Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusimamia Sera za Elimu hapa nchini. Mheshimiwa Waziri nianze kwa kukuomba kukipatia fedha za maendeleo Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ili kiweze kukamilisha ujenzi wa jengo la ghorofa lililoanza kujengwa miaka minne iliyopita. Mheshimiwa Waziri Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere zamani Kivukoni ni chuo kinachobeba historia kubwa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni chuo cha kwanza kujengwa na Watanzania wenyewe tena kabla ya kupata uhuru. Chuo kile kimesaidia sana kuwaandaa viongozi wa nchi jirani kama vile Jocob Zuma, Rais wa Afrika Kusini. Mheshimimiwa Waziri jambo lingine ni kuhusu kuzisimamia na kuziangalia kwa karibu mno shule binafsi. Utaratibu wa shule binafsi ni mzuri sana tena sana, umesaidia kwa kiwango kikubwa mno kupungua kwa watoto waliokuwa wanakwenda nchi jirani kutafuta elimu bora. Hivyo umuhimu wake ni mkubwa mno, lakini kuna haja ya kuziangalia mara mbili zaidi hususani katika mambo muhimu mawili; kwanza ni kuhusu suala la ada kuwa kubwa mno na pili, huduma ya chakula kinachotolewa shuleni; kwa nini shule nyingi za binafsi hususani za Dar es Salaam hazitoi chakula kwa wanafunzi hasa zile shule za kutwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa watoto wadogo kuchukua pesa kwa wazazi wao ili wanunue chakula si mzuri hata kidogo na unapelekea watoto wetu kula vyakula visivyoeleweka, lakini pia ni chanzo cha kuwafundisha watoto tabia mbaya ya kupenda pesa wangali wadogo. Mheshimiwa Waziri naomba Wizara yako itoe maelekezo kwa shule zote binafsi zile za kutwa kuhakikisha zinawapatia chakula watoto wadogo wawapo shuleni badala ya kuwaambia wazazi watoe pesa kuwapatia watoto wakanunue wenyewe chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni uchache wa vyuo vya elimu ya juu na ufundi katika Mkoa wetu wa Lindi. Mkoa wetu wa Lindi una vyuo viwili tu ambavyo ni VETA Lindi na Chuo cha Utabibu. Naomba Serikali ilete vyuo zaidi Lindi kwani ardhi ya kujenga vyuo ipo na usafiri hivi sasa umeimarika hivyo kuharakisha mawasiliano. Nashukuru sana.