Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa nimshukuru sana Mungu kwa ajili ya kutujalia afya sisi wote tuliomo humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na pole kwa wanafunzi waliopoteza maisha kule Arusha na nimpe pole mmiliki wa shule ya Lucky Vincent. Pia niwashukuru sana wale Wamarekani waliokuja kuchukua wale majeruhi watatu na kuwapeleka Marekani kwa ajili ya matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa ku- declare interest, mimi ni mdau wa shule binafsi. Nimwombe sana Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, hivi navyozungumza magari mengi ya shule katika kila mkoa yanakamatwa na kuwekwa yard. Gari asubuhi limetoka na wanafunzi nyumbani, linapeleka wanafunzi shule, wakienda kushusha watoto magari yale yanachukuliwa yanapelekwa yard kwamba gari hili bovu, tumepata pressure kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zitafungwa ndani ya wiki mbili kuanzia sasa. Tunaomba wamiliki hawa wa shule binafsi wapewe nafasi ili wakati ule wa mwezi wa saba kipindi shule zikiwa likizo hayo mapungufu yaliyoko kwenye hayo magari yakafanyiwe kazi lakini wawaache watoto sasa hivi waendelee na shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaumiza kuona kwamba tunafanya vitu kwa kukurupuka. Hawa ma-traffic walikuwepo barabarani miaka yote wakati hawa watoto wanaenda shuleni na hayo magari. Leo imetokea ile ajali imekuwa mateso kwa wamiliki wengine. Mheshimiwa Mwigulu tusaidie kwenye hili, wasitishe hilo zoezi. Shule zitakapofungwa mwezi huu wa Saba magari yatarekebishwa halafu ndiyo michakato mengine iendelee. Hilo ni ombi kwa Mheshimiwa Mwigulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la hivi vitabu. Mimi nina maswali kama matano na Mheshimiwa Profesa Ndalichako atakapokuja hapa tunaomba atusaidie. Je, ni nakala ngapi za vitabu vya darasa la kwanza, la pili na la tatu vilivyokwishasambazwa. Pili, vitabu vimetayarishwa kwa gharama za walipa kodi Watanzania ambavyo ni vibovu, nani anawajibika kwenye hili? Fedha kiasi gani zimetumika kuandika, kuchapisha na kusambaza vitabu hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitabu hivi vilitumia muda wa miaka mitatu kuviandaa, tunasema vitabu hivi sasa havifai viondoke sokoni, je, ni muda gani zaidi utatumika mpaka tupate vitabu mbadala wa hivi? Sisi wamiliki wa shule binafsi, mfano mimi nimenunua vitabu vya shilingi milioni 18, najiuliza nalipwa na nani gharama zile? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naongea na Mheshimiwa Mulugo amenunua vitabu zaidi ya shilingi milioni 30, nani analipa gharama hizo? Wakati hawa watu wa TET wanaandaa huu mtaala, tuliomba kwamba wawashirikishe watu wengine mbalimbali kwa maana hata kutoka kwenye sekta binafsi ili waweze kupata inputs, wakajifungia vyumbani, wakakataa ushauri, leo wamekuja na vitu vibovu, nani anawajibika? Kwenye vitabu nimemaliza, ninavyo hapa ni upuuzi mtupu unaendelea hapa. Hata Kiingereza cha mtoto wa English Medium wa darasa la tatu hawezi kutunga vitabu vya namna hii. Sijui ni wataalam gani walitumika kutunga hivi vitabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya vitabu naomba nielekee kwenye suala zima la kodi kwenye shule binafsi. Waheshimiwa Wabunge wenzangu, naomba leo mnielewe, wakati mmiliki wa shule binafsi anaposimama na kuzungumza habari ya kodi 15 tunazizungumza, niliwahi kuzisoma hapa Bungeni mkashika vichwa, hatujitetei sisi maana kodi hizi mnazilipa ninyi ambao watoto wenu wanasoma kwenye hizo shule, tunawatetea akinamama ntilie na wananchi wa Tanzania kwa ujumla wao. Maana kama kwenye shule ada ingekuwa Sh.200,000 inakuwa Sh.400,000 kwa ajii ya hizi kodi na anayezilipa ni wewe mwananchi sio mimi mwenye shule, mimi ni wakala tu wa kuzikusanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaposimama hapa, ile negative attitude kupitia kwa wamiliki wa shule tuliopo humu Bungeni iondoke kwamba hawa watu wamekuja kutetea maslahi yao binafsi. After all kipele kinachokuwasha wewe mgongoni mwako unakijua wewe mwenyewe na maumivu yake, sasa nisiposema mimi atasema nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imagine majengo ya shule yalivyo makubwa unatakiwa ulipie property tax. Sheria ya Elimu ya mwaka 1977 iliomba watu binafsi waweze kuisaidia Serikali kutoa elimu kwa nchi hii. Sheria ya Elimu ya mwaka 1977 inatutambua sisi kama watoa huduma, Wizara ya Fedha inatutambua sisi kama wafanyabiashara, tushike lipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya nchi yetu inasimamiwa na Wizara zaidi ya moja, Wizara ya Elimu, TAMISEMI, Wizara ya Fedha, Wizara ya Afya, Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi yaani nazungumzia SUMATRA huko kwenye mabasi na kadhalika, kwa hiyo, kila mtu anakupiga kivyake. Kusema ule ukweli it is like a crime for you owning a school in this country, wakati Uganda na Kenya mtu anayetaka kuanzisha shule anasaidiwa na Serikali almost 60%. Leo sisi watu wamejitoa, halafu haya mambo yangekuwa yamewekwa bayana wakati unatafuta usajili wa shule kwamba kuna kodi hizi na hizi, these are the criteria hakuna mtu angeanzisha shule kwenye hii nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna dirisha la wawekezaji kusamehewa kodi wanaokuja kuchukua Tanzanite zetu, ardhi zetu, malighafi mbalimbali lakini mwekezaji Mtanzania ambaye yeye ndiye ana uchungu na Watanzania wenzake, anayewekeza kwenye elimu ya nchi hii hana msamaha wa kodi hata kwenye vitu tu kama cement, bati na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya wenye shule 100 ukiwapima wote wana pressure na sukari labda wasiokuwa na maradhi haya ni wawili. Ni tabu tupu. Kama Serikali tu yenyewe inashindwa kutengeneza miundombinu mizuri na kutoa elimu bora kwa watu wake sembuse mtu mmoja? Ifike mahali Serikali itambue juhudi zinazowekwa kwenye hizi shule na watu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nimwombe Mheshimiwa Profesa Ndalichako, ilikuja barua kutoka kwa Kamishna wa Elimu kwamba hakuna mwanafunzi kukaririshwa darasa. Naomba nisome effect ya hilo suala la kutokumkaririsha mtoto darasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, matokeo ya mwaka jana na mwaka juzi ya kidato cha nne, wanafunzi waliopata division one mpaka division three ni 53,000. Mwaka 2015 wanafunzi waliopata division four na zero 354,000. Wanafunzi waliopata division one mpaka three mwaka 2016 ni 54,000 na wanafunzi 347,000 waliopata division four na zero. Yet mnatuambia hakuna kukaririshwa darasa, hivi tunawaandaa watoto wamalize darasa la saba na form four au tunawaandaa ili elimu wanayoisoma iwasaidie? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, huko kwetu kwenye shule za binafsi ni mapatano ya mzazi na mwenye shule, kila shule ina joining instruction kwamba mtoto wako asipofikia hii marks kwa kweli hawezi kwenda mbele na mzazi ana sign na tunakubaliana. Imetokea tu mzazi mmoja amekwenda kulalamika huko Wizarani ndiyo inakuja kuandikwa waraka wa namna hii, this is not fair!

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu tunashangaa ufaulu ambao ni mbovu kiasi hiki, watoto wanaofaulu division one mpaka three ni 54,000 kwenye malaki ya wanafunzi unatoa waraka kama huu. Naomba Wizara ya Elimu itazame hivi vitu. Wakati mwingine wanapotoa maamuzi ya namna hii watushirikishe. Ninayezungumza ni Mwenyekiti wa wadau wa shule binafsi Tanzania niko humu humu ndani. Tunaomba tushirikishane hivi vitu vingine maana tunaumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna wanafunzi zaidi ya laki saba kwenye shule za binafsi Tanzania. Tumeajiri zaidi ya watu 45,000 Walimu na wasio walimu, kuna matrons, madereva, wapishi na kuna kila kitu. Tunachangia uchumi wa nchi hii kwa kununua vyakula na mahitaji mengine, sisi sio watu wadogo, tunaomba tutambulike kwenye hii nchi kwamba tunasomesha Watanzania wenzetu. Hakuna Mchina atakayekuja kujenga shule hapa, hakuna Mwingereza atakayekuja kujenga shule Tanzania ili Watanzania wasome. Wakiwasaidia kwenye elimu watawatawala namna gani? Sisi ndiyo wenye uchungu na Tanzania na ndiyo maana tumewekeza kwenye elimu. Kwa hiyo, tunaomba juhudi zetu zitambulike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunacheza na referee mchezaji. Watoa elimu nchi hii ni TAMISEMI na watu wa shule binafsi lakini sisi tumekuwa watu wa kupokea maelekezo kutoka TAMISEMI, kutoka Wizara ya Elimu, tunaletewa tu hatushirikishwi. Kuwe na chombo maalum ambacho kita-regulate elimu ya nchi hii ili kuwe na fair play kati ya watoa elimu. Tuanzishe chombo kinaitwa Tanzania Education and Training Regulatory Authority ili kama kuna shule ya msingi ya Serikali haina choo ifungwe kama inavyofungwa shule ya mtu binafsi ambayo haina choo.