Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka niwakumbushe kidogo hili suala la vitabu kuonekana vina makosa humu Bungeni siyo jambo geni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Susan Lyimo alisema hapa kwamba hivi vitabu vina makosa na Mheshimiwa Simbachawene alitoka kule kuja kuangalia na akajibu kwa mbwembwe na kejeli kwamba anachokisema Mheshimiwa Susan Lyimo siyo kweli. Sasa Mwenyezi Mungu kila siku yupo na wanadamu, nashukuru tu kwamba tumeona, kila mtu ameona ama amesikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Elimu, naomba uchukue hatua stahiki, tumepoteza pesa, lakini pia tumewapoteza watoto kwa maana wamepewa knowledge ambayo siyo sahihi. Wakati sijaingia Bungeni nilikuwa namsikia sana Mheshimiwa Mbatia anazungumzia mambo ya mtaala na vitabu vina mapungufu, lakini tumechukua hatua gani naona kila siku hali inazidi kuwa mbaya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Elimu nafikiri una jukumu kubwa la kuangalia na inawezekana kwenye somo la Sayansi labda alipelekwa mwalimu wa historia maana hivyo vitu vipo, watu wanaangalia zaidi mshiko (kipato) kuliko kuangalia maslahi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Vyuo vya Ualimu mwaka jana nililizungumzia na leo ninalizungumzia. Mradi wa ICT implementation katika Teachers Education; server zote sasa hivi kwenye Vyuo vya Ualimu ambako mradi ule umepita hazifanyi kazi, lakini ukifungua kitabu cha hotuba ya Waziri anazungumza zaidi mfano, hata pale ukurasa wa 27 anazungumza suala la kuhakikisha TEHAMA inafundishwa, kuhakikisha walimu wanaandaliwa na TEHAMA na vitu kama hivyo. Nikuhakikishie tuma watu wako ama nenda mwenyewe kwenye Vyuo vya Ualimu vingi kama siyo vyote hakuna computer na kama zipo ni mbovu na pia server hazifanyi kazi na wala hawapewi GB wala kitu gani, tunategemea hiyo TEHAMA itaendaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa ya Kamati tuna upungufu wa vyumba vya madarasa 158,674; lakini kwenye bajeti mwaka ujao wa fedha tumetenga kujenga vyumba vya madarasa 2000 tu kama pesa itapatikana. Kwa maana hiyo, kwa mahitaji haya 158,674 kila mwaka tukijenga vyumba vya madarasa 2000 maana yake tutatumia miaka 79 ili tuweze kukamilisha. Nafikiri inatakiwa kuwe na mkakati wa makusudi, madawati tunajua yalipatikana yaliyo mengi mengine yapo nje yanalowa mvua yanaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshauri Waziri ili kusudi tuboreshe elimu yetu na watoto wetu wakae katika vyumba vya madarasa kunahitaji pia mkakati wa makusudi. Wakati wa kuhitimisha Mheshimiwa Waziri naomba anijibu maswali yangu haya rahisi, tunaposema quality education Tanzania tunamaanisha nini? Pia napenda kujua falsafa yetu ya elimu sasa hivi ni nini? Bado ni ile elimu ya ujamaa na kujitegemea ama kuna kitu kingine? Kama ndivyo basi tujue mitaala ambayo tunaitumia kweli inawafanya watoto wetu kwenda kwenye kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Wakaguzi ama sasa hivi wanaitwa Wadhibiti Ubora. Mheshimiwa Waziri nikuombe kile kitengo kipo chini yako, Wizarani kwako, naomba ukipe kipaumbele kwa umuhimu wake, kwa sababu bila ukaguzi kwenye elimu ni sawa na hakuna. Maana yake hawa Wadhibiti Ubora wa elimu ndiyo CAG kwenye elimu, ndiyo wanaangalia kila kitu na kujua kuna matatizo gani. Inawezekana hata hili suala la vitabu leo tusingekuwa tunaliongelea hapa kama wangekuwa wanafanya kazi zao vizuri.