingia kwenye uchapishaji na matokeo ndiyo tunayoyaona hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makosa haya kwenye kitabu cha jiografia pekee cha form four yapo zaidi ya makosa 15, kwenye kitabu cha form three yapo zaidi ya makosa 18, humu kwenye I Learn English Language ndiyo usiseme yako mengi, hata neno below linaandiwa double L, ni jambo la kusikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaitaka Serikali kwamba bado hatujakosea sana kwa sababu mambo haya yamefanyika humu Bungeni tuone namna gani tunaweza tukairejesha tena ile bodi ya EMAC ambayo inaweza ikaja kufanya hii kazi ya uhakiki wa vitabu. Pia lazima tuangalie kwamba hii sekta binafsi itafanya wapi biashara. Tunazungumza sasa hivi kiswahili kinakua katika Afrika ni lugha ya pili kwa ukubwa, kama kiswahili kinakua tunatarajia kwamba Serikali peke yake ndiyo itachapisha hivi vitabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni wakati maufaka kabisa kuwajengea uwezo ili waweze kushindana na hawa akina Oxford University Press, washindane na kina Pearsons, washindane na kina Longhorn, kwa sababu haya ni makampuni makubwa duniani na yapo hapa Tanzania wanachapa vitabu, tena wao mara nyingi wanachapa nje ndiyo maana hata vitabu vinakuwa bei nafuu. Sisi gharama za uchapishaji kwa hapa ndani peke yake zitakuwa ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri hili jambo kama lilifanyika kwa mihemuko ya kisiasa hebu sasa kaa na hawa wadau, hawa ni Watanzania wenzetu, tujaribu kupata mbinu muafaka ambazo zitakuja kutatua tatizo la elimu ya hawa watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la ukarabati wa shule kongwe. Nimeangalia katika kitabu sijua labda nimeangalia kwa haraka lakini sikuona sekondari kongwe za Tabora Boys na Tabora Girls. Mheshimiwa Waziri umesoma Tabora Girls, na mimi nimesoma Tabora Boys ni lazima tukumbuke tulikotoka. Naomba uangalie namna ya kuboresha mazingira ya sekondari hizi. Tulikuja ofisini kwako na timu ya Elites ya watu wa Tabora Boys, tukionesha kwamba tunaweza kuunga mkono jitihada za Serikali katika hili na ukatuambia kuna nia njema, sasa tunataka nia njema hiyo iende hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, isiishie hapo iende na shule ya Malangali, Mimi nilipotoka Tabora Boys nilikwenda Malangali nayo sijaiona humu. Mheshimiwa Waziri mimi nimesoma shule za zamani ndiyo maana siyo mtu wa mchezo mchezo, naomba shule hizi tuzifufue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika elimu, Chuo Maalum cha Ualimu cha Patandi pia humu sijakiona. Tanga Galanos sijaiona lakini Korogwe Girls pia sijaiona, Korogwe TTC sijaiona. naomba sana Mheshimiwa Waziri, hivi pia ziingie katika mfumo huu na ninadhani ulishaniambia kwamba zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nizungumzie vifaa vya maabara. Hapa tumeona kwamba mmesambaza vifaa vya maabara katika maeneo mbalimbali, tunashukuru kwa hivyo ambavyo tumevipata. Katika Halmashauri ya Lushoto tumepata katika shule tisa pekee. Kama nilivyokuambia tukizungumza Lushoto kama Halmashauri tuna sekondari 65, tukichanganya na Bumbuli ambayo ina Halmashauri yake ndiyo zinafika 85. Kwa hiyo, utaona kabisa kwamba kati ya shule 65 zikipata tisa ina maana bado shule nyingi zimekosa hivi vifaa.

Kwa hiyo, nikusihi sana utuangalie kwa jicho hilo kwamba tumejitahidi katika ujenzi wa hizi shule za sekondari, zipo kata Mheshimiwa Waziri kuna kata moja ina vijiji vinne kila kijiji kina sekondari. Utaona kabisa kwamba huu muitikio ni mkubwa na maabara hizi tumezijenga kwa nguvu za wananchi kwa kiasi kikubwa, tupo tu katika hatua za usafi tunaomba sasa mtuunge mkono katika usafi pamoja na vifaa. Naomba sana utuangalie katika mukhtadha huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala zima la mitaala kwamba mitaala iangaliwe ili iweze kwenda na mahitaji ya Tanzania ya sasa. Tunagundua kwamba sisi angalau tuliobahatika kwenye mitaala ile ya Mwalimu Nyerere ndiyo maana unakuta hata mtu akimaliza darasa la saba anaweza akajiongeza mwenyewe. Lakini tumegundua kwamba sasa hivi, wanafunzi wa sasa anamaliza Chuo Kikuu bado hata kuandika barua au hata yeye mwenyewe kutafuta namna ya kujiwezesha inashindikana. Kwa hiyo, hapa tatizo moja kwa moja inaonekana kwamba ni mitaala yetu haimuandai mwanafunzi ili aje kuwa nani.

Ninaomba sana tuachane na hii dhana ya wanafunzi kumaliza degree halafu kutembea na bahasha mitaani. Tutengeneze mitaala ambayo itakuwa ni shirikishi na inaeleweka kwamba atakapomaliza chuo basi anaweza mwenyewe akajiongeza kwa namna yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tumeona mlundikano mkubwa huu wa wanafunzi wa masomo ya sanaa, sasa watakuwa hawana ajira, ndiyo anachouliza Mheshimiwa Mlinga waende wapi, kosa lao ni nini, kwa sababu Serikali yenyewe ndiyo iliyofanya udahili leo haiwezi kuwaajiri, ni lazima tutafute vitu mbadala. Pia ni lazima pia tutumie fursa yakuwepo katika hili Shirikisho la Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.