Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nawatakia Mawaziri kila kheri katika kusimamia sera, sheria na kanuni za sekta hii muhimu ya elimu. Nina mambo muhimu katika maeneo matano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, uboreshwaji wa miundombinu katika Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Sumve. Shule hii Serikali imeisahau kama vile ni private secondary school. Shule hii inachukua wanafunzi toka maeneo mbalimbali ya nchi yetu wa kidato cha tano, lakini haina walimu wa kutosha, vitanda, magodoro hayafanani na jina la shule na mengine mengi. Naomba shule hii Wizara iithamini kama ilivyokuwa zamani hasa ikizingatiwa kuwa ni shule ya wasichana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Wilaya ya Kwimba leo ni zaidi ya miaka kumi tumetenga eneo la kujenga Chuo cha VETA lakini Wizara imekuwa ikiahidi kila mwaka kuwa kitajengwa lakini imekuwa ni hadithi isiyoisha. Naomba katika bajeti hii nipate ufumbuzi wa ahadi ya siku nyingi ya Wizara ya ujenzi wa VETA Kwimba au niambiwe nitumie mbinu gani ili ujenzi huo uanze. Chuo hicho kinahitajika sana, mimi kama Mbunge kwa zaidi ya miaka 20 nimekuwa nikiomba ujenzi wa Chuo cha VETA Kwimba, nimekuwa nikitumia lugha ya kiungwana, naomba na Wizara nao wawe waungwana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, FDC Malya. Tunacho Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Malya ambacho ni kama Wizara imekitelekeza, kinaendeshwa isivyo au kama siyo cha Serikali. Chuo hiki nilipendekeza kama Serikali inaona imeshindwa kukihudumia kupitia Wizara ikifanye kiwe Chuo cha VETA kwani shughuli inazozifanya zinafanana na za Chuo cha VETA. Huo ni ushauri wangu endapo Wizara haijajipanga kujenga chuo, miundombinu iliyopo Malya inajitosheleza, inachotakiwa ni uboreshaji, lipo eneo kubwa la kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, hayo niliyoyaomba ya shule ya wasichana ya Sumve, VETA na FDC Malya yatazamwe kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, katika jimbo langu tunayo shule ya sekondari ya wasichana ya waliokosa fursa baada ya kupata mimba, kuishia kidato cha kwanza au cha pili inayojulikana kama Arch Bishop Mayala iliyosajiliwa. Mwaka jana Makamu wa Rais alipata nafasi ya kuitembelea ambapo alivutiwa sana na uamuzi huo wa kuanzisha shule hiyo. Nimuombe Mheshimiwa Waziri katika ratiba zake Mkoani Mwanza aitembelee shule hiyo ili ajionee mwenyewe na kutoa ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, suala la ugawaji wa vitabu katika shule zetu za sekondari ni vizuri ukafuata uwiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.