Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Na mimi niungane na wenzangu kutoa pole sana kwa wafiwa wote waliofiwa na watoto wetu wale waliofariki kule Arusha kwa ile ajali.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nielekeze mchango wangu katika upande wa umwagiliaji maana najua hapa ndio kwenye maisha yetu Watanzania wote. Ukiangalia tafiti ambazo zimefanyika za REPOA na ESRF zote zimeonesha kwamba, Tanzania kama tunataka kutoka katika umaskini lazima msisitizo uwe katika kilimo cha umwagiliaji, kama hatukuweka msisitizo katika kilimo cha umwagiliaji hata tukitengeneza barabara kiasi gani tutakuwa tunajidanganya, maana nchi ambayo haiwezi kujilisha haina heshima yoyote hapa duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata Jarida la Economist la 2012 linatueleza jinsi ambavyo Tanzania ni nchi ya kumi na moja duniani ya kuwa na maji mengi ambayo ni maji yale tunasema maji ya baridi au maji ambayo hayana chumvi. Ukiangalia Ziwa Tanganyika peke yake lina asilimia 17 ya maji yote masafi katika ulimwengu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiweka na Mito ya Pangani, Rufiji na Maziwa mengine tuliyonayo hakika utajua kwamba Tanzania tuna utajiri mkubwa sana wa maji. Licha ya maji tuna mabonde makubwa sana yanayofaa kwa umwagiliaji. Tafiti pia zimeonesha na Mheshimiwa Waziri amezungumza, kwamba tuna mabonde hekta milioni 29.4 yanayofaa kwa umwagiliaji. Lakini inasikitisha kwamba mpaka sasa ni hekta 468 tu ambazo zimejengewa miundombinu, na hiyo ni kama asilimia mbili tu ya sehemu yote ambayo imejengewa miundombinu ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunauliza hivi kweli Watanzania tunatakaje kuondokana na umaskini wakati hatutilii mkazo zile sekta ambazo zitatutoa kwenye umaskini? Unaangalia unajua je, ni kwamba hatutaki kutumia akili zetu tuko tayari tukaombe misaada kutoka nje, tukachukue misaada kutoka nje? Tungekuwa kama nchi za huko Ethiopia, Sudan, hivi nchi hii si tungekuwa tumeshakufa wote. Kwa hiyo, ninachosema, ni kwamba nchi yetu bado hatujatumia busara, hekima na akili Mungu alizotupa kwa ajili ya kuona vipaumbele vyetu viwe katika nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kilimo kwa mwaka 2010 kilikua kwa asilimia 2.7 lakini mwaka jana kimeshuka hadi asilimia 1.7, tatizo unaambiwa uhaba wa mvua, ni aibu. Maji yamejaa tunazungumzia uhaba wa mvua kwa nini akili zetu zote tunapeleka kwenye mvua? Haya mambo ya kilimo cha umwagiliaji tumezungumza miaka nenda, rudi tangu kilimo kwanza, lakini mpaka leo tuna tatizo hilo, sijui tusemeje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija Jimbo la Same Mashariki Mungu ametujalia tuna mito mikubwa ukichukulia Nakombo, Hingilili, Saseni, Yongoma lakini mito yote hii inakwenda baharini, mito yote inapita kwenye vichaka. Tumeomba tujengewe mabwawa ili akinamama ambao wengi ndio wanaolima wapate nafuu, akinamama ndio watekaji maji wengi ndio wanahangaika. Watoto wetu wa shule wako wengine boarding wanafuata maji kilometa nzima au mbili, ugonjwa wa UTI haupungui kwenye boarding schools, ugonjwa wa kuharisha watoto, akinamama kila siku wako hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba bajeti ya Wizara ya Afya iongezwe. Tunasema hapa Wizara ya Afya iongezewe pesa kumbe yote inaenda kutibu kuharisha, matumbo, kwa nini tusingeboresha maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nasema, nchi yetu tukiendelea kwa mtindo huu, tusipojali maji na hasa tuseme maji ya kumwagilia akina mama, mboga mboga, akina baba mashamba, vijana wetu hasa kule Jimbo la Same Mashariki kilimo cha tangawizi ambapo LAPF wanataka wajenge kiwanda kikubwa, hakiwezi kufanya kazi kama tangawizi haitapata maji ya umwagiliaji. Kwa hiyo naomba wenzetu walione hilo tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishuke kuangalia nini kinachotufanya Tanzania tunarudi nyuma. Hata tukisema bajeti ya Wizara ya Maji iongezwe, ambavyo naunga mkono, je, ubadhirifu ambao uko katika Wizara ya Maji nao tutaufanya nini? Ukiangalia ukaguzi wa ufanisi wa ujenzi wa miradi ya maji hasa ya mijini kwa mwaka 2010/2011 na mwaka 2013/2014 imeonesha katika miradi tisa, miradi nane iliongeza gharama zake kuanzia asilimia 10 mpaka asilimia 229 sawa na ongezeko la shilingi bilioni 30. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa je, Wizara ikiongezewa bajeti sasa hivi itatuhakikishiaje kwamba haya maji yatawafikia hasa akina mama ambao katika Tanzania wako asilimia 51 na na kati yao asilimia 60 wako vijijini? Tupunguze bajeti ya kwenda huko kwenye miji ili asilimia 30 iende mjini, 70 iende vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nasisitiza kwamba tungeanzisha Wakala wa Maji Vijijini badala ya Mfuko wa Maji ili tuwe na uhakika maji kweli yanaenda vijijini na kwamba maji yatawafikia wananchi vijijini. Kinyume cha hapo fedha itawekwa kwenye mfuko halafu hela zitakwenda ndivyo sivyo. Kwa hiyo, ningeomba sana, hata kama tukisema tunaweka umeme mwingi, barabara za lami kama akina mama vijijini watakuwa wanahangaika na maji, hakika nchi hii hatutaendelea. Akina mama ndio wenye uchumi mkubwa katika nchi hii, ndio wakulima wadogo wadogo. Tume-fail katika mambo mengi lakini hebu tuwape akinamama chance, tupeleke maji vijijini, tuanzishe huu Wakala wa Maji Vijijini ili tuwe na hakika hela kweli inaingia huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapo.
Ahsante.