Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Wilfred Muganyizi Lwakatare

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Bukoba Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza napongeza hotuba iliyotolewa na Mheshimiwa Komu, Waziri wetu Kivuli, lakini pia napongeza hotuba au mchango uliotolewa na dada yangu, Mheshimiwa Riziki pamoja na Mheshimiwa Mwaifunga pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Kivuli, Mheshimiwa Cecil Mwambe.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwelekeza ndugu yangu, Mbunge mwenzangu, Mheshimiwa Kingu, ajaribu kuchukua hotuba ya Upinzani ukurasa wa 42 na 43 atajua namna gani brain ya Oppostion ilivyo. Hili ndilo tatizo, kwamba watu wengine wanasoma hivi vitabu kwa kutumia miwani ya mbao. Hilo ndilo tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba watu wote wenye vitabu vya rangi hii; na kaka yangu Mheshimiwa Mwijage, asome vizuri hotuba ya Upinzani pamoja na Kamati ya Viwanda na Biashara, zitamusaidia sana. Acha maneno ya sound hizi nyingine zinazotoka kwingine…

KUHUSU UTARATIBU. . .

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naamini bado dakika zangu tisa zilizokuwa zimebaki, ziko palepale. Matatizo yote haya nafikiri ambulance zitatoa watu roho hapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua wazi kabisa, kaka yangu Mheshimiwa Mwijage, Waziri wa Wizara hii; Wizara hii ndiyo mlezi wa wafanyabiashara, ni mlezi wa watu wanaotaka kufanya biashara, ni mlezi wa watu wanaotaka kukuza biashara, ni mlezi wa watu wanaotaka kuweka mitaji katika biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mahali huwa najiuliza kwamba wakati wa vikao vya cabinet kama kweli Mawaziri mnamsaidia Mheshimiwa Rais inavyopasa. Kwa sababu pale inapokuja kutokea kila Wizara kuendesha operesheni zake kivyake vyake bila coordination kuonekana kama Serikali inafanya kazi, mimi huwa nachanganyikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tunapozungumza, wafanyabiashara wakijua fika kwamba Wizara hii ndiyo mlezi, wanakamatiwa mali, wengine wanakamatiwa magari yakiwa barabarani, eti kwa sababu kuna gari ambayo imesimama miaka sita haijalipa road license.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kituko kimemgusa Msukuma mmoja alikuwa amepakia samaki anatoka Mwanza anakwenda Dar es Salaam, akasimamishwa na Maaskari gari likapelekwa kituoni. Msukuma akalia akasema kwamba pesa niliyonayo yote imemalizika katika kusafirisha; niko tayari kulipa faini pindi nitakapofikisha mzigo wangu mahali unapokwenda, lakini walimng’ang’ania na samaki wakaoza akaenda kupaki hiyo gari katika kituo. Hii ukiangalia kwa undani ni kukosa busara na akili ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Wizara kama mlezi mama wa wafanyabiashara, naomba ichukue jukumu lake kama mlezi wa wafanyabiashara. Hivi sasa mazingira siyo rafiki kwa wafanyabiashara. Policies zinabadilika badilika, haieleweki! Yaani siku hizi watu wanakaa kwenye TV na redio, hawajui kiongozi akiwa kwenye ziara atazungumza kitu gani. Lolote linaweza likabadilika! Policies zinabadilika! Wafanyabiashara hawako tayari kuwekeza kwenye mazingira ambayo hayaeleweki kwamba leo na kesho itakwendaje? Naomba hili mliangalie sana. Play role ya kulea wafanyabiashara, mazingira yawe rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Bukoba, wafanyabiashara, wajasiriamali waliowekeza kwenye mashine za unga, TFDA wamekwenda pale na kufunga biashara ya kusaga unga kwa sababu tu wanataka watu wajenge ma-godown au wajenge nyumba kubwa za kuweka mashine kwa kutumia matofali.

Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli hiyo imesababisha Bukoba Mjini unga umepanda bei kwa sababu ya maamuzi ya mtu mmoja tu. Ukienda Halmashauri, wale wafanyabiashara wanashindwa kujenga hayo ma-godown kwa sababu hawajapata vibali toka Halmashauri ambayo ni owner wa eneo hilo. Sasa unakuta maamuzi ya mtu mmoja tu yanakuwa tatizo kwa watu wengi na mazingira yanakuwa siyo rafiki kwa wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Mwijage, watu wangu wa Kashai, Soko Kuu, Rwamishenye, pale sokoni Kibeta Uswahilini wanataka awaeleze, pesa iko wapi? Pesa imekwenda wapi? Mzunguko wa pesa mbona mbaya? Mtu anapanga nyanya mshumaa, ntongo, yaani inaanza ikiwa Azam, inabadilika rangi inakuwa Yanga, mwisho inakuwa Simba na matokeo yake hakuna anayeinunua ntongo tena. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanataka kujua pesa inakwenda wapi, mbona kodi wanalipa? Nitaomba kwa lugha nyepesi awaeleze wafanyabiashara pesa imekwenda wapi? Inafungiwa wapi? Kufuli gani hili? Ni kubwa kiasi gani linafungia hela? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yupo kiongozi mmoja aliwahi kusema kweli kwamba jero itaitwa mia tano; buku itaitwa 1,000; na mtu mwenye kifua cha kukaa Dar es Salaam kama atavuka mwezi wa Saba, basi huyo ni mwanaume. Nafikiri huko ndiko tunakoelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, benki sasa hivi zinashindwa hata kukopesha, hata uwe na nyumba yenye hati, kwa sababu hata zile watu walizokopesha kwa kutumia collateral za nyumba, haziuziki; benki zinashindwa hata kuziuza. Pesa haizunguki! Pesa haipo!

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwijage, akija hapo mbele atueleze, pesa iko wapi? Watu wafanyaje? Waipatie wapi? Waifukuzie wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wa Bukoba walio-supply taasisi za Serikali wanadai mpaka sasa hivi zaidi ya shilingi milioni 900 kuelekea shilingi bilioni moja; na kwa bahati mbaya wafanyabiashara hawa, wengi ndiyo wale waliokuwa na nyumba zilizopigwa na tetemeko. Sasa walitarajia hata kale kadogo kalikochangwa na wadau angalau wangekatiwa kidogo. Sasa hivi ni maskini, hawawezi kukopa kwa sababu hawana collateral, nyumba zina nyufa lakini pia hawawezi kukopeshana kwa sababu hela iko mikononi mwa taasisi za Serikali, hazijawalipa, wanafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, pia atambue Bukoba imepigwa tetemeko la mwezi wa Kumi; juzi hapa limepiga lingine, mafuriko yamepita! Nashukuru Mheshimiwa Profesa Muhongo atakwenda Bukoba na wataalam wake kuweza kutoa ripoti ya athari ya tetemeko na aina ya miamba, uchunguzi wao. Hiyo itakuwa ni taarifa ya kuhusu tabia za miamba ili tuweze ku-project watu wa Bukoba kwamba wanaweza kujenga nyumba za namna gani? Tuletewe michoro ya Japan, ya Australia, ya Paris ili tupewe ushauri wa nyumba za namna gani zinazoweza kuhimili matetemeko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, huyo ni Mheshimiwa Profesa Muhongo, nampongeza sana. Kwa upande wa Mheshimiwa Mwijage, hizi athari za wafanyabiashara ambao sasa, yaani kwanza Bukoba imeshakuwa dangerous zone… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kushiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lwakatare, ahsante.